MISS TANZANIA SEHEMU YA 23



MISS TANZANIA

SEHEMU YA 23

MTUNZI: PATRICK.CK

ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
.Mambo mengi yatajitokeza lakini nitakabiliana nayo” akasema Happy kwa kujiamini
“Nitakutana na Mike baadae na nitaitumia nafasi hiyo kumweleza ukweli na nina imani atanielewa na kuniacha huru ili niweze kuwa na mtu ninayempenda kuliko wote katika maisha yangu” Happy akasema na Margreth akamtazama dada yake kwa huruma.

ENDELEA……………..

Saa sita za mchana gari ndogo nyeupe yenye namna za ubalozi wa Marekani ilisimama mbele ya nyumba ya akina Happy na kijana mmoja mtanashati aliyevalia suti nzuri nyeusi iliyomkaa vyema akashuka.Alikuwa ni kijana mwenye sura nzuri sana na ambaye ni wazi alikuwa akiwasisimua mabinti kila apitapo.Huyu alikuwa ni Mike mchumba wa Happy.kwa uzuri aliokuwa nao happy alistahili kuwa na kijana kama huyu
Margreth ambaye alikuwa amekaa sebuleni akatoka kwa kasi na kwenda kumpokea shemeji yake na kumkaribisha ndani.Mike akasalimiana na familia yote kisha akaletewa kinywaji na kuanza kunywa taratibu wakati akimsubiri Happy aliyekuwa chumbani kwake akijipamba.
“ Mike amekuja yuko sebuleni anakusubiri” Margreth akamwambia Happy baada ya kumfuata chumbani kwake.
Baada ya kupokea taarifa ile toka kwa Margreth Happy akakaa kitandani na kupumua kwa nguvu.Akauweka mkono wake mahala unapokaa moyo .Alipatwa na mawazo mengi ya ghafla.
“happy kulikoni? Margreth akamuuliza dada yake baada ya kuona namna alivyonyong’onyea ghafla
“Maggy nahisi miguu mizito sana kwenda kuonana na Mike.nashindwa nitaanzaje kumweleza kuhusiana na suala la kuachana.Nina wasi wasi mkubwa”
Margreth akamtazama dada yake na kusema
“happy huna sababu ya kuogopa.Hii ni kwa ajili ya furaha ya maisha yako.Kama kweli una nia ya dhati ya kuachana na Mike ili uwe na Patrick usisite kufanya hivyo.Huu ndio wakati wako.Umeipata nafasi naomba uitumie.Usisubri nafasi nyingine ijitokeze.Mueleze Mike ukweli na nina imani ni mtu mwelewa sana na atakuelewa vizuri.Najua ugumu uliopo katika kufanya hivyo hasa kwa mtu ambaye tayari mmeshakuwa wapenzi kwa muda wa miaka mingi na tayari mmeshaingia katika uchumba lakini kama ulivyosema kwamba chaguo lako ni Patrick basi huna budi kuachana na Mike.kwa maana hiyo basi vuta pumzi ndefu inuka hapo kitandani nenda kaonane na Mike,mtoke kwa chakula cha mchana na uitumie nafasi hiyo kumueleza Mike ukweli kuhusiana na msimamo wako huo.Kama kutakuwa na tatizo lolote lile nipigie simu nitakufuata haraka sana.”
Maneno yale ay Margreth yanamfanya Happy atabasamu na kisha akamkumbatia mdogo wake.
“nashukuru sana Maggy kwa kunipa moyo.Ninakwenda kuonana na Mike.” Akasema Happy huku akiichukua pochi yake nogo na kujiangalia kwa mara ya mwisho katika kioo.Akaufungua mlango wa chumba chake akatoka na kuelekea sebuleni.Mara tu alipotokeza sebuleni Mike alishindwa kuvumilia na kwa kasi akainuka na kumkumbatia Happy kwa nguvu.
“Ouh malaika wangu. Nafurahi nimekuona tena.Ningeingiwa na uchizi kama siku aya leo ingekwisha bila kuitia machoni sura yako nzuri” akasema Mike huku akimshika mkono Happy na kumketisha sofani
“habari yako Mike.habari za Marekani? Hajambo Michelle? Happy akauliza
“habari za Marekani ni nzuri.Michelle ni mzima ila mimi ndiye nilikuwa mgonjwa.Nilikuwa nikiumwa ugonjwa wa kutoiona sura yako lakini kwa sasa nimepona baada ya kukutia machoni.” Akasema Mike na wote mle sebuleni wakacheka.Mama yake Happy akainuka na kuondoka kuelekea chumbani kwake na kuwaacha vijana wake pale sebuleni.
