JINI WA DARAJA LA SALENDA SEHEMU YA 7&8
SIMULIZI: JINI WA DARAJA LA SALENDA
MTUNZI: ALLY MBETU
SEHEMU YA SABA NA YA NANE
ILIPOISHIA: Kila aliyemuona hakumdhania vibaya, aliacha eneo la bahari na kuingia makazi ya watu, alipokaribia maeneo ya nyumba ya mganga aliuona moto ukiwaka tena. Alikwenda kwenye nyumba ya jirani na kuomba kupumzika, kutokana na kuonekana mstaarabu alikaribishwa na kupewa kiti. Mwenyeji wake hakujishughulisha naye aliendelea na shughuli zake na kumuacha Kulani akitupia jicho njia ya kutokea kwa Mganga Njiwa Manga. SASA ENDELEA... Muda ulikwenda bila mganga kuonekana, kila alipopata wazo la kwenda kwenye nyumba ile alishangaa kuuona moto ukiwaka, lakini ulipotulia nyumba ilikuwa katika hali ya kawaida. Alijikuta yupo kwenye wakati mgumu akiamini kabisa ngoma ile ni nzito kwake kuchezeka. Kilichomchanganya zaidi ilikuwa ni kauli ya mfalme Barami Hudirud ya kuhakikisha anammaliza mganga
ndipo arudi, japo muda aliopewa ulipita. Kulani alipata pigo baada ya mwenyeji wake kutaka kuondoka, akiwa bado kichwa kinamuuma alimwambia: “Samahani kaka.” “Bila samahani.” “Nataka kuondoka kwenda pwani.” “Hakuna tatizo funga mlango wako mimi niache hapa nimekaa baada ya muda nitaondoka.” “Hapana kaka sikujui nimekukaribisha kibinadamu, lakini siwezi kukuamini kukuachia nyumba yangu, dunia haiaminiki siku hizi.” “Sawa.” Kulani alikubali kuondoka pale, lakini sehemu iliyokuwa nzuri kupaona kwa mganga ilikuwa kwenye nyumba ile iliyokuwa ikitazamana na ya mganga. Aliondoka kwa kuzunguka nyumba ile na kujigeuza haraka kuwa mjusi. Aliupanda ukuta haraka na kwenda kujificha chini ya bati bila kuonekana. Mwenye nyumba ile alishtuka na kuzunguka nyuma ili kupata uhakika kama kweli yule mgeni atakuwa ameondoka. Lakini ajabu alipozunguka nyuma ya nyumba iliyokuwa na uwazi mkubwa wa kumuona mtu kama anatembea kutoka pale, hakumuona mgeni wake. Alijiuliza kwa sauti: “Sasa atakuwa amekwenda wapi, mtu azunguke sasa hivi asionekane, mmh! Lisiwe jini lile, Mungu aniepushie mbali.” Kulani alimtazama na kutulia akiwa amejilaza kwenye ukuta chini ya bati. Baada ya kusema yale mwenye nyumba ile aliondoka na kumwacha Kulani palepale nyumbani bila kujua. Baada ya kuondoka, Kulani aliendelea kumsubiri mganga palepale ukutani chini ya bati katika umbile lile lile la mjusi kama atatokea Mganga Njiwa Manga amvae na kumuulia mbali. Alisubiri kwa saa kumi mpaka jioni ilipoingia ndipo alipomuona akiwa anamsindikiza mmoja wa wateja wake. Jini Kulani aliteremka na kurudi katika umbile la mwanadamu na kumfuatilia kwa nyuma bila ya mganga kujua. Nia yake ilikuwa kukutana naye wakati anarudi ili amvae. Taratibu alitembea kumfuata kwa nyuma mganga aliyekuwa mbele akitembea huku akizungumza na wateja wake. Njiani Mganga Njiwa Manga alianza kuhisi kama ardhi inatetemeka na mwili kuwa mzito, kitu kile kilichomfanya ageuke na kutazama nyuma. Alishtuka kukiona