DIMBWI LA HUBA SEHEMU YA 2
SIMULIZI: DIMBWI LA HUBA
MTUNZI: ALLY MBETU
SEHEMU YA PILI
Mama yake baada ya kumkosa mchana wakati wa chakula, baada ya kumuona
amerudi alimfuata kutaka kujua alikuwa wapi. Alipoingia chumbani alishtuka
hali aliyomkuta nayo mwanaye.
“Sued mwanangu mbona hivi! Unaumwa?”
“Hapana.”
“Sasa mbona upo hivyo?”
“Basi tu mama natamani kufa.”
“Kufa?”
“Ndiyo mama.”
“Kwa nini?”
“Nina imani bila Zulfa siwezi kuishi?”
“Zulfa ndiye nani?”
“Mwanamke niliyemchagua kuwa mke wangu.”
“Sasa huyu Zulfa kafanya nini?”
“Nimeambiwa anataka kwenda nje kusoma.”
“Sasa tatizo nini?”
“Sicho tulichokipanga, mzee wake ana roho mbaya aliona kumuoa mwanaye
ningefaidi.”
“Huyo Zulfa anakaa wapi?”
“Kayenzo.”
“Kayenzo, mtoto wa nani?”
“Kipepeo.”
“Yule tajiri wa Kayenzo?”
“Ndiyo mama.”
“Mwanangu mbona unataka mazito, kwanza baba yako akisikia unafikiri
kutakuwa na usalama? Unataka kumchokoza baba yako? Kwanza mapenzi
umeyaanza lini mpaka kufikia hatua ya kupanga na ndoa wakati huna kazi wala
chumba.”
“Ningejua nitamuweka wapi na anakula nini.”
“Mwanangu achana na wazo hilo, muda ukifika utampata msichana mwingine
mzuri kuliko Zulfa.”
“Mama hakuna mwanamke mwingine atakayempiku Zulfa, mama sikuwahi
kupenda na sitapenda tena zaidi ya Zulfa.”
“Basi ndiyo hivyo amekwenda kusoma na akirudi atatafuta msomi mwenzake
wewe wa kidato cha nne umeula wa chuya.”
“Mama wee fanya utani, mimi bila ya Zulfa siwezi kuishi.”
“Umekula?”
“Kuna faida gani ya kula wakati sina furaha.”
“Mwanangu kula, kila kitu niachie mimi.”
“Utafanya nini?”
“Mimi najua, kula kwanza.”
Sued alikubali kula huku akisubiri kujua mama yake anataka kufanya nini ili
kuweza kumpata Zulfa.
***
Upande wa pili, Zulfa wiki mbili kabla ya kurudi shuleni moyo wake ulikuwa
na shauku ya kumuona mpenzi wake Sued, kiumbe aliyeuteka moyo wake.
Wiki mbili kwake ilikuwa kama miaka ishirini, akiwa amekaa chumbani kwake
akicheza gemu kwenye laptop yake, mama yake alikwenda chumbani kwake
akiwa na uso wa furaha.
“Hodi mwanangu.”
“Karibu mama,” Zulfa aliacha kucheza gemu na kumtazama mama yake,
akakutana na uso uliojaa furaha.
“Mama mbona unaonekana una furaha?”
“Ni kweli mwanangu nina habari njema kwako.”
“Habari gani mama?”
“Ile nafasi aliyokuwa akiitafuta baba yako imepatikana.”
“Nafasi! Nafasi gani?”
“Ya kwenda kusoma nje.”
“Nje wapi?”
“Ina maana huna taarifa kuwa kuna nafasi ya kwenda Sweden?”
“Ndiyo najua.”
“Basi mwanangu baada ya miezi miwili na nusu unatakiwa uondoke kwenda
kuanza masomo.”
“Nitakwendaje wakati sijamaliza shule?” Zulfa alishangazwa na taarifa zile za
ghafla.
“Hiyo siyo sababu, elimu yako haihitaji kumaliza shule unaweza kujiunga tu.”
“Lakini mimi sikupanga kwenda sasa hivi.”
“Hiyo siyo juu yako, wewe ni mtoto tu unatakiwa kukubaliana na
kinachoamriwa na wazazi wako.”