“Happy mpenzi wangu vipi maendeleo yako? Mike akauliza huku ameushikilia mkono wa happy
“namshukuru Mungu ninaendelea vizuri sana” Hapy akajibu
“Nashukuru kama unaendelea vizuri.Nilipata taarifa kwamba ulipatwa na maradhi ya ghafla baada ya kulitwaa taji la Miss Tanzania.Niliogopa sana ikanilazimu kuchukua likizo ya ghafla na kuja hapa kuungana nawe katika kipindi hiki ambacho nina imani ulihitaji sana uwepo wangu.Hongera sana kwa kufanikiwa kulitwaa taji hili kubwa la urembo.Nina zawadi nzuri sana kwa ajili ya ushindi wako huo” akasema Mike na kumfanya Happy atabasamu
“ahsante sana Mike kwa kuja kunifariji.Ni kweli nilipata kitu kama mstuko Fulani baada ya kutangazwa mshindi wa taji lile la Miss Tanzania.Sikuwa nimetegemea kama ningeweza kulitwaa taji lile kutokana na ushindani mkubwa uliokuwepo baina ya washiriki.Baada ya hali ile kunitokea ilinilazimu kuchukua siku kadhaa za mapumziko na kuwa mwenyewe kwa ajili ya kuweza kutafakari na kujipanga namna nitakavyoweza kuishi maisha mapya na namna nitakavyoweza kulibeba jukumu hili kubwa nikiwa kama mrembo wa Tanzania.Nashukuru kwamba ninaendelea vizuri kwa sasa .ahsante kwa zawadi yako” Happy akasema na kisha kikapita kimya kifupi
“vipi uko tayari kwa kutoka? Tulikubaliana kwamba leo tutatoka kwa ajili ya chakula cha mchana .” Mike aksema
“Niko tayari Mike tunaweza kutoka” Happy akajibu na kisha Mike akamshika mkono Hapyy wakatoka wakaingia garini na kuelekea mahala ambako Mike alitaka waende wakapate chakula
“Happy nimefurahi sana kwa kukuona tena.Huwezi kujua ni furaha ya namna gani ambayo ninayo kwa kuwa nawe tena .Kwa mahala nilipofika sasa sintaweza kuishi bila kuwa nawe.Niko tayari kufanya kila kitu ili mradi niwe nawe.Niko tayari kuacha hata kazi ninayoifanya kule Marekani kwa ajili ya kuwa nawe .Ninakupenda sana Happy “ Mike akasema wakiwa garini kuelekea hotelini.Happy akatoa kitambaa katika mkoba wake akafuta jasho lililokuwa likimtoka.Alikuwa akitokwa jasho kutokana na mtihani mgumu aliokuwa nao juu ya kuusitisha uhusiano kati yake na Mike.
“Mungu nisaidie.Niko katika mtihani mgumu sana wa kumueleza Mike ukweli kwamba nimekutana na Patrick na nimeamua kurudiana naye.Mike ananipenda sana na sijui nitaanzaje kumueleza ukweli kwamba hatutaweza kuendelea tena na uhusiano wetu.” Happy alizama katika mawazo na ghafla akastuliwa na sauti ya Mike
“Unawaza nini mpenzi wangu? Halafu mbona jasho linakutoka sana? 
“ Ni hili joto la Dar “ happy akasema
“Ni kweli hata mimi ninalisikia joto kali sana.Ningejua ningechukua gari la wazi “ akasema Mike Happy hakujibu kitu akatabasamu.
Walifika hotelini ambako tayari Mike alikwisha weka oda ya meza moja maalum kwa ajili yake na Happy.Wakaonyeshwa meza yao na kwenda kukaa na kisha wakaagiza chakula .Wakati wakisubiri chakula kiwe tayari,walikuwa wakiendela kuburudika kwa vinywaji
“Happy bado naendela kukupa hongera zangu kwa kushinda taji la mrembo wa Tanzania.Siku zote nilikuwa nikiamini kwamba una vigezo vyote ya kuwa mrembo mwenye jina kubwa lakini niliogopa kukwambia kuhusiana na masuala ya urembo kwa sababu toka nimekufahamu sijawahi kusikia hata mara moja ukigusia kwamba unapenda mambo ya urembo.” Akasema Mike
“Mike ni kweli sijawahi kukutamkia kwamba ninapenda urembo lakini toka siku nyingi nilikuwa nipenda sana mambo haya ya urembo japokuwa nilikuwa bado sijaamua kujiingiza rasmi katika fani hii.Kuna mtu aliniona akanishauri nijaribu kushiriki mashindano ya miss Tanzania na kweli nikajaribu na nikashinda.” Happy akasema huku akitabasamu.
Chakula kikaletwa wakala na baada ya kula wakaendelea na maongezi mengine.kadiri muda ulivyokuwa ukisonga na ndivyo Happy alivyozidi kuwa na wasi wasi mwingi hali iliyomfanya Mike kugundua kwamba kuna jambo ambalo haliko sawa.Akamuuliza kama kuna jambo linamsumbua.
“hapana Mike hakuna jambo linalonisumbua.Unajua kwa sasa kila nionekanapo ninakuwa nikipigwa picha na waandishi wa habari.Ndiyo maana ninakuwa sina imani kila mahala ninapokuwa” Happy akajibu
“Suala hilo lisikuumize kichwa mpenzi wangu.Kwa sasa wewe ni mrembo wa taifa na ni kioo cha jamii.Hutakiwi kujificha.Unatakiwa kutoka na kuchangamana na jamii inayokuzunguka.usiwe na wasi wasi kuhusu jambo la kupigwa picha ni suala la kawaida” Mike akasema na kisha wakaendelea na maongezi mengine.