kiumbe cha ajabu kwa mbali kikija taratibu. Kwa haraka alichutama chini na kushika michanga huku akilikemea jitu lile ambalo liligundua limejulikana. Wakati Kulani akijitayarisha kumvaa Mganga Njiwa Manga baada ya kugundua amejulikana, kabla hajamfikia alirusha vumbi la mchanga lililomuingia machoni na kumpofua macho. Alipiga kelele za maumivu na kujipiga chini kwa hasira na kusababisha kishindo kizito kilichotikisa eneo kubwa la Bagamoyo. Kishindo kile kilisababisha watu waliokuwa karibu na sehemu kilipotokea waanguke na kupoteza fahamu. Nyumba nyingine zilipata nyufa kutokana na kushindo cha Kulani kupasua ardhi na kupotea. Baada ya robo saa hali ya eneo la Bagamoyo ilirudi kuwa ya kawaida. Baada ya kurudi hali ya utulivu Mganga Njiwa Manga alinyanyua alipokuwa ameangukia baada ya kurushwa na udongo uliotoka kwenye shimo alilozama jini Kulani baada ya kupofuka macho. Alimtuma mtu kwenda nyumbani kumletea dawa ambayo alikunywa na kujimwagia kichwani. Baada ya kuyafanya yale alikwenda hadi kwenye shimo lililokuwa limechimbika kama kumelipuka bomu. Sehemu ile aliweka dawa kisha aliondoka na kurudi nyumbani kwake. Alipofika nyumbani mwili ulikuwa umechoka sana, hakuweza kuendelea na kazi ya matibabu, aliwaomba wagonjwa wake apumzike baada ya kunusurika kifo toka kwa jini ambaye hakujua ametoka wapi. Siku ile hakufanya kazi yoyote, alilala mpaka siku ya pili huku akiviona viungo vyake vikipoteza nguvu. Hata alipolala hakuweza kujigeuza mpaka siku ya pili, kwake ulikuwa upinzani mkubwa katika kazi yake. Mara nyingi upinzani uliishia nje ya ngome yake, lakini hakikuwahi kiumbe chochote cha ardhini majini au angani kilichoweza kumdhuru. Pia katika kazi yake haikuwahi kutokea kiumbe kilichowahi kumvizia njiani kwa ajili ya kumdhuru. Wengi walivamia sehemu aliyokuwa akifanya kazi na kukutana na vikwazo. Lakini uwezo wa kinga yake ya mwili ndiyo uliomsaidia, bila hivyo angemalizwa na jini yule. *** Jini Kulani baada ya kuzama chini ya ardhi kwa kujipigiza kwa hasira, aliibukia pembeni ya bahari. Alitembea taratibu huku akipapasa ili kuingia majini. Baada ya kutembea kwa muda alibahatika kuyakanyaga maji. Pale pale alizama chini. Mfalme wa bahari alishangaa kumuona Mkuu wa Watwana Kulani amesimama mbele yake akiwa haoni. “Kuna nini tena kimekusibu mtwana wangu mtiifu?” “Mtukufu mfalme, safari yangu imekuwa mbaya.” “Kulani umefanya makosa, kwa nini jana hukurudi?” “Niliogopa mtukufu mfalme kurudi bila kutimiza ulichonituma.” “Umekitimiza?” “Hali yangu kama unavyoniona.” “Tatizo nini?” “Nimepofuka mtukufu mfalme.” “Lakini hujanijibu, umemmaliza?” “Sikuweza, yule mtu hata wewe sikushauri uende.” “Kwa nini?” “Amejidhatiti, ana nguvu za ajabu sijawahi kuona, ameizindika ngome yake haiingiliki, na yeye mwenyewe alichonifanya sitasahau mpaka nakufa.” Jini Barami Hudirud, mfalme wa bahari atakubali ushauri wa Kulani kuachana na Mganga Njiwa Manga?