“Sawa, lakini mimi naona hakuna umuhimu wa kwenda kusoma nje kwani
elimu ya sasa nchini imekuwa sana.”
“Acha ujinga huoni watoto wa vigogo wote wanasoma nje?”
“Mbona Wazungu wanakuja kusoma chuo kikuu huku?”
“Zulfa sitaki kuulizwa maswali ya kitoto, mi nilifikiri ungefurahi kusikia
umepata nafasi adimu ya kwenda kusoma nje! Nafasi yenyewe baba yako
kapoteza fedha nyingi ili kuhakikisha unaipata hasa baada ya kuonesha una
uwezo wa kielimu kuliko ndugu zako wote. Tena mimi mama yako ndiye
niliyekuwa nikimsumbua kila siku, hata sehemu aliyokata tamaa nilimpa moyo
na hatimaye imepatikana.”
“Lakini mama mimi sasa hivi siendi popote mpaka nimalize elimu yangu si
bado miezi sita tu?”
“Hiyo miezi sita ya kwako, lakini yetu unatakiwa uondoke haraka ili kuwahi
mwanzo wa masomo mapema.”
“Mama mi siendi.”
“Nini?” mama Zulfa alishtushwa na kauli ya mwanaye.
“Nasema siendi mpaka nimalize shule.”
“Zulfa unatania au unasema kweli?”
“Nasema kweli mama, siendi popote mpaka nimalize shule.”
“Zulfa hebu acha utani mama.”
“Mama nasema kweli wala sitanii, siendi popote mpaka nimalize shule, kama
mlijua hivyo hakukuwa na haja ya mimi kusoma mwaka huu.”
“Hayo unayosema utakuja kumueleza baba yako?”
“Nitamueleza tu mama.”
Mama Zulfa alitoka chumbani kwa binti yake huku akiwa amepoteza furaha
yake na kumshangaa mwanaye kugoma kwenda kusoma nje ya nchi na kutaka
kuendelea na elimu ambayo siku zote ilionekana ya kubabaisha japo kuna shule
za kulipia zilikuwa zikijitahidi kidogo.
Aliamini kinachomsumbua mwanaye ni hali ya mazoea, kuzoea mazingira ya
shule na mashoga zake. Lakini aliamini kama angemuelewesha faida ya kwenda
kusoma nje bila kutumia nguvu wala kulifikisha suala hilo kwa baba yake
angemuelewa.
Chumbani, Zulfa baada ya kutoka mama yake alijikuta akipoteza furaha ya
muda mfupi aliyokuwa nayo ya kuomba muda uende haraka ili aende kuonana
na mpenzi wake Sued. Taarifa ya mama yake iliivuruga furaha yake yote kwa
kumlazimisha kwenda kusoma nje.
Moyoni aliichukia safari ile ya kwenda kusoma nje, kitu alichokitaka mbele
yake ni penzi la Sued na si kingine kwa wakati ule. Aliapa kupigana kwa
nguvu zote ili amalize kipindi kile ndipo ajue atafanya nini.
Jioni mama yake kabla ya kufikisha ujumbe wa Zulfa kwa baba yake,
alimfuata tena chumbani kwake na kumbembeleza:
“Mwanangu Zulfa bado una msimamo wako?”
“Mama mimi siendi popote bila kumaliza muda wangu uliobakia.”
“Sikiliza mwanangu, hebu funguka mawazo. Safari hii ina faida kubwa sana
maishani mwako.”
“Sijakataa, ila mpaka nimalizie muhula wa mwisho. Nimejiandaa kwa ajili
ya kumaliza shule na mawazo yangu yote nimeyaelekeza huko na si nje ya
nchi.”
“Mwanangu hebu nielewe, hii ni nafasi adimu tena nimemlazimisha sana
baba yako, unafikiri atanielewaje?”
“Mwambie miezi sita siyo mingi avumilie nitakwenda.”
“Na masomo nayo yakusubiri?”
“Mlitakiwa mnieleze mapema, nimejifua kuhakikisha mtihani wa mwisho
napata ‘division one’, tena ya alama za juu.”
“Hiyo haina umuhimu kama elimu tuliyokutafutia.”