*****************************

Saa tisa za alasiri tayari viti vyote vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya wale wote waliokuwa wamealikwa kuhudhuria kikao hiki cha mwisho cha maandalizi ya harusi.ya Patick na Vero vilikuwa vimejaa.Kikao hiki kilichojumuisha kamati nzima ya maandalizi ya harusi hii pamoja na ndugu wengine muhimu ambao Patrick alikuwa amependekeza wawepo katika hiki kikao ambacho yeye alikiita ni muhimu sana .
Saa tisa na dakika ishirini gari la Patrick likawasili katika nyumba ya wazazi wake ambako ndiko kikao hiki cha leo kilikuwa kikifanyikia.Toka ndani ya ile gari wakashuka Patrick na Veronika na kuanza kupiga hatua kuelekea ndani.Ni wao pekee waliokuwa wakisubiriwa.katika kikao kile.
Mara tu walipoingia bustanini ambako ndiko kikao kilikuwa kifanyikia vikasikika vigere gere vingi na watu wakaanza kushangilia.Wote waliamini kwamba muda si mrefu tayari familia hizi mbili zingeungana na kuwa kitu kimoja.Akina mama walipiga vigere gere na kushangilia kwa nguvu baada ya kuwaona Patrick na Vero pamoja.
Moja kwa moja Patrick akaanza kwanza kusalimiana na baba yake ambaye hakuwa ameonana naye kwa muda mrefu kidogo na kisha akamsalimu mama yake Vero na ndugu wengine na baada ya zoezi hilo wakachukua nafasi zao.
Mwenyekiti wa kikao kile ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya maandalizi akafungua kikao kwa sala fupi na kisha akawakaribisha wote katika kikao kile.Baada ya kufungua kikao kile akatoa taarifa ya kamati kuhusiana na maaandalizi yote ya harusi ile kwa ujumla.Baada ya kuisoma taarifa ile ya jumla ,mwenyekiti akawakaribisha wenyekiti wa kamati ndogo ndogo ili nao waweze kutoa ripoti zao na kisha wote kwa pamoja waweze kuangalia kama kuna sehemu yoyote yenye mapungufu ili waweze kuyafanyia kazi.Kabla hajasimama mtu yeyote kuongea Patrick akasimama na kuomba kuongea machache.
“ Wapendwa sana wazazi wetu,ndugu wote mliohudhuria kikao hiki,ndugu wanakamati wote mabibi na mabwana nilikuwa nimeomba nafasi ya kusema machache katika kikao hiki hivyo kabla mambo mengine hayajaendelea naomba niitumie nafasi hii niseme mambo machache sana kwenu nyie ndugu zangu.Kwanza nawashukuru sana kwa namna mlivyojitolea kwa kila hali kuhakikisha kwamba maandalizi ya harusi yangu yanakamilika.Nawashukuru sana kwa jitihada zenu na ushirikiano wa kila mmoja wenu.Sina kitu chochote cha kuwalipa ni mwenyezi Mungu pekee atakayewalipa.Jambo la pili ninalotaka kulisema hapa ni jambo ambalo linahusu historia yangu kwa ujumla.Ni jambo linalonihusu mimi na maisha yangu.Wengi bado hamjafahamu historiia yangu ,wapi nimetoka hadi leo hii tuko hapa pamoja mkinisaidia kuandaa harusi yangu.Sitaki kuchukua muda mrefu sana ila naomba nitumie dakika chache kuwakumbusha japo kwa muhtasari nimetoka wapi hadi nilipo hivi sasa.” Patrick akasema na kuwafanya watu wote wajiulize nini anataka kuwaambia.
“Historia ambayo katu haitaweza kufutika maishani na itaendelea kuwapo kichwani mwangu daima ni siku ile ambayo nilihamia katika shule ya sekondari Malangali Iringa nikitokea shule ya Mazwi sekondari Sumbawanga ambako wazazi wangu walikuwa wakiishi na kufanyakazi kule kama watumishi wa umma.Nakumbuka nikiwa katika kituo cha magari yaendeayo katika kijiji cha malangali nilikutana na msichana mmoja ambaye naye alikuwa akielekea huko.Msichana huyu ambaye kwa jina aliitwa Happy baadae alikuwa rafiki yangu mkubwa sana.”