“Hapana lazima niende, hawezi kushindana na nguvu zangu.” “Mtukufu mfalme, bado himaya ya chini ya bahari inakuhitaji lazima atataka kutumia nguvu za ziada kukumaliza. Nashukuru sikugusana naye ningeweza kupoteza maisha.” “Kwa hiyo tuwaache wanadamu watuchezee?” “Hapana, ila nguvu zinazidiana, yule mwanadamu ana nguvu za ajabu sana, nilijitahidi kuuzima moto alioutega kwenye himaya yake, nilishindwa kila nilipouzima na nilipotaka kuingia uliwaka tena nikajikuta kukipambazuka bila ya kuweza kuingia kwenye himaya yake. Ndiyo sababu ya kuchelewa kurudi na kuamua kubaki ili nihakikishe nammaliza akitoka kwake. Lakini haikuwa hivyo matokeo yake nimekuwa kipofu.” “Mmh! Nimekuelewa, basi mpelekeni akapate tiba.” Watwana wengine walimchukua Kulani na kwenda kumpatia tiba ya macho, baada ya kuondoka, mfalme alimgeukia mkewe aliyekuwa kimya akimuangalia Kulani kwa huruma. “Mke wangu umeona hali ilivyo, unanishauri nini kutokana na hali aliyorudi nayo Kulani?” “Mmh! Mume wangu hali inatisha, inaonesha wazi vita ni nzito, tukifanya mchezo tutakwisha, mpaka Kulani kusema hivyo ujue kuna kazi. Kwa nini tusiachane na mpango wa kumfuatilia huyo mwanadamu?” “Lakini mke wangu si unajua uwezo wangu? sijawahi kushindwa na kitu,” Mfalme alijitapa. “Naujua vizuri, hata Kulani anaujua lakini mpaka kakukueleza vile naomba umsikilize huenda kuna kitu amekiona kinaweza kukupotezea maisha kama utashindana na yule mwanadamu.” “Lakini kumbuka jini ana nguvu kuliko mwanadamu?’ “Lakini mwanadamu ndiye kiumbe mwerevu kuliko viumbe wote wa Mungu?” “Hilo nalijua lakini bado hawawezi kushindana na sisi.” “Mume wangu majini sisi hatuna ushirikiano, kuna majini wengine huwakinga mwanadamu na kuwafanya kuchanganya nguvu za kijini na akili ya kibinadamu lazima tu atakushinda.” “Kwa hiyo tufanye nini?” “La muhimu tuachane na mpango huo.” “Na suala la Balkis kuolewa na jini mwenzake?” “Hilo nalo ni gumu, tuendelee kumshawishi aweze kubadili mawazo na kuendelea na kazi ya kukusanya vizazi vya wanadamu na kutengenezewa dawa.” “Mimi nina hasira, jaribu kuongea naye wewe.” “Nitafanya hivyo jioni nitazungumza naye.” Walikubaliana mke wa mfalme azungumze na Balkis ili aweze kubadili uamuzi wake wa kung’ang’ania kuolewa na mwanadamu. **** Baada ya kuamka siku ya pili, Mganga Njiwa Manga bado mwili wake haukuwa na nguvu, wagonjwa wengi waliofika siku ile hawakupata huduma kutokana na hali yake. Ilibidi siku ile na yeye kutumia dawa za kujifusha na kunywa ili kujirudisha katika hali ya kawaida, baada ya kukumbwa na upepo wa jini Kulani. Kilichomshangaza kilikuwa rangi ya jini yule, alikuwa mweusi kama rami tofauti na majini wote aliowahi kukutana nao. Siku ya pili tangu akutane na dhahama nzito ya jini Kulani, aliendelea na kazi ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotoka mbali. Baada ya kuingia katika chumba chake kutoa huduma, alitulia kwenye mkeka kisha aliweka ubani kwenye kitezo na kutulia kwa muda ili ajiandae kwa matibabu ya wagonjwa waliokuwa wameongezeka kutokana na kusimama kwa huduma yake. Ilikuwa ajabu baada ya moshi wa ubani kupanda juu, ulimfuata mbele ya uso wake na akaanza kuona picha asiyoielewa. Alikiona kiumbe cha ajabu kikitoka kwenye maji na ghafla kiligeuka na kuwa mwanadamu, kisha kilitembea taratibu toka kwenye ufukwe na kuingia maeneo ya watu. Baada ya kiumbe kile kilichojigeuza kuwa binaadamu kukaribia ngome yake, kilijigeuza umbile na kurudia lile alilotoka nalo chini ya maji. Ajabu kilipotaka kuingia kwenye himaya yake aliona moto ukiwaka kuzunguka eneo lake, ghafla kiumbe kile kilitoka mbio kurudi baharini na kuchota maji kisha kuja kuzima moto. Kiliendelea kuzima moto mpaka kulipopambazuka, kila kilichoendelea alikiona mpaka kupambana na jini lile. Hapo ndipo alipogundua jini lile lilitoka wapi, alicheka na kuona kinga aliyokuwa nayo ndiyo iliyomsaidia bila hivyo angekufa vibaya. Taratibu moshi ulipungua na hali ya ndani ikarudi kuwa ya kawaida, Mganga Njiwa Manga aliendelea kuweka tena ubani uliotoa moshi wa kawaida bila kuwepo na kitu kisichokuwa cha kawaida. Alimtuma msaidizi wake kuwaita wagonjwa. Nini kiendelea baada ya mganga kuonekana kudhibiti nguvu za kijini? Je, nini hatma ya Brighton katika chumba cha giza?