“Elimu ya hapa kwangu ina muhimu mkubwa, kuna watu tulipinga nani
atamzidi mwenzake, itaonekana nimewakimbia.”
“Hata wakisema, ukirudi utakuwa upo juu kuliko wao.”
“Sawa, lakini mimi siendi.”
“Kwa hiyo upo tayari nimwambie baba yako?”
“Nipo tayari.”
“Haya tusilaumiane.”
“Nitamwambia ukweli.”
Mama Zulfa aliona ushawishi wake umegonga mwamba kutokana na akili za kitoto za mwanaye. Aliamua kwenda kumwambia baba yake huenda akimkemea atabadili msimamo wake.
Mama Zulfa aliona ushawishi wake umegonga mwamba kutokana na akili
za kitoto za mwanaye. Aliamua kwenda kumwambia baba yake huenda
akimkemea atabadili msimamo wake.
Baba Zulfa aliamini ule ni utani wa mwanaye, alijua anamtania mama yake
hivyo hakuwa na wasiwasi na taarifa ile.
Majira ya saa nne usiku baada ya shughuli zote za kutwa, kula na kuoga,
mzee Kipepeo alimtuma msichana wa kazi kumfuata Zulfa aliyekuwa
chumbani amejilaza huku amefura kwa hasira kutokana na taarifa
alizoletewa na mama yake za kwenda kusoma nje ya nchi.
Zulfa alikuja mbele ya wazazi wake waliokuwa wamekaa sebuleni
wakiangalia vipindi vya usiku kwenye runinga. Alipofika, bila kusema kitu
alikaa kochi la karibu na wazazi wake. Mzee Kipepeo aliyaondoa macho
kwenye runinga na kumgeukia mwanaye aliyeonesha hayupo katika hali yake ya
kawaida.
“Zulfa mama,” alimwita kwa sauti ya chini yenye kusikika.
“Abee,” aliitikia kwa sauti ya chini bila kuwaangalia wazazi wake.
“Eti mama kuna nini?”
Zulfa hakujibu kitu, alitazama chini tu kitu kilichomfanya baba yake kumgeukia
mkewe na kumuuliza:
“Mke wangu ni hilihili tu au kuna lingine?”
“Ni hilo tu mume wangu kama kuna lingine aseme mwenyewe.”
“Eti mama hutaki kwenda kusoma nje?”
“Sijakataa ila mpaka nimalize muda wangu uliobakia.”
“Mwanangu elimu ya maana ni nje ya nchi hivyo nafasi hii ni ya dhahabu
mwanangu.”
“Baba nielewe, mimi nipo tayari kwenda kusoma nje lakini nina imani miezi
minne iliyobakia si mingi kwa nini nisimalizie nijue nimevuna nini?”
“Hayo hayana umuhimu tena, kama umepata nafasi hii ambayo tumegombea
watu wengi, tulikuwa watu zaidi ya mia moja, nafasi zilikuwa tano tu, tena watu
maarufu lakini uwezo wangu na nguvu yangu kubwa serikalini tumepata moja
kati ya nafasi hizo chache.”
“Wazazi wangu sijakataa, nimekubali ila baada ya kufanya mtihani wangu wa
mwisho.”
“Sikiliza, kuondoka kwako si ombi bali amri, umebakiwa na miezi miwili, shule
hutarudi tena zaidi ya kujiandaa na safari yako.”
“Kama amri mi siendi.”
“Nini?” baba yake aliuliza kwa sauti ya ukali.
“Nasema siendi popote,” Zulfa alijibu kwa kiburi.
“Kama huendi na hapa uondoke,” baba yake alimtisha.
“Sawa nitaondoka,” Zulfa alizidi kumjeuria baba yake.
“Wewe Zulfa jeuri ya kumjibu hivyo baba yako umeitoa wapi?” mama aliingilia
kati.
“Sijaitoa popote, kwa nini hamtaki kunisikiliza na mimi? Hata kama ni mtoto
nina haki ya kusikilizwa.”
“Sasa nasema hivi shule utakwenda kwa nguvu au kwa hiyari,” baba alitoa
amri.
“Kama mtanilazimisha nitakunywa sumu.”
“Kunywa tu.”