Wazazi wa Patrick wakatazamana.Kila mmoja alikumbuka mbali sana .Vero alionyesha mstuko wa dhahiri.Patrick akaendelea
“ msichana huyu alitokea kuwa rafiki yangu mkubwa kwa sababu ni mimi pekee ambaye nilimuelewa na kumuamini.Happy alikuwa akisemekana kwamba ni muathirika wa virusi vya ukimwi na hivyo wanafunzi wote wakamtenga.Kati ya wanafuni wote ni mimi pekee ambaye nilimuamini aliyonieleza kwamba hakuwa muathirika kama alivyokuwa amezushiwa bali alikuwa na matatizo ya kiafya.Nilifanya kila nilivyoweza na nikafanikiwa kumfanya Happy asikate tamaa na hivyo akaanza kusoma tena kwa bidii na kuanza kushika nafasi za juu kimasomo.Kitendo hiki hakikuwafurahisha wanafuni wengi na hivyo kuzidisha chuki na uhasama.Sitaki kueleza kila jambo kwa sababu ni mambo mengi yalitokea lakini katika kila jambo nilisimama imara kumtetea na sikuwa tayari kuona Happy akinyanyaswa.” Patrick akanyamaza akameza mate .Kila mtu alikuwa akaishangaa ni kitu gani alichokuwa akikiongea Patrick.
“ Ilitokea siku moja kulikuwa na muziki wa disko pale shuleni.Nikiwa sina hili wala lile kumbe kuna baadhi ya wanafunzi watukutu walikuwa wameunda mpango wa kutaka kumdhalilisha Happy.Tukiwa tumekaa peke yetu tulivamiwa ,nikapigwa na kitu kizito kichwani nikapoteza fahamu baada ya hapo Happy akapelekwa katika kichaka na wahuni wale wakaanza kujiandaa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji.kwa bahati nzuri nilipata fahamu haraka na kuwafuata wale jamaa kule kichakani nikampiga kiongozi wao na chuma kichwani akaanguka na kufariki dunia.Baada ya hapo nilikamatwa na kufungwa gerezani “ Patrick akanyamaza tena na mara watu wakaanza kusemezana wao kwa wao.Wengi hawakuwa wakifahamu historia ya Patrick.Vero alikuwa amejikunyata akiwa na mawazo mengi sana.
“Nikiwa gerezani bado Happy ambaye kwa kipindi hicho tayari nilikuwa na mahusiano naye ya kimapenzi aliendelea kuwa nami hadi pale wazazi wake walipomtaka akaendelee na masomo yake nchini marekani.Alikataa kwenda huko na kuniacha peke yangu lakini ni mimi ndiye niliye msisitiza kwamba akubali kwenda huko .Hata baada ya kwenda huko bado tuliendelea kuwasiliana kila mara .Matatizo yalianza baada ya mimi kuhamishwa gereza.Nilihamishiwa katika gereza jipya huko Songea na baada ya hapo mawasilano kati yangu na Happy yakawa magumu sana.Siku moja nilikutana na mtu ambaye baadae nilimtambua kwamba ni Veronika ambaye yeye pamoja na mimi tumewakutanisha nyote hapa leo .Nilimweleza historia yangu na nikamuomba Veronika ili aweze kunisaidia katika kufanya mawasiliano kati yangu na Happy.” Patrick akanyamaza tena.Vero alikuwa akimuangalia kwa macho makali .Watu woe walikuwa kimya wakisikiliza
“Siku moja Vero alikuja na taarifa ambayo ilinitesa kwa miaka mingi.Alinieleza kwamba mpenzi wangu Happy ameamua kuolewa huko Marekani na tayari ni mjamzito.Sitaki kukumbuka mateso na maumivu nililyoyapata siku ile.Niliumia mno .Baada ya miaka mingi kupita niliamini kwamba nikweli Happy aliamua kunisaliti.Niliamua kuendelea na maisha yangu na hivyo mimi na Vero tukawa wapenzi.Siku moja tukiwa nyumbani nilitazama katika luninga na mara nikamuona Happy nikapatwa na mstuko na kuzimia.Sikumueleza mtu yeyote yule sababu ya kuzimia kwangu.Siku ya kinyang’anyiro chakumtafuta mrembo wa Tanzania Happy akafanikiwa kunyakua taji la Miss Tanzania na nilipomkaribia alinitambua na yeye akapoteza fahamu.Baada ya hapo nilifanya juhudi mpaka nikafanikiwa kuonana naye.Nilishangaa sana aliponiuliza ni kwa nini niliamua kudanganya kwamba nimekufa hali niko mzima.Nilishangaa sana na sikuamini hadi aliponikabidhi barua aliyoandikiwa na mtu ambaye alimtaarifu kwamba nimefariki nikiwa gerezani.Niliisoma barua ile nikatoa machozi baada ya kugundua kwamba ilikuwa imeandikwa na Vero.Baua yenyewe hii hapa” Patrick akasema huku akimkabidhi baba yake ile barua ili aisome. Watu wote walibaki vinywa wazi.Vero alikuwa ameinama akilia kwa kwikwi.