CHINI YA BAHARI Malkia Huleiya, mama mzazi wa Balkis alikwenda hadi chumba cha giza na kuomba Balkis atolewe, baada ya kutolewa alimpeleka kuoga na kukaa naye kwenye pwani ambayo huitumia kupumzika familia ya kifalme. Muda wote Balkis alikuwa akibubujikwa na machozi. Baada ya kukaa kimya kwa muda malkia Huleiya alimwita mwanaye. “Balkis” “Abee mama.” “Najua utatuona sisi wazazi wako makatili lakini unajua kabisa ubaya wa wanadamu na pia ni aibu jini kutoka katika ukoo wa kifalme kuzaa na mwanadamu.” “Mama kabla ya kuzungumza lolote naomba mumtoe mpenzi wangu na kama hamtaki awe huku naomba mumrudishe duniani.” “Hakuna tatizo.’ Alitumwa mtu kwenda kumtoa Brighton kwenye chumba cha giza na kumpa maji ya kuoga kisha kuwekwa kwenye chumba kizuri. Baada ya hatua zile mazungumzo yaliendelea. “Nina imani imefurahi?” Mama yake alimuuliza. “Siwezi kufurahi kwa vile sijatimiza dhamira yangu.” “Ipi?” “Ya kuolewa na mwanadamu.” “Hilo ndilo baba yako hataki kusikia.” “Lakini kumbuka tunachokifanya hakimpendezi Mwenyezi Mungu.” “Kipi hicho.” “Cha kuwafanya wanawake matasa.” “Ni kweli, lakini tunafanya hivyo kwa ajili yako.” “Kama unaona kufanya vile ni dhambi kwa nini msiniache na mpenzi wangu aliyekuwa tayari kukaa huku hata watoto wangezaliwa wangekuwa wetu.” “Mwanangu hujui vita ya wanadamu ni kubwa, huwezi kuamini kizazi kimoja kimechukuliwa. Kama kizazi kimechukuliwa je, mwanadamu watakubali aishi huku?” “Mwanadamu kanipenda mwenyewe wala sikumlazimisha.” “Lakini si ana mchumba wake?” “ Alimkana mbele yangu na kuwa tayari kunioa.” “Kwa sababu hakujua kuwa wewe ni jini.” “Hata alipojua alikubali ndiyo maana nimekuja kuishi nae huku.” “Lakini kumbuka baba yako alikuwa akikutegemea sana, ulichokifanya kimemchanganya sana.” “Lakini mama tatizo nini, kutafuta vizazi vya wanawake na kuzaa bila vita na wanadamu kipi bora, ona kama ulivyoniambia mkuu wa watwana Kulani kawa kipofu, kwa nini tusiachane na vita na wanadamu ili hamu ya mtoto apatikane bila kupata madhara zaidi.” “Uamuzi wako umemuweka baba yako katika wakati mgumu, kumbuka anakupenda kuliko kitu chochote, hakuota hata siku moja utamkosea heshima.” “Ni kweli najua baba ananipenda lakini alitakiwa kunisikiliza kuliko kuchukua maamuzi mazito, ona katumia nguvu nyingi matokeo yake Kulani kawa kipofu.” “Balkis mwanangu hakuna jini anayekubali kushindwa na mwanadamu.” “Ni kweli lakini kuna wanadamu nao huamini kabisa majini hawawawezi, kama wameweza kuchukua kizazi kimoja wanashindwa nini kuvichukua vyote?” “Balkis mwanangu kama ungekwenda kwa kitu tulichokutuma, nina imani kazi yako ingekuwa nyepesi sana kuliko ulichokifanya cha kuanzisha uhusiano na mwanadamu. “Kitendo kile kilituchanganya sana hasa baba yako, hata kuzungumza na wewe alishindwa na kunituma mimi. Anaamini hata matatizo ya Kulani chanzo ni wewe.” “Chanzo ni mimi kwa vipi? Wakati niliwakataza tuachane na vita na wanadamu lakini mkawa wabishi.” “Balkis mwanangu naomba uifanye kazi tuliyokutuma, tunaamini wewe ni mtoto mwenye heshima na usikivu. Nakuomba chonde chonde mwanangu msikilize baba