“Sawa, nitakunywa mfurahi.”
“Unajua wewe mtoto unataka kunichezea,” mzee Kipepeo alisema huku
akinyanyuka na kumfuata Zulfa aliyekuwa bado amekaa kwenye kochi. Alipofika
alimshika mkono na kumnyanyua, akamuuliza kwa hasira:
“Wee kinyago unasemaje?”
“Kama nilivyosema siendi mpaka nifanye mtihani wa mwisho,” Zulfa alijibu
kwa kujiamini.
“Etiii,” mzee Kipepeo alimsukuma kidogo mwanaye na kumpelekea kofi zito
lililomrusha nyuma na kujigonga ukutani, akateremka chini ya zulia.
“Pumbavu, wewe ni nani unayeweza kubishana na mimi?” mzee Kipepeo
alisema kwa hasira.
Lilikuwa ni kofi zito lililompata barabara Zulfa, akajigonga ukutani na kuanguka
chini akiwa amepoteza fahamu.
“Mume wangu umefanya nini?” mama Zulfa alishtuka baada ya kushtushwa
na muanguko wa mwanaye.
“Mpumbavu huyu, hawezi kunikosea heshima. Nimepoteza kiasi gani cha
fedha kwa ajili yake?”
“Lakini mume wangu hukutakiwa kuchukua uamuzi mzito kama huu, ona
mtoto ulivyomfanya.”
Mama Zulfa alisema huku akimtazama mwanaye aliyekuwa amepoteza
fahamu huku damu zikimtoka mdomoni na puani.
“Umeua mume wangu,” mama Zulfa alisema huku akilia.
“Nini?” Mzee Kipepeo alishtuka.
“Umemuua mtoto.”
“Nooo, hapana!”
Mzee Kipepeo alimbeba Zulfa na kutoka naye nje hadi kwenye gari na safari
ya kuelekea hospitali ikaanza mara moja, mkewe akiwa ametoka na nguo ya
kulalia, khanga aliyojifunga ilimdondoka bila mwenyewe kujua, hakukumbuka
hata kuvaa viatu.
****
Wakati nyumbani kwa mzee Kipepeo yakiendelea hayo, mjini Sued naye
alikuwa ameuwasha moto. Usiku baba yake baada ya kurudi alielezwa na
mkewe matatizo ya mwanaye. Baada ya kumsikiliza mkewe alitumwa mtu
kwenda kumwita. Sued aliyekuwa amevimba macho kwa kulia, alifika mbele ya
baba yake.
“Vipi wewe?”
Sued hakujibu kitu, alitazama chini baba yake alimuuliza tena.
“Una tatizo gani?”
“Sina,” alijibu kwa sauti ya chini.
“Eti na wewe umekua siku hizi?”
Sued hakujibu kitu, aliinama tu. Kitendo kile kilimuudhi sana baba yake,
akamsogelea na kumtikisa huku akimuuliza:
“Unalia nini?”
Sued bado hakujibu kitu, alihofia kumwambia baba yake yaliyo moyoni
mwake.
“Baba Sued si nimekueleza vituko vya mwanao?”
“Eti una mpenzi?”
Swali lilikuwa zito kwa Sued na kujikuta kwa mara nyingine akikosa jibu,
kitendo kile kilimuudhi baba yake. Kwa hasira alisema kwa sauti ya juu:
“Unasikia wewe ngedere, upuuzi wako sitaki kuusikia tena, haya toka mbele
yangu.”
Sued alirudi chumbani kwake huku akishukuru kutopigwa na baba yake
ambaye alikuwa mkali kama pilipili. Moyoni alijiapiza kuwa atamtafuta popote
mpenzi wake kabla hajaondoka. Japo alikuwa hajawahi kufika Kayenzo lakini
aliapa kuhakikisha anafika hata kuingia katika jumba la mzee Kipepeo ili tu
amuone mpenzi wake Zulfa.
Zulfa baada ya kufikishwa hospitali, alipatiwa huduma ya haraka na kuonesha
alipata mshtuko kichwani baada ya kujigonga ukutani. Alipewa mapumziko ya
siku moja kabla ya siku ya pili kuruhusiwa kurudi nyumbani huku msimamo
wake ukiwa uleule wa kuendelea kusoma na kufanya mtihani ndipo aende Ulaya
kusoma.