“ Ndugu zangu nimewaeleza haya yote ili mtambue ni kwa jinsi gani Vero alivyonifanyia ukatili mkubwa.Ni wazazi wangu pekee ambao wanafahamu ni mateso gani niliyoyapata wakati ule.Nimeumia sana baada ya kuufahamu uongo huu mkubwa alioutunga Vero na kusababisha mimi na Happy tukasambaratika.Mbele yenu wazazi na ndugu wengine wote naomba mnisamehe sana kwa haya nitakayoyasema lakini huu ni uamuzi wangu kutoka moyoni….” Patick akanyamaza kidogo na kisha akasema
“Nimeamua kuachana na Vero na kusitisha kila kitu kuhusiana na ndoa yetu. kuan…………….” Patrick hakumaliza kauli yake mara akina mama watatu akiwemo mama yake na mama yake Vero wakaanguka na kuzirai.Kizaa zaa kikaibuka.Baba yake jasho lilianza kumtiririka ,shinikizo la damu lilimuanza.Kila mtu alihisi kuishiwa nguvu.
Eneo ambalo saa chache zilizopita watu walikuwa wakifurahi na kupongezana , akina mama wakipiga vigere gere kwa furaha kubwa waliyokuwa nayo wakiamini kwamba hakuna kipingamizi chochote cha kuwazuia kuziunganisha familia zao kupitia kwa watoto wao wawili Patrick na Veronika , kwa sasa liligeuka sehemu yenye vilio na mstuko mkubwa sana.Kila mtu aliyekuwepo eneo lile alikuwa amestushwa mno na kilichotokea.Hakuna aliyekuwa ametegemea kama Patrick angeweza kuongea kitu kama kile alichokiongea.Hakuna aliyeota kama ingetokea siku Patrick angeweza kusitisha mipango yua ndoa yake na mchumba wake Veronika.Kila mtu aliona hii ni kama ndoto na si kitu cha kweli..
Haraka haraka wale wote waliozirai kutokana na mstuko walioupata wakaanza kusaidiwa kwa kupatiwa huduma ya kwanza ii waweze kurejewa na fahamu zao .Mahala hapa palionekana kama vile kumetokea msiba.Watu waliokuwa wakiishi jirani na eneo lile wakaanza kujaa katika nyumba hii wakiamnini kuna tatizo limetokea baada ya kusikia vilio vya akina mama.Baba yake Patrick alikuwa katika hali mbaya kutokana na shinikizo la damu .Hali ilikuwa ya kuogopesha sana na kwa haraka Patrick akalisogeza gari na kisha baba yake akapakiwa na kukimbizwa hositali.Patrick jasho lilikuwa likimtoka.Alionekana kama ni mtu aliyechanganyikiwa kutokana na alichokishuhudia kikitokea.
“Ee Mungu naomba unisaidie katika suala hili ambalo limeanza kuwa gumu sana” akawaza Patrick wakati wakiwa garini wakimkimbiza baba yake hospitali.Patrick hakuwa akiongea kitu alikuwa ameinamisha kichwa chini akitafakari.
“Sikutegemea kama mambo yangeweza kufika hapa yalipofika .Nilitegemea kungekuwa na ugumu na upinzani mkubwa katika jambo hili lakini sikuwa nimetegemea kama jambo la namna hii lingetokea.Imekuwa ni zaidi ya msiba.Hakuna aliyekuwa ametegemea kama ningeweza kuachana na Vero na hasa katika kipindi hiki cha mwisho cha maandalizi ya harusi yetu.Nimewaumiza watu wengi sana .Kila mtu atakayesikia kuhusu suala hili atanilaani na kuniona mkatili mkubwa.Lakini ni kwa nini basi hakuna hata mtu mmoja ambaye yuko tayari kunisikiliza na kunielewa? Kwa nini hawataki kuupa uzito upande wangu pia? Nimejaribu kuwaelezea kwa ufasaha mkubwa sana ili wanielewe lakini hakuna hata mmoja anayeonekana kunielewa.Hakuna hata mmoja ambaye ameguswa na machungu niliyoyapata kwa uongo huu mkubwa wa Vero“ akawaza Patrick halafu akatoa kitambaa na kujifuta jasho lililokuwa likimtiririka kama maji..
“Litakalo tokea na litokee .Sintaweza kurudi nyuma kamwe.Nilimuahidi Happy kufanya kila niwezalo kwa ajili ya kuwa naye tena.Siwezi kubadili maamuzi yangu.Hata kama nitakabiliana na magumu ya kiasi gani lakini sintarudi nyuma katika azma yangu ya kutaka kuachana na Vero.Kwa sababu ya Happy nitafanya kila litakalowezekana hata kama nikilazimika kuutoa uhai wangu.” Patrick bado alizidi kusongwa na mawazo mengi.

******************************

“Kitu gani cha kwanza umepanga kukifanya ukiwa kama mrembo wa Tanzania? Mike akamuuliza Happy wakiwa wanaendelea na kupata vinywaji.Happy akamtazama Mike kisha akatabasamu na kusema
“Kama mrembo wa Tanzania nitakuwa nikipangiwa majukumu ya kufanya na ofisi maalum inayohusika na mambo yote ya Miss Tanzania.Lakini pamoja na kufanya kazi hizo nitakazokuwa nikipangiwa ambazo ni kazi za kujitolea katika jamii ninafikiria kuanzisha umoja au taasisi itakayowawezesha watu mbali mbali kuweza kujitolea katika jamii.” 