yako.” “Mamaa kwa nini msinikubalie, kwani kuna ubaya gani?” “Kumbuka baba yako ni mfalme wa majini, ni aibu kwa mwanaye kuolewa na mwanadamu, ndiyo maana alikutuma kutafuta kizazi cha mwanamke ili kuhakikisha unapata tiba na kuolewa na jini mwenzako.” “Kwa hiyo nimrudishe Brighton duniani?” “Ikiwezekana.” “Mbona unasema ikiwezekana.” “Lazima tumuulize baba yako ataamua nini juu ya mwanadamu aliyejua siri yetu.” “Sasa naona unataka kuharibu mazungumzo, mmenikataza kuolewa na mwanadamu basi nimrudishe kwao.” “Lakini si atakuwa amejua siri yetu?” “Sasa mnataka kumfanya nini?” “Sijajua mpaka tupate maelekezo ya baba yako.” “Sikiliza kama nimekubaliana na uamuzi wenu wa kuachana na mwanadamu ili niendelee na kazi yangu ya kutafuta vizazi vya wanawake, naomba kwenye suala la kurudi kwao mpenzi wangu msiniingilie.” “Lakini kumbuka mwanangu chini ya bahari hii mwenye sauti ya mwisho ni baba yako.” “Hata awe na sauti gani uamuzi wowote tofauti na kumrudisha duniani hatutaelewana.” Nini hatima ya Brighton? Je, ataruhusiwa na mfalme kurudi duniani baada ya kuijua siri ya majini?“Mbona umefika mbali, ngoja nimpelekee taarifa hizi, atafurahi sana kusikia kuwa umekubali kurudi dunia kutafuta vizazi vya wanawake. Pia nitamueleza suala la mpenzi wako la kurudishwa duniani. Siamini kama atakuwa na maamuzi mazito ya kukuumiza.” “Mmh! Haya basi naomba nafasi ya kuzungumza na Brighton.” “Mmh! Basi ataletwa huku ili baba yako asijue chochote.” Baada ya kusema vile, Huleiya aliondoka na kumuacha Balkis akiwa amejilaza kwenye kiti cha uvivu. Japo moyo ulimuuma kumuacha Brighton mwanaume aliyeamini ndiye mume wa maisha yake. Bado hakuamini kama anaweza kutoa siri za majini. Lakini aliamini hakuwa akijua lolote katika siri za chini ya bahari kutokana na kufikia kwenye chumba cha giza. Baada ya muda Brighton alifikishwa bustanini na kukutana na Balkis, baada ya kukutana Balkis alimueleza hali halisi na yeye kuwa tayari kumrudisha duniani. Kwa upande wake Brighton alijikuta akizama kwenye dimbwi la mahaba ya Balkis na kumuomba atafute njia yoyote ili asirudishwe duniani. “Mpenzi kwa nini usimbembeleze baba yako ili tuishi pamoja?” “Hilo ndilo lilikuwa lengo langu lakini limeleta mtafaruku mkubwa ndani ya familia. Kwa hiyo nakuomba ukubali kurudi duniani ila sitakuwa mbali nawe.” “Mmh! Sawa lakini nitalikosa penzi lako.” “Ni kweli, lakini lazima nikubaliane na matakwa ya wazazi wangu.” “Sawa, sina jinsi,” Brighton alikubali kwa shingo upande. Malkia Huleiya baada ya kuzungumza na mwanaye alipeleka taarifa ya kikao kwa mumewe mfalme Barami. Alipofika alimkuta akimsubiri kwa hamu. “Karibu malkia wangu.” “Asante mfalme wangu.” “Mh, nijuze yaliyojiri huko?” “Mmh! Namshukuru Mungu yamekwenda vizuri.” “Kakubali?” “Ndiyo.” “Ooh! Afadhali.” “Lakini..” “Lakini nini tena malkia wangu?” Mfalme alishtuka. “Kuhusu yule mpenzi wake.” “Ana nini?” “Anataka arudishwe duniani.” “Ina maana hajui sheria yetu mwanadamu anayejua siri zetu huwa harudi tena duniani?” “Hapo ndipo penye tatizo.” “Tatizo gani?” “Mwanao anataka amrudishe duniani.”
