JOANA ANAONA KITU USIKU SEHEMU YA 1
*JOANA ANAONA KITU USIKU!* 01
*Simulizi za series inc.*
Jua linapozama, Joana hukosa raha. Si kwasababu anaishi Brussels, Ubelgiji, kipindi hiki cha baridi, la hasha! Bali kwasababu usiku huwa mzito sana kwake.
Punde giza linapoingia, anapoteza amani na mwili wake unaanza kutetemeka kwa hofu. Na zaidi pale ambapo kila mtu akishalala, machozi huanza kumbubujika na hujifunika shuka gubigubi.
Si kwamba Joana ni mwoga kukithiri. Hapana. Joana huona watu usiku. Watu waliokufa, watu wanaotisha na kuogofya!
Habari hii ilianzia miaka kumi na mitano huko nyuma kwenye jiji la Berlin, Ujerumani. Joana alikuwa anasoma huko chuo kikuu akichukua fani ya sheria.
Alikuwa ni msichana mrembo na mwenye kuvutia kwa namna alivyokuwa anajipangilia nguo, maneno na hata hoja.
Alikuwa na marafiki lukuki, lakini zaidi mpenzi wake mwenye asili ya Brazil, akiitwa Moa Santos. Aliyekuwa anampenda na kumheshimu sana.
Mara kadhaa Joana alikuwa anaonekana na mpenzi wake huyo wakirandaranda maeneo ya chuo wakishikana mikono.
Kama ingelikuwa si vipindi kutofautiana, Moa alikuwa anasomea mambo ya ugavi, basi wangelikuwa wanaonekana pamoja muda wote, kuanzia asubuhi mpaka jioni kabla hawajaenda hostel.
Moa hakuwa mbahili wa tabasamu wala cheko. Hakuwa na sababu yoyote ya kununa wala kuyaona maisha machungu.
Baba yake alikuwa mfanyakazi wa kampuni kubwa ya simu ya Samsung, huko Korea. Na mama yake alikuwa mwanasiasa nguli huko Ubelgiji.
Kabla hajalia shida, babaye alikuwa tayari ashamfikia na kumkabidhi pesa, ama basi mamaye.
Ila leo hii Joana ni mpweke, macho yamemvimba muda wote. Uso wake umekuwa mweusi na mhaba wa furaha. Amekuwa mtumwa wa kujificha, kukwepa wengine na kujiona mtupu.
Maisha yalibadilikia wapi?
Punde baada ya kumaliza muhula wake kwanza wa masomo chuoni, Joana alisafiri kwenda Rio de Jenairo pamoja na mpenzi wake, Moa.
Lengo la safari hii ilikuwa ni kwenda kutambulishwa kwa kina Moa kama mchumba mtarajiwa. Mwanamke ambaye Moa anampenda zaidi.
Walipofika Rio, Joana akatembezwa kwanza jiji lote la Rio. Akafurahia sana kwani alipenda sana kutembea na kujifunza mambo mapya.
Alikutana na wazazi na ndugu wa Moa, akatambulishwa kama mchumba. Alikaribishwa kwa tafrija waliyokula na kunywa kwa kusaza wakifurahia haswa.
Familia ya Moa ilikuwa ni ya watu wa kati. Hawakuwa na uwezo wa juu wala hawakuwa duni. Baba yake Moa, mzee Santos alikuwa mkulima mfanyabiashara.
Mama alikuwa mwanamke tu wa nyumbani akilea familia. Umri wao ulikuwa umeenda sana, Moa akiwa ndiye mtoto wao wa mwisho.
Ila kuna jambo lilitokea kumtatiza Joana na akataka kulipatia ufumbuzi. Jambo hilo lilikuwa linamhusu mama yake Moa, bi Lusia.
Mwanamke huyo alikuwa na macho yote mabovu, yenye viini vilivyomezwa na ute kama maziwa. Upande wake wa kushoto wa uso ulikuwa una alama ya kushonwa kana kwamba alipigwa panga.
Lakini mbali na hayo, alikuwa mchangamfu, tena asiyeonyesha kasoro yoyote kwenye kuona. Alishika alichokitaka, na kutenda alichokitaka.
Hili likamshangaza sana Joana. Aliwezaje kufanya haya?
Alimuuliza Moa, Moa akaonyeshwa kutofurahishwa na hilo swali. Joana naye akahisi vibaya kwani hakutaka kumkwaza Moa.
Kwa namna moja ama nyingine, Joana akahisi huenda Moa amehisi amemdharau mamaye, kitu ambacho hawezi kufanya kabisa.
Hivyo basi akaamua kupotezea mada hiyo.
Baada ya juma moja aliaga kuondoka Brazil aende kwao Ujerumani kabla ya kurudi tena chuo. Basi kama zawadi, mama Moa akamkabidhi Joana bangili.
Ilikuwa bangili ya bati inayometameta. Bangili hii ilikuwa ina maandishi madogomadogo ambayo Joana hakuyaona.
Pasipo kujua, siku hiyo Joana akawa ameingia agano asilolijua.
Alifurahia sana zawadi hiyo na akaitumia kuwaonyesha wenzake huko chuoni akijitapa kwa namna gani alivyopendwa na kutunukiwa na mama mkwe wake mtarajiwa.
Aliipenda sana bangili yake, si tu ilikuwa nzuri bali ilikuwa inamkumbusha upendo wake kwa Moa.
Lakini kuna jambo lilikuwamo ndani bangili. Na jambo hili lilikuwa linatukia usiku tu. Bangili hii ilikuwa inawaka pindi inapofika saa nane usiku.
Zaidi, ilikuwa inamwamsha Joana pasipo kujua na kumfanyisha mauaji ya kutisha!
Punde Joana aliporudi chuoni, ndani ya mwezi mmoja, wanachuo nane wakauawa kwa mtindo mmoja wa kifo.
Wote waliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani. Mauaji haya yakaamsha taharuki kubwa chuoni. Hata ikapelekea kuundwa kwa ulinzi shirikishi kumng'amua muuaji.
Siku moja Joana aliamka, hana hili wala lile, akaandaa kifungua kinywa chake kabla hajaenda darasani.
Alikuwa amevalia gauni jeupe la kulalia miguuni akiwa amejivesha viatu vyepesi vya chuichui.
Akiwa anapika, mara mwenzake anayelala naye chumba kimoja, kwa jina aitwa Lisa Moan kutoka Uingereza, anafunika mdomo wake kwa kiganja akitoa macho.
Aliona kitu mgongoni mwa Joana. Alipiga kelele akimshtua Joana akisema:
"Joana nini hiko mgongoni mwako?"
Joana akakurupuka na kuruka. Alidhani buibui. Alijikuta anavua nguo yake kwa upesi mno na kuitazama.
Loh! Ilikuwa imelowa damu!
Alishangaa damu ile imetoka wapi na ilhali hakuwa na jeraha. Iliwatia hofu mno. Lakini wakamezea hilo jambo na wakakubaliana litakuwa siri.
Siku hiyo baadae wakiwa darasani, wakapokea taarifa zingine za msiba. Alikuwa amekufa mwanafunzi mwingine. Tena chumba kinachofuatia na cha wakina Joana.
ITAENDELEA........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni