PENZI LISILO NA MWISHO SEHEMU YA 1
Simulizi: PENZI LISILO NA MWISHO
Mtunzi: NYEMO CHILONGANI
SEHEMU YA 1
“Nahitaji kubadilisha tairi, unaweza kunisaidia kaka?” ilisikika sauti ya mwanaume mmoja akimuuliza kijana aliyekuwa amekaa pembeni kwenye tofali.
“Hakuna tatizo, kuna hela?”
“Kunisaidia tu mpaka hela?”
“Ndiyo! Hakuna msaada bila hela, hasa kwa nyie mnaomiliki magari ya kifahari! Yaani Range Rover SUV, thamani zaidi ya shilingi milioni mia moja, ushindwe hata kunitoa buku teni! Acha masihara.”
“Basi sawa! Nitakupa! Nisaidie kwanza.”
Ukimya ulikuwa umetawala sehemu kubwa ya Posta Feri, watu wachache walikuwa wamesimama pembeni kwa ajili ya kusubiri pantoni waweze kuvuka na kuelekea Kigamboni.
Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa ni saa sita usiku muda ambao si watu wengi waliokuwa wakivuka eneo hilo kwenda Kigamboni.
Gari zuri la thamani, Range Rover SUV nyeusi ilikuwa imesimama pembezoni mwa barabara ya kuingia katika kivuko cha pantoni karibu kabisa na Kituo cha Polisi cha Magogoni.
Halikuwa limeegeshwa kwa makusudi bali kutokana na tairi lake kupata pancha, dereva hakutaka kuendelea na safari, ilikuwa ni lazima kubadilisha tairi na kuweka tairi jingine kabla ya kuendelea na safari yake.
Mwanaume huyo mwenye mwenye hilo gari ambaye alikuwa Mwarabu, Razak Mahmoud alisimama pembeni ya gari hilo akimwangalia jamaa aliyekuwa akihangaika kutoa tairi la gari lake kwa ajili ya kuweka jingine.
Muda wote, Razak alionekana kuwa na haraka mno, kila wakati alikuwa akiangalia saa yake huku akitembea huku na kule, kwa kumwangalia harakahara ilikuwa ni rahisi kujua kwamba alikuwa na uharaka wa kwenda kule alipotaka kwenda.
“It’s impossible, I have to see him right now!” (haiwezekani, ni lazima nimuone sasa hivi!) alisema Razak huku akionekana kama mtu aliyechanganyikiwa.
Japokuwa kijana yule aliyekuwa akimsaidia alijitahidi kufanya kazi hiyo kwa haraka lakini kila alipomwangalia, aliona akiifanya kazi hiyo taratibu sana, alitamani kumuharakisha, amalize haraka ili aendelee na safari yake lakini kufanya hivyo lilikuwa jambo gumu.
“Vipi?” aliuliza.
“Ndiyo naendelea kiongozi, nitamaliza sasa hivi,” alijibu jamaa huyo.
“Hivi Kigamboni kutakuwa na bodaboda niende na kuacha gari hapa?”
“Sasa hivi?”
“Ndiyo!”
“Mmh! Sidhani, na kama zitakuwepo inabidi uwe makini tu, si unajua usiku una mambo mengi,” alisema kijana huyo.
“Kwa nini?”
“Kwani wewe unataka kwenda wapi?”
“Mji Mwema!”
“Kuna nini usiku wote huu? Au ndipo unapoishi?”
“Hapana! Kuna mtu nakwenda kumcheki mara moja,” alisema Razak.
Muda ulizidi kusonga mbele, ilipofika saa sita na dakika arobaini usiku, tayari kijana yule alimaliza kufanya kazi aliyokuwa akiifanya na hivyo kulipwa fedha aliyotaka kulipwa na kuondoka zake.
Alikuwa amekwishajiandaa tayari kwa kuvuka kivuko hicho, kitu kilichomshangaza ni kwamba bado geti lilikuwa limefungwa. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, ikambidi ateremke na kwenda kwenye kidirisha na kuuliza kilichokuwa kikiendelea, akaambiwa kwamba ilikuwa ni utaratibu wa kivuko kila ifikapo saa sita usiku, kufungwa kwa saa moja kisha baadaye safari kuendelea.
“Kwa hiyo mpaka saa saba?”
“Ndiyo!”
“Sawa.”
Razak akarudi ndani ya gari na kukaa. Kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, mambo aliyokuwa akipitia yalimpa changamoto iliyomfanya kuchanganyikiwa mno.
Alitoka katika familia ya kitajiri, alipata kila kitu alichokihitaji, maisha mazuri, kubadilisha magari na kufanya mambo yote aliyokuwa akiyataka, lakini pamoja na hayo yote, bado mapenzi yaliusumbua moyo wake.
Aliyekuwa akikisumbua kichwa chake alikuwa msichana Sabrina tu, msichana aliyetokea kumpenda lakini ndiye kila siku alikuwa kwenye ugomvi naye. Sabrina hakuwa msichana masikini, kama alivyokuwa Razak, hata naye alitoka katika familia ya kitajiri.
Katika maisha yake, hakujua shida ilifananaje, alipata alichokitaka, alikwenda alipopataka, alizunguka katika nchi nyingi za Kiarabu kwa sababu baba yake alikuwa mfanyabishara mkubwa wa mafuta aliyejiwekea heshima kubwa Afrika Mashariki.
“Sabrina, tutagombana mpaka lini, kwa nini mapenzi hayana furaha kabisa, kila siku, ugomvi, ugomvi, ugomvi, ugomvi mpaka lini Sabrina?” aliuliza Razak huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Mpaka kiama...”
“Unasemaje?”
“Kwani umesikiaje?”
“Hebu niambie ukweli! Kwa nini mambo yanakuwa hivi? Una mtu mwingine?” aliuliza Razak.
“Unataka kujua ili iweje?”
“Nijue tu, nahisi hakuna uhusiano ulio kama hivi halafu nyuma ya pazia kukawa kusafi, kuna kitu. Hebu niambie, kuna nini mpenzi?” aliuliza Razak.
“Wewe Razak, mbona unapenda kunisumbua? Kila siku mapenzi, mapenzi tu, mapenzi, wengine yanatuchoshaaaa...” alisema Sabrina.
“Kweli unaniambia hivyo?”
“Ndiyo!”
Hayo yalikuwa mazungumzo yaliyokuwa yakijirudia kichwani mwake wakati huo alipokuwa ndani ya gari. Kichwa chake kilichanganyikiwa mno, hakuamini kama yeye ndiye aliyekuwa akipitia katika uhusiano huo uliojaa misukosuko ya kila aina.
Kila siku alimuomba Mungu, mambo yabadilike, awe na furaha kama siku za kwanza alipokutana na Sabrina lakini kitu cha ajabu, kila siku alijiona kuishi katika tanuru la moto, maumivu kila siku.
Moyo wake uliumia na kuumia, alikosa kimbilio, alipowaambia wazazi wake, kitu kimoja tu ndicho walichomwambia kwamba ilikuwa ni lazima amuoe Sabrina kwani wao na wazazi wake walikuwa kwenye uhusiano mzuri.
“Hivi wanajua ninayoyapitia?” alijiuliza.
“Au wanahisi ninaogelea kwenye dimbwi la mahaba?” alijiuliza Razak lakini akakosa jibu.
Dakika ziliendelea kwenda mbele, alichoka lakini hakutaka kurudi kule alipotoka. Magari binafsi machache yalikuwa yamepaki kwenye foleni yakisubiria muda ufike, geti lifunguliwe na safari ya kuvuka kivuko kuanza.
Hapo alikuwa safarini kuelekea Kigamboni ili kuonana na rafiki yake, Jafari Saydou kwa lengo la kuzungumza naye kuhusu msichana Sabrina.
Jafari alikuwa rafiki yake wa kipindi kirefu, mwanaume huyo alikuwa akisoma chuo kimoja na Sabrina. Akili ya ya Razak ilimwambia kwamba ilikuwa ni lazima kuna kitu kilichokuwa kikiendelea nyuma ya pazia juu ya msichana wake huko chuoni.
Usiku huo japokuwa ulikuwa umekwenda sana lakini alitaka kuonana na rafiki yake huyo, alitaka kuzungumza naye ili amwambia ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea chuoni.
Alimtafuta sana kwenye simu, hakumpata, alimtumia meseji, zilikwenda lakini hazikufika, alichoka, alikuwa na haraka ya kutaka kujua na ndiyo maana aliamua kufunga safari na kumfuata hukohuko Kigamboni.
“Puu...Puu...Puu...” alishtuka kutoka kwenye lindi la mawazo baada ya kusikia kioo cha gari lake kikigongwa na mtu aliyekuwa nje, akakishusha.
“Kuna nini?”
“Chokoraa wameng’oa taa za nyuma ya gari lako,” alisema jamaa huyo maneno yaliyomfanya Razak kushtuka, akafungua mlango na kutoka ndani ya gari, akaelekea nyuma, kweli taa mbili za gharama zilikuwa zimeng’olewa, hasira zikampanda, akarudi ndani ya gari na kuchukua bastola yake.
“Wamekimbilia wapi?” aliuliza huku akionekana kuwa na hasira.
“Wameshuka chini karibu na bahari, kule kwenye mawemawe...” alijibu jamaa huyo.
Razak hakutaka kusubiri, alionekana kama mbogo aliyejeruhiwa hivyo kuanza kuteremka kule baharini kulipokuwa na mawe mengi. Alikimbia kwa kasi kubwa, bunduki ilikuwa mkononi mwake na alikuwa tayari kwa kila kitu, hata kuua, siku hiyo alikuwa radhi.
Mbele yake, kwa mbali kabisa aliweza kuwaona watu wawili wakikimbia, walikuwa watoto wa kiume, akaongeza kasi kwa kujua kwamba hao ndiyo walikuwa wezi walioiba taa za gari lake.
Mawe yalikuwa mengi, giza lilikuwa totoro lakini hakujikwaa, alikuwa imara na aliweza kukimbia kwa kasi kana kwamba alikuwa akikimbia sehemu iliyokuwa na mchanga.
Alipofika mbele kabisa, cha kushangaza, aliangalia huku na kule, hakuona mtu, yaani watoto wale waliokuwa wakikimbia, walimpotea, na mbele yake palikuwa peupe.
“Wapo wapi?” alijiuliza huku akiangalia huku na kule, wakati mwingine akahisi kama walitumbukia ndani ya bahari.
“Mna bahati mmekimbia, ningewaua paka nyie...” alisema Razak kwa sauti ya juu kana kwamba alikuwa akiongea na mtu aliyekuwa umbali wa hatua mia moja toka pale alipokuwa.
“Wakina nani?” ilisikika sauti ya msichana mmoja, ikamfanya Razak kuogopa, akageuka kule sauti ilipotoka, akanyoosha bunduki kuelekea kule.
“Unataka kuniua?” ilisikika sauti hiyo ikiuliza.
“Wewe ni nani?” aliuliza Razak huku kwa mbali akitetemeka.....
ITAENDELEA......
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni
Chapisha Maoni