Mike akatabasamu na kuuliza
“Sijakuelewa vizuri mpenzi wangu kuhusiana na taasisi hiyo unayotaka kuianzisha”
Happy akatabasamu kama kawaida yake,tabasamu ambalo linamfanya Mike naye atabasamu.
“Umoja huu ninaotaka kuuanzisha lengo lake ni kujenga ule moyo wa kujitolea miongoni mwa wanajamii.Kila mtu ataruhusiwa kujiunga na umoja huu na kila mwisho wa wiki tutakuwa tukitembea katika sehemu mbali mbali kama vile mahospitali,magerezani ,mashuleni,katika vituo vya kulelelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu na hata kuwatembelea wale watu walioko majumbani wasiojiweza na kisha kila mtu akatoa msaada wake.Sitaki kujikita katika sehemu moja tu kama ilivyozoelekea katika jamii yetu kwamba kila mrembo wa Tanzania malengo na mtazamo wake ni kusaidia mayatima.Mtazamo wangu mimi utakuwa tofauti kidogo na wengine kwa sababu mimi ninataka kuisaidia jamii masikini na yenye uhitaji kwa ujumla wake bila kubagua.Katika suala hili sintahitaji mfadhili bali nitaitumia kofia ya Miss Tanzania kupita kila kona ya nchi hii kutoa elimu na kuwafundisha watu maana ya kujitolea .Kila mtu atakayeguswa atakuwa akijitolea kile kitu alichokuwa nacho kwa ajili ya watu wenye uhitaji.Kama atatokea mtu mwenye ufadhili nitashukuru na tutauelekeza ufadhili wake katika kada maalum yenye uhitaji mkubwa.” Happy kasema na kumtazama Mike ambaye alikuwa kimya kabisa akisikiliza.
Mike akatabasamu baada ya kuisikia mipango ile ya mchumba wake Happy.
“Happy siku zote ninamshukuru sana Mungu kwa kunipa mchumba mwenye akili nyingi na mwenye roho ya huruma sana.Nina kila sababu ya kujivuna kuwa nawe na siku zote za maisha yangu nitahakikisha kwamba unakuwa ni mwanamke mwenye furaha kubwa.Ninakuahidi msaada wangu mkubwa katika jambo hili unalolifikiria.Siku zote ntitakuwa nyuma yako ili kukupa ushirikiano wangu.Nikiwa Marekani nitakuwa nikifanya kazi ya kuwakusanya watu wenye asili ya afrika na kuwaomba tuuchangie mfuko huu kwa ajili ya maendeleo ya jamii zetu huku afrika.Natumai baada ya muda mfupi mfuko huu utakuwa mkubwa na kuwasaidia watu wengi sana.” Mike akasema na kumfanya Happy atabasamu halafu akainama chini.
“Kila nikimuangalia Mike nashindwa nitaanzaje kumueleza kwamba uhusiano wetu umefikia mwisho.Siwezi kuishi bila Patrick lakini kumweleza Mike ukweli ninashindwa.Nitafanya nini sasa? Happy akawaza.Mike akagundua kwamba mchumba wake Happy alikuwa katika mawazo mengi.
“Happy malaika wangu una matatizo gani? Naona kama bado hauko sawa sawa.Kuna jambo gani linalokusumbua akili yako? Ninakufahamu vizuri sana na ninafahamu kuna kitu kinakuuumiza kichwa chako.tafadhali naomba unieleze nini kinakusumbua akili yako.Niko hapa kwa ajili yako Happy” Mike akamweleza Happy
“Mike ni kweli nina tatizo kubwa na sijui hata nianzie wapi kukueleza” Happy akasema huku moyo wake ukimuenda mbio sana
Mike akalegeza tai yake na kumsogelea karibu zaidi Happy ili aweze kusikia ni tatizo gani hilo alilonalo Happy
“Happy niambie una tatizo gani? Mimi niko hapa kwa ajili yako.Nitakwenda hadi mwisho wa dunia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba unakuwa na uso wenye tabasamu daima.Niambie tafadhali una tatizo gani? Mike akasema huku akiupeleka mkono wake katika bega la Happy
Happy akakosa la kusema.Kila alipojitahidi kufumbua midomo yake iligoma kufunguka na kubaki ikicheza.Alikuwa akiogopa.Mara simu yake ikalia.Kwa haraka akafungua mkoba wake akaichukua na kuangalia mpigaji ambaye jina lake lilisomeka kama “My everything”.Hili ni jina alilotaka lisomeke katika namba ya Patrick.Moyo ukamuenda mbio.
“Excuse me “ akasema Happy huku akiinuka na kusogea pembeni akabonyeza kitufe cha kupokelea simu.
“Hallo Patrick “ akasema Happy kwa sauti ndogo
“Happy uko wapi sasa hivi? Patrick akauliza na kumfanya Happy astuke kidogo kutokana na sauti ya Patrick kuwa na mabadiliko
“Patrick mbona sauti yako haiko kawaida? Whats wrong? Happy akauliza kwa sauti na kumfanya Mike astuke baada ya kusikia Happy akitamka jina la Patrick.