Wazazi wake hawakujua mtoto wao hakuwa na hamu ya kusoma kama
alivyosema zaidi ya kukutana na mpenzi wake Sued. Moyoni aliamini kabisa
alichokuwa akikikosa katika maisha yake kilikuwa ni kumpata mtu sahihi
atakayeupokea moyo wake kwa mikono miwili.
Sued alikuwa mwanaume wa kwanza kumteka kiakili, kimoyo na kimwili,
hakuwaza kumkosa kwa ghafla kiasi kile. Aliamini kama atakubali kwenda Ulaya
kusoma tena bila kumuaga lazima atamuona si mkweli na kutafuta mpenzi
mwingine.
Siku zote aliamini mapenzi ya kweli si fedha bali upendo wa dhati toka moyoni
mwa mtu, hata kama angekwenda kusoma nje na kurudi na madigrii mangapi
kama hakuonesha upendo wa dhati kwa Sued hawezi kumkubali na matokeo
yake kuangukia kwa wanaume wasio na mapenzi ya kweli.
Pamoja na umri wake wa miaka 19, alikuwa na ufahamu mkubwa katika
mapenzi. Aliogopa kumpa mtu asiye sahihi moyo wake na mwisho kuambulia
mateso mazito. Katika maisha yake, alipanga kumpa mtu dhamana ya moyo
wake ambaye atakuwa sahihi.
Cha ajabu, kwa nguvu za aina yake alijikuta akimkabidhi moyo wake Sued,
mvulana ambaye kwa muda mfupi moyo wake ulimuamini kwa asilimia kubwa
na kumuona ndiye chaguo sahihi kwake.
Cha ajabu, kwa nguvu za aina yake alijikuta akimkabidhi moyo wake Sued,
mvulana ambaye kwa muda mfupi moyo wake ulimuamini kwa asilimia kubwa
na kumuona ndiye chaguo sahihi kwake.
Kwa kipindi kifupi, alijikuta akitamani kuwa naye kiasi cha kutotamani tena
kuendelea na masomo zaidi baada ya mtihani wake wa kidato cha sita. Alijiona
tayari anafaa kujiamulia maisha yake, hasa katika mapenzi kwa vile alikuwa
tayari anajua zuri na baya pia kuwa na utashi wa kujiamulia kitu akipendacho.
Moyoni alipanga kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha haendi nje kusoma
japo aliamini wazazi wake walikuwa na nguvu kubwa. Kwa muda uliokuwa
umebaki, alipanga kutoroka na kwenda mjini kumfuata Sued ambaye angejua
wafanye nini kwa kuamini angeondoka na kiasi kikubwa cha fedha ambacho
kingewawezesha kuishi sehemu yoyote chini.
Pamoja na kujua hasira za baba yake huku mama yake akijitahidi
kumbembeleza kubadili msimamo wake, lakini hakuwa tayari kumkubalia
mama yake ili wajue kweli amepania kumaliza mtihani wake wa kidato cha sita
uliokuwa umebakia miezi minne kufanyika.
***
Wazazi wake walizidi kumbembeleza aende shule kwa hiyari yake kuliko
kulazimishwa lakini bado Zulfa alishikilia msimamo wake. Baba yake alimueleza
atake asitake lazima atakwenda kusoma. Akaendelea kuwatishia wazazi wake
kuwa kama watamlazimisha basi atajiua. Tishio lile lilimtisha sana mama yake na
kutaka ushauri kwa mumewe kuliko kutumia nguvu nyingi.
“Sasa mume wangu tutafanya nini maana mtoto pamoja na vitisho vyote
bado msimamo wake upo palepale na sasa bado wiki mbili wakati kila kitu kipo
tayari kwa safari, itakuwaje?”
“Mke wangu ni utoto tu unamsumbua, akifika huko atatulia mwenyewe,
kwani wewe ulikuwa na wazo gani?”
“Wasiwasi wangu ni kumpoteza mtoto wetu, si unajua ndilo jicho letu.”