“Haiwezekani.” “Amesema iwe isiwe lazima tumrudishe duniani.” “Yeye ni nani anayetaka kutulazimisha tufanye anavyotaka, siwezi kuwa na sauti mbili katika himaya yangu ya chini ya bahari.” “Lakini mume wangu..” “Hakuna cha lakini, aendelee na kazi ya kutafuta vizazi tena tutampangia kwa siku moja alete vingapi ili awahishe kutimiza lengo la kuolewa tuondokane na adha hizi.” “Mume wangu si vyema kila wakati kutumia nguvu, ifike wakati mwingine uwe unawasikiliza walio chini yako.” “Siwezi, nasema kauli yangu ni ya mwisho na maamuzi yangu yaheshimiwe,” mfalme alikuwa mkali. “Mume wangu hii itakuwa vita nyingine, kwa jinsi nilivyomsikiliza mwanao hawezi kukubali hili.” “Nitakachomsikiliza ni kumuacha hai, lakini si kumrudisha duniani.” “Mwanao amesema kwa hili hamtaelewana.” “Hebu kamlete hapa,” mfalme alisema kwa hasira. Alitumwa kijakazi kumfuata bustanini, Balkis alifika mbele ya baba yake kusikiliza kile alichoitiwa. “Abee mtukufu mfalme,” Balkis aliitikia akiwa amesimama mbele ya baba yake. “Kwanza nimefurahi kusikia umeweza kubadili uamuzi wako ila umeniudhi kwa kunilazimisha nifanye utakavyo.” “Baba kukulazimisha kitu gani?” “Kuhusu kumrudisha mwanadamu duniani.” “Sasa tatizo liko wapi? Mmemkataa asinioe sasa si nimrudishe nilipomtoa.” “Ina maana hujui sheria za majini, kama mwanadamu atajua siri zetu?” “Nazijua lakini huyu nimemleta miye hakujileta mwenyewe, wala hakuletwa kwa lipizo.” “Sheria za huku mwanadamu yeyote atakayeingia huwa hatoki salama, lakini kwa heshima yako hatutamuua bali ataishi huku milele.” “Kwa hilo baba sitakubali hata kwa kukatwa kichwa, ni mimi ndiye niliyemlazimisha kuja huku iweje mumshikilie?” “Hiyo ndiyo sheria ya huku kamwe haibadiliki.” “Nasema kwa hili itabadilika.” “Tunabisha?” “Hatubishani ukweli ndiyo huo, ikifanywa kinyume nikiondoka hapa sitarudi tena.” “Sooba,” alimwita mtwana msaidizi wa Kulani kwa sauti ya juu. “Rabeka mtukufu mfalme,” Sooba aliitika na kusimama imara mbele ya mfalme. “Mpeleke huyu kwenye chumba cha giza.” Balkis alichukuliwa tena na kurudishwa kwenye chumba cha giza. Nini kiliendelea?
ITAENDELEA........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni