ANGA LA WASHENZI SEHEMU YA 1

ANGA LA WASHENZI -- 001 Simulizi_za_series Mvua ilikuwa inanyesha sana. Hali ya hewa ilikuwa baridi ikiambatana na upepo wa wastani. Watu wengi hawakwenda kazini, na hata wanafunzi pia wakitega shule kwa kisingizio cha barabara kufurika maji. . . . Pengine watu hawa walikuwa na hoja kutokana na miundombinu dhaifu ya jiji la Dar es Salaam ambayo haiwezi kurandana na mikikimikiki ya mvua. Ila kwa mwanaume Jonathan Mchau, hilo halikuwa na mashiko kamili kwani yeye alikuwa ofisini akiendelea na kazi zake kama ilivyo ada. . . . Ni ndani ya chumba kidogo kinachopatikana maeneo ya mwenge. Kwenye kuta za chumba hicho kulikuwa kumetundikwa picha kadhaa za kuchorwa kwa mikono. Picha hizi zilikuwa zimeundwa kimafumbo lakini pia zikibeba utajiri wa tamaduni za Afrika kwa ujumla. . . . Kama ungelipata nafasi ya kutembelea hapo basi ungepatwa na kamshangao kidogo kutazama picha hizo zilizofumwa na rangi mbalimbali za kuvutia kiasi kwamba ukasahau kuwa eneo hilo limepakana na barabara yenye makelele ...