“Ni kweli lakini lazima wazazi tuoneshe msimamo ili mtoto asituendeshe.”
“Utakuwa umesababisha wewe.”
“Kwa nini mke wangu?”
“Ulimlea kama mtoto wa jicho kiasi cha kunikataza hata mimi mama yake
nisimfokee.”
“Lakini mke wangu kumtafutia shule nje kuna ubaya gani?”
“Hakuna ubaya lakini ndiyo hivyo na yeye alikuwa amepanga yake sasa
tutafanyaje?”
“Ile ni tisha toto tu, atatulia mwenyewe.”
Wakiwa katikati ya mazungumzo, Zulfa alitokea na mabegi yake, kitu
kilichowashangaza wazazi wake.
“Wee mtoto unakwenda wapi?” mama aliuliza.
“Shule,” aliwajibu kwa mkato.
“Kufanya nini?” baba mtu aliuliza.
“Kusoma.”
“Wee mtoto una wazimu, hebu rudisha mabegi yako ndani bado wiki mbili
uondoke.”
“Kwenda wapi?” Zulfa alijibu kwa kiburi, kitu kilichowashangaza wazazi wake
na kujiuliza jeuri ile kaitoa wapi.
“Mwanangu Zulfa una nini mama?” mama yake alimuuliza huku akimfuata
alipokuwa amesimama.
“Mama kwa nini hamtaki kunielewa?”
“Kukuelewa kivipi?”
“Nataka kurudi shule nikafanye mtihani japo nina imani nimepoteza vitu
vingi lakini kwa muda uliobakia lazima nitapata chochote, bado dhamira
yangu ya kupata ‘division one’ tena ya juu ipo palepale.”
“Tunajua lakini chonde mwanangu hebu badili msimamo wako kwani elimu
ya nje ni nzuri hata kukuwezesha kupata kazi nzuri popote katika dunia hii.”
“Ni kweli lakini kwanza nimalizie elimu niliyoisotea kwa miaka kumi na tatu,
nawashangaa nyie kwani bado miezi mitatu tu nimalize lakini hamtaki.”
“Sikiliza mwanangu, sisi wazazi wako hatuwezi kukupeleka sehemu
mbaya, tumepoteza fedha nyingi kuipata nafasi hiyo. Nakuomba mwanangu
kipenzi badili uamuzi wako ili uende kusoma,” mzee Kipepeo alimbembeleza
mwanaye.
“Si mnanilazimisha, basi mtapeleka mzoga wangu kwenda kusoma.”
Zulfa alisema huku akielekea chumbani kwake, kauli ile iliwafanya wazazi
wake kugeukiana na kutazamana, kila mmoja akitafuta jibu kwa mwenzake.
“Itakuwaje?” mama Zulfa alimuuliza mumewe.
“Yaani naushangaa ujasiri wa mwanao, sijui ameutoa wapi? Lakini utapoa
tu, bado utoto unamsumbua kwa vile hajui faida ya kile anachokifuata huko
nje.”
“Mume wangu unafanya utani mtoto yupo serious.”
“Sasa unataka tukubaliane na matakwa yake, mtoto siku zote ni kupata amri
ya wazazi wake.”
“Lakini kauli yake ya kupeleka mzoga wake umeichukuliaje?”
“Ni vitisho tu, kwenda nje ndiyo ajiue?”
Zulfa pamoja na vitisho vyote bado wazazi wake hasa baba yake msimamo
wake ulikuwa uleule wa yeye kwenda kusoma nje ya nchi. Aliamini akitumia
kiburi huenda akakosa kila kitu, akaamua kurudi matawi ya chini ili wazazi
wake waamini amekubali kwenda kusoma na yeye kupata nafasi ya kutoroka
kumfuata Sued mjini.
Alitoka chumbani na kuwafuata wazazi wake waliokuwa wamekaa sebuleni
wakiwa hawajui wafanye nini baada ya msimamo mkali wa mtoto wao,
kitu kilichowachanganya sana. Kama isingekuwa amelipa fedha nyingi basi
wangekubaliana na matakwa yake.
Wazazi wake walipomuona akisogea mbele yao bila mabegi, walinyamaza
na kumtazama mtoto wao anataka kusema nini. Zulfa alipofika mbele ya
wazazi wake alipiga magoti, kitu kilichowashangaza na kujiuliza kwa nini
anafanya vile.
