BEYOND LOVE ( ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA 8
SIMULIZI: BEYOND LOVE ( ZAIDI YA MAPENZI)
SEHEMU YA 8
ndani ya gari kwenda hospitali ya Ocean Road, Tom akiwa ameacha maagizo kwa wauguzi kwamba ikitokea Mariam akaonekana na kuulizia basi aelekezwe mahali walikokuwa, wauguzi wakaahidi kumsaidia kufanya hivyo. Safari ya hospitali ya Ocean Road ikaanza, siku zote Tom alipita nje ya hospitali hiyo akielekea feri lakini hakuwahi kuwaza kwamba siku moja angeingia humo akiuguliwa na baba yake, hakuamini kama Saratani ingeweza kuingia ndani ya familia yake, aliuona ugonjwa wa watu wengine.
Matibabu yalianza siku hiyo hiyo kwa njia ya vidonge, mionzi na dawa za sindano ambazo badala ya kuonekana kumsaidia mzee Chacha zilimdhoofisha zaidi, afya yake ikaharibika kabisa na kupoteza uzito mwingi ndani ya muda mfupi! Nywele zote zikanyonyoka kichwani sababu ya ukali wa dawa alizokuwa akipewa.
Kila mara Tom alipomwangalia baba yake alishindwa kuvumilia na kutoka nje ambako alibubujikwa na machozi akitamani angalau Mariam angeonekana na kumpa maneno ya faraja lakini haikuwa hivyo, hatimaye wiki mbili zikakatika hali ya mzee Chacha ikizidi kuwa mbaya, madaktari wakashauri mgonjwa arudishwe nyumbani hasa baada ya kugundua alikuwa ni mtu wa Tarime na mke wake hakuwa tayari azikwe jijini Dar es Salaam kama kingetokea kifo jambo ambalo kila mtu alikuwa akilitarajia.
“Sawa tu daktari nimekubali, tatizo letu kubwa ni nauli, hatuna fedha kabisa!”
“Mimi na wafanyakazi wenzangu tutawachangia fedha kidogo lakini pia ninyi mnaweza mkajitahidi kutafuta kwa ndugu jamaa na marafiki!”
“Tutajitahidi!”
Alichokifanya mama yake Tom ni kuuza vyombo vyote vya ndani, akaenda Pepsi kazini kwa mume wake na kuomba msaada, Mkurugenzi wa kiwanda hicho akampa shilingi laki moja na nusu na kuja nazo hadi hospitali ya Ocean Road ambako wafanyakazi walimkabidhi shilingi laki moja, jumla akawa na shilingi laki sita pamoja na zilizopatikana kwa kuuza vyombo, mipango ya safari ikaanza kuandaliwa.
Siku mbili tu baadaye bila Tom kuonana na Mariam, moyo wake ukiwa umejaa hasira, walipanda daraja la tatu la treni kuelekea Mwanza ambako wangeunganisha kwa basi hadi Tarime, kwa jinsi hali ya mzee Chacha ilivyokuwa mbaya ilibidi abiria wote waliokuwa naye kwenye kiti, wanyanyuke kumpisha alale, hakuna aliyekuwa na uhakika angefika mzee huyo angefika Mwanza siku tatu baadaye akipumua.
Ulikuwa ni mlio mkubwa mno kwa mtu yeyote aliyekuwa jirani na eneo hilo kutosikia, watu wengi waliokuwa jirani walianza kukimbia kwenda mahali magari yalipogongana, baadhi wakiwa na nia ya kuokoa lakini wengine wakifikiria kuiba mali yoyote ambayo wangeikuta. Magari yaliyokuwa yakipita kwenye Barabara ya Nyerere kwenda au kutoka Uwanja wa Ndege yalishindwa kuendelea na safari sababu barabara ilikuwa imezibwa na magari mawili yaliyogongana uso kwa uso katikati ya barabara, hii iliwafanya abiria wote waliokuwa kwenye magari washuke kwenda kutoa msaada.
Kwenye daladala kulikuwa na abiria wengi walioumia, dereva wake akiwa amelaza kichwa kwenye usukani, damu zikimtoka puani na mdomoni, tayari alishakufa! Taratibu wakamwondoa na kumlaza chini. Sababu tairi za mbele za daladala zilikuwa zimesimama juu ya gari dogo lililogongwa, ilibidi watu wajitolee kulisukuma kurudi nyuma ili kutoa nafasi ya kuangalia kama kulikuwa na watu wengine ndani ya gari dogo. Hayo yalifanyika wakati abiria waliojeruhiwa wakipakiwa ndani ya magari mengine tayari kwa kupelekwa hospitali ikiwa ni pamoja na dereva wa daladala aliyekufa.
“Mungu wangu kuna mtoto mdogo, tena kwenye usukani, sijui ndiye aliyekuwa akiendesha? Mbona mdogo sana?” Mtu mmoja aliuliza baada ya daladala kuondolewa juu ya gari dogo.
“Ni mdogo mno huyu, hawezi kuwa dereva kama ni hivyo basi itakuwa aliiba gari, hawa watoto wa matajiri ndio wanasababisha sana ajali barabarani, si ajabu alikuwa ametoka zake disko akiwa amelewa!” Mwingine aliitikia.
Mariam alikuwa amelala ndani ya gari lililogongwa, akiwa kimya kabisa huku damu nyingi zikimtoka hasa kwenye paji la uso palipoonekana kuvimba, damu nyingine ilikuwa ikimtoka puani na masikioni. Kwa jinsi alivyokuwa amebanwa ilikuwa kazi ngumu kidogo kumtoa, hata hivyo baada ya muda si mrefu walifanikiwa na kumlaza chini kisha kuanza kumgusa kifuani kuona kama alikuwa na uzima.
“Anahema!” Aliongea mwanaume aliyekuwa akimgusa kifuani.
“Basi hajafa, tumkimbizeni hospitali!”
“Ni jambo jema, mleteni huku kwenye gari yangu nimpeleke mara moja Muhimbili!” Mwananchi mmoja alijitolea, Mariam akabebwa juu juu na kwenda kupakiwa kwenye gari dogo aina ya Mark II, safari kwenda hospitali ikaanza ambako walikuta pia majeruhi wengine wamekwishawasili.
Mapokezi hawakuona sababu ya kuuliza maswali mengi kwa jinsi hali ya mgonjwa ilivyokuwa mbaya, haraka akakimbizwa mpaka kwenye chumba cha daktari ambaye baada ya kumwona aliamuru akimbizwe haraka sana Chumba cha Upasuaji, kisha yeye kuwasiliana na madaktari wengine ambao walikutana kwenye chumba hicho na Mariam kuwekewa Mashine ya Hewa ya Oksijeni kisha kupandishwa kitandani ambako kazi ya kwanza iliyofanyika ni kuziba mishipa yote iliyokuwa ikivuja damu kuzuia upotevu mkubwa.
“Haraka sana mfanyieni CT-Scan!” Dk. Majaliwa, Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Uti wa Mgongo, alisema.
“Sawa daktari, acha tuwapigie simu hawa watu waje kuifanya kazi hiyo mara moja!”
“Fanyeni hivyo haraka kwani kwa dalili ninazoziona nahisi kuna tatizo kwenye ubongo wake!”
“Sawa daktari!”
Dakika ishirini baadaye Bingwa wa Kipimo cha CT-Scan alifika kwenye Chumba cha Upasuaji cha Hospitali ya Muhimbili na vifaa vyake na kumfunga Mariam kichwani, kisha yeye na madaktari wote wakaanza kuangalia, haikuhitaji muda mrefu sana kugundua kilichokuwa kikiendelea chini ya fuvu la Mariam; damu nyingi ilikuwa imevuja chini ya fuvu, kichwa chacke kilijipiga kwenye chuma sehemu ya paji la uso na ubongo kuumia kwa ndani.
“She has a subdural haemorrhrage!” (Anavuja damu chini ya fuvu!) Dk. Majaliwa aliongea baada ya kuitazama picha kwenye kompyuta.
“So?” (Kwahiyo?)
“She needs an urgent operation!” (Anahitaji upasuaji wa haraka)
“Are we ready?” (Tuko tayari?)
“Yes!” (Ndiyo)
“Can the people from laboratory do urgent blood grouping and cross matching check? As well as HB level?” (Watu wa maabara wanaweza kupima kundi lake la damu na anaweza kuongezewa na kundi gani? Pia kiasi cha damu alichobakiza?) Dk. Majaliwa alisema na wote wakakubaliana, watu wa maabara wakaitwa haraka na kuifanya kazi hiyo.
Hapakuwa na mtu wa kujiuliza mtu waliyekuwa wakimshughulikia aliitwa nani, mtoto wa nani na alitokea wapi. Kwao alikuwa ni mgonjwa na kazi yao kubwa ilikuwa ni kuokoa maisha yake, hilo ndilo madaktari walilotaka kulifanya. Damu ilipopatikana, vipimo vya moyo wake vikawa viko sawa, Mariam aliingizwa kwenye
ITAENDELEA.......
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni
Chapisha Maoni