“Happy matatizo makubwa yametokea.” Patrick akasema
“Matatizo gani Patrick ? Happy akauliza
“Happy nashindwa hata nianzie wapi kukueleza kwa sababu hapa nilipo nahisi kuchanganyikiwa kutokana na mambo yaliyojitokeza. Kwa sasa niko hapa hospitali kuu ya magonjwa ya moyo kama unaweza ukapata nafasi njoo ili niweze kukueleza kwa undani kilichotokea”
“Patrick umenistua sana nieleze ni kitu gani kimetokea? Happy akauliza kwa wasi wasi
“ Baba amepatwa na shinikizo la damu na tumemleta hapa hospitali hali yake si nzuri hata kidogo” 
“Ok Patrick nakuja sasa hivi” akasema Happy huku sura yake ikiwa imebadilika na alionekana kuchanganyikiwa ghafla.
“Happy nini kimetokea mbona umebadilika ghafla? “ Mike akauliza baada ya kugundua mabadiliko katika sura ya Happy
“Mike…it.s….uuhhmm...Its nothing “ Happy akasema kwa kubabaika.
“Niambie ukweli Happy nini kimetokea? Mbona umestuka na kubadilika ghafla? Mike akauliza akiwa amemshika Happy mkono
“Mike its nothing.take me back home” Happy akasema huku akiutoa mkono wake toka katika mkono wa Mike
“Happy don’t say its nothing wakati nafahamu kabisa kwamba kuna kitu umeambiwa na mtu aliyekupigia simu kilichokustua na kukufanya uwe katika hali hii.Halafu nimesikia ukimtaja Patrick..Ni nani huyo Patrick ? Mike akauliza na kumfanya Happy amtazame kwa mshangao uliochanganyika na uoga ndani yake.
“Niambie happy ,Patrick ni nani ? kwa sababu amekufanya ubadilike ghafla “Mike akauliza hali uso wake ukionyesha wasi wasi mkubwa.
“Mike please take me back home” Happy akasema kwa sauti kali.
Mike akamtazama Happy kwa makini halafu akamsogelea akamshika mabega yake kwa mikono yake na kusema
“happy wewe ni mchumba wangu na unafahamu kwamba ninakupenda na siwezi kuishi bila kuwa na wewe.tafadhali naomba uniangalie machoni na uniambie huyo Patrick ni nani? Mike akauliza
Happy akashindwa kumuangalia Mike usoni akainama chini huku machozi yakimdondoka.
“take me home Mike” happy akasisitiza
“happy hapa hatutaondoka mpaka unieleze huyo Patrick uliyekuwa ukiongea naye simuni ni nani? Na amekupa habari gani ambayo imekufanya ustuke namna hii? Mike akauliza na uso wake ulionesha kwamba hakuwa akihitaji masihara.
“Mike please..not now…don’t bother I’ll take a taxi” Happy akasema akiwa ameanza kupiga hatua kuondoka.Mike akamkimbilia.
“happy samahani.Sikuwa na nia mbaya kukuuliza vile.Yote hii ni kwa sababu ninakupenda na sipendi kukuona ukiwa katika hali hiyo na ndiyo maana nilihitaji kufahamu kilichokusibu .Naomba unisamehe mpenzi wangu” akasema Mike kwa unyenyekevu.Toka wameanza mapenzi yao haijawahi kutokea hata siku moja wakawa katika hali hii. Mike akamfungulia mlango Happy akaingia garini na kisha wakaondoka kurudi nyumbani.
“Kuna jambo ambalo linamsumbua Happy.Nimeanza kuwa na wasi wasi mwingi kuhusiana na mwenendo wake.Naona kuna mabadiliko makubwa sana.Happy niliyemzoea hakuwa namna hii.Amekuwa ni mwingi wa mawazo na si mchangamfu kama nilivyomzoea.Kuna kitu gani kinachoendelea? Halafu nilisikia akiongea na mtu akamtaja jina la Patrick.Ni nani huyo mtu ? Nakumbuka aliwahi kunisimulia kwamba aliwahi kuwa na mpenzi wake aliyeitwa Patrick ambaye alifariki dunia na ndiyo maana akaamua kunipa mimi nafasi ndani ya moyo wake.Huyu Patrick mwingine ambaye kwa maongezi ya dakika chache ameweza kuibadiisha hali ya Happy ni nani? Kitu gani kimetokea kiasi cha kumfanya Happy astuke namna ile na ghafla tu anaamua kurejea nyumbani? Lazima nifahamu kitu gani kinaendelea.Lazima nifahamu jambo gani lialomsumbua Happy.” Mike alikuwa katika mawazo mengi sana
Baada ya kufika nyumbani kwao Happy akashuka ndani ya gari ya Mike na kwa haraka akaingia chumbani kwake,akachukua ufunguo wa gari lake na kutoka kwa kasi.
Mike alikuwa amesimama na Margreth wakijadili jambo wakati Happy alipotoka ndani kwa kasi na kuingia katika gari lake.Margreth akamsogelea na kugonga kioo cha gari kwa mkono wake .Taratibu Happy akashusha kioo na kumtazama
“happy nini kimetokea? Margreth akauliza
“Maggy tutaogea baadae.I need to see Patrick now.Kuna tatizo kubwa limetokea.” Akasema happy huku akiwasha gari na kumfanya mdogo wake azidi kushangaa.
“Happy nini kimetokea? Magreth akajaribu kuuliza lakini tayari Happy alikwisha liwasha gari lake na kuondoka kwa kasi.
“Mike nini kimetokea? Mbona Happy amebadilika ghafla hivi? Margreth akamuuliza Mike ambaye bado alikuwa amesimama asiamini kilichotokea
“hata mimi nilitaka kukuuliza swali kama hilo kwa sababu nimegundua kuna mabadiliko makubwa sana kwa Happy.Si Happy yule niliyemzoea.Kitu gani kinamsumbua? “ Mike akauliza
“Hakuna jambo lolote amekueleza huko mlikokuwa? Margreth akauliza
“hapana Margreth.Happy hajanieleza jambo lolote lile.Kwani kuna nini? Mike akauliza.Margreth akainama chini.
“Ninachokikumbuka ni kwamba kuna wakati nilimuona amezama katika mawazo mengi ikanilazimu kumuuliza ni kitu gani kinachomsumbua .Akaniambia kwamba kuna jambo ambalo limekuwa likimuumiza kichwa na alipotaka kunieleza simu yake ikaita na sielewi aliambiwa kitu gani na huyo aliyempigia simu kwa sababu alibadilika ghafla sana na akaniomba nimrudishe nyumbani.” Mike akasema na kumtazama Margreth.
“Margreth ,kuna jambo ambalo hata mimi limekuwa likiniumiza kichwa sana.” Mike aksema
“Jambo gani hilo Mike? Margreth akauliza
“Happy alipopigiwa simu alisogea pembeni na kwenda kuongelea huko kitu ambacho haikuwa kawaida yake.Wakati akiongea nilisikia akilitaja jina la Patrick,nikastuka sana.Unaweza ukamfahamu huyo Patrick? Mike akauliza na kumfanya Margreth astuke kidogo halafu akatabasamu na kusema .
“Uhhm …unajua Mike kwa sasa Happy ni mrembo wa Tanzania kwa hiyo atakuwa akipigiwa simu na watu mbali mbali.Usihofu kuhusu huyo Patrick.Huyo ndiye mbunifu wake wa mavazi na ndiye aliyemsaidia sana happy hadi akashinda taji la Miss Tanzania.” Magreth akadanganya huku akitabasamu na kumfanya Mike naye atabasamu.
“Nashukuru sana Margreth kwa kuniondolea huu mzigo niliokuwa nao kichwani kwangu.Tayari nilikwisha anza kuwa na wasi wasi mwingi labda Happy amekutana na Patrick aliyekwisha fariki kwa sababu nakumbuka jinsi Happy alivyokuwa akimpenda.” Mike akasema
“Usiwe na wasi wasi Mike.Jisikie amani.halafu kitu kingine unachotakiwa kukifahamu kwa sasa ni kwamba happy anahitaji kuvumiliwa kwa sababu hakuzoea kuishi maisha haya ya kufuatiliwa kila siku mara na waandishi wa habari n.k.Anahitaji muda ili kuweza kuiweka akili yake sawa sawa kwahiyo kuna mambo ambayo anaweza akayafanya ambayo yanaweza yakakuudhi lakini naomba usichukie na uendelee kumvumilia” Margreth akamweleza Mike
“Nakusukuru sana Margreth nimekuelewa vizuri”Mike akasema huku akitabasamu.
“Happy amekwambia anakwenda wapi? Mike akauliza
“hapana hajanieleza ni wapi anaelekea.Karibu ndani upumzike wakati ukimsubiri” 
“Nashukuru sana margreth lakini kwa kuwa sina uhakika kwamba atarudi saa ngapi mimi naona itakuwa vyema kama nikiondoka nitaonana naye kesho” Mike akasema na kuingia katika gari lake akaondoka.
“Nilimuonya Happy kuhusiana na mpango wake wa kuachana na Mike.Inavyoonekana hajamweleza kitu chochote Mike na hivyo kuzidi kumfanya awe na mawazo mengi sana.Happy Anasema Patrick amepatwa na matatizo,ni matatizo gani hayo? Nahisi yanaweza yakawa yanahusiana na huu mpango wao wa kuachana na wapenzi wao wa sasa ili waweze kurudiana.Namuonea huruma sana dada yangu ,yuko katika wakati mgumu.” Akawaza Margreth akitembea taratibu kuingia ndani.



ITAENDELEA......


TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU πŸ”ž SEHEMU YA 11

MCHUNGAJI MCHAWI, EPISODE:08

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5