“Baba,” alianza kumwita baba yake.
“Naam mwanangu,” baba yake aliitikia kwa shauku ya kutaka kujua mtoto
wake anataka kusema nini.
“Mama,” alimwita pia mama yake.
“Abee mwanangu.”
“Wazazi wangu naomba mnisamehe sana kwa yote niliyoyafanya kwa
kuwakosea heshima kwa kukataa mlichonitafutia. Naomba radhi sana wazazi
wangu kwa kuwakosea kwa kiasi kikubwa.”
“Tumekusamehe mtoto wetu, pia nilifurahi sana kusikia kauli yako na
kugundua kosa lako hakika umekuwa mwenzetu,” Mzee Kipepeo alisema akiwa
amejaa tabasamu pana.
“Hata mimi mwanangu sijawahi kupata furaha ya ajabu kama leo yaani
nimefarijika sana kama siku niliyojifungua na kukuleta duniani, asante
sana mwanangu kwa kutambua thamani yetu kwako,” mama Zulfa alisema
akimkumbatia mwanaye huku machozi yakimtoka.
“Wazazi wangu najua kiasi gani nimewavunjia heshima, najua kiasi gani
uamuzi wangu ulivyowachanganya. Kuanzia sasa hivi wazazi wangu nimekubali
kwenda kusoma nje ya nchi.”
“Asante mwanangu kwa kukubaliana nami,” mzee Kipepeo alimkumbatia
mwanaye aliyeanza kumnyima raha.
“Basi wazazi wangu naomba nikapumzike.”
“Hakuna tatizo mama kapumzike.”
Zulfa alirudi chumbani kwake akiwa na furaha baada ya mpango wake kwenda
kama alivyotaka kwa kuwapumbaza akili wazazi wake ili wiki mbili zilizobaki
aweze kujipanga na kutoroka.
Baada ya kuondoka, wazazi wake walikuwa na furaha sana, mzee Kipepeo
akamwambia mkewe:
“Unaona eeh! Tungelegeza angetupanda kichwani.”
“Siamini yaani mwanangu leo kanifurahisha sana.”
“Wacha nifike mjini mara moja, Zulfa leo alinichanganya sana.”
Mzee Kipepeo alitoka nje kwa ajili ya kwenda mjini na kumwacha mkewe
akiwahimiza wafanyakazi waandae chakula cha mchana.
***
Sued baada ya uzalendo kumshinda aliamua kwenda Kayenzo kumtafuta Zulfa
kabla ya muda wake wa kusafiri. Alipanda malori hadi njia panda ya kuelekea
Kayenzo, haukupita muda mrefu ilipita ‘pick up’ inayoelekea Kayenzo aliomba
lifti na kukubaliwa.
Alifika katika Mji wa Kayenzo majira ya saa tano asubuhi, mji ule alikuwa
mgeni hivyo hakujua mzee Kipepeo anakaa sehemu gani. Alimuuliza kijana
mmoja aliyekuwa akiuza karanga.
“Samahani, eti mzee Kipepeo anakaa sehemu gani?”
“Fuata hii barabara kuelekea ziwani, ukifika tu utakuta jumba la kifahari ndipo
hapo kwa mzee Kipepeo.”
“Asante.”
“Tena mzee Kipepeo huyo anapita.”
Sued alimtazama yule mzee aliyekuwa kwenye gari la kifahari, kisha
alimshukuru yule kijana. Alifuata barabara ya kuelekea ziwani kwa mwendo wa
dakika kama saba na kujikuta akitokea kwenye jumba kubwa lililokuwa na uzio
mkubwa.
Alisimama na kujiuliza atafanyaje ili kuwasiliana na mpenzi wake, alijitahidi
kuuzunguka ule uzio labda atamuona Zulfa au hata mfanyakazi wa pale ili
amuagize. Kwa mbali alimuona mfanyakazi akikatia majani alimwita kwa
kumfanyia:
“Psiiiii.”
Yule jamaa aliacha kukata majani na kusogea kwa Sued.
ITAENDELEA........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni