JINI WA DARAJA LA SALENDA SEHEMU YA 6
SIMULIZI: JINI WA DARAJA LA
SALENDA
MTUNZI: ALLY MBETU
SEHEMU YA SITA
IIPOISHIA; “Ewe mwanadamu, acha kumkosea heshima mtukufu mfalme, kila utakalojibu tanguliza neno mtukufu mfalme.” Mkuu wa watwana alimkumbusha tena Brighton. “Ndiyo mtukufu mfalme.” “Vizuri, Balkis.” “Mtukufu Mfalme.” “Unajua sababu ya kukutuma duniani?” “Ndiyo mtukufu mfalme.” “Mbona imekuwa kinyume?” “Mtukufu mfalme nimekwisha kujibu kila kitu.” “Bado hujanibu.” “Unataka jibu gani mtukufu mfalme?” “Sababu kuu ya kukutuma huko, hujanijibu.” “Ni kweli mtukufu mfalme shida kubwa ni kuongeza familia yetu.” “Sasa kwa nini umekaidi amri yangu, nakuomba urudi duniani akaifanye kazi niliyokutuma.” SASA ENDELEA... “Mtukufu mfalme, kupitia huyu mwanadamu nitapata mtoto unayemtaka. Nina imani tatizo lilikuwa damu zetu kukosa virutubisho. Lakini damu ya mwanadamu huwa ina virutubisho vingi.” “Hatutaki mtoto mchanganyiko.” “Lakini mtukufu mfalme si atakuwa mwanangu?” “Sipo tayari kuchanganya damu.” “Mtukufu mfalme, nami sipo tayari kumpoteza mpenzi wangu.” “Tunabishana?” mfalme Barami alikuja juu. “Baba hatubishani, ila ukweli ni huo.” “Mwana wa mfalme mwite mtukufu mfalme si baba,” mtwana mkuu, Kulani alimwambia Balkis aliyekuwa amemvunjia heshima baba yake na kusimama wima. “Wewe nani unayeingilia mazungumzo na baba yangu? Nani kakupa ruhusa ya kunikemea. Huna heshima, kibaraka mkubwa wee,” Balkis alimfokea mkuu wa watwana. “Balkis umekosa heshima?” mfalme Barami alimfokea mwanaye. “Sijakosa baba, natetea haki yangu.” “Kulaniiii, wachukueni mkawaweke kwenye chumba cha giza haraka.” Mfalme Barami alisema kwa sauti ya juu baada ya kumuona mwanaye amemvunjia heshima. Kulani na wenzake waliwabeba juu juu na kwenda kuwafungia katika chumba cha giza. **** Suzana alishtuka siku ya pili na kujikuta akiwa amelala kwa mara nyingine kitandani kwake. Alijiuliza kuwa pale kitandani ni kweli au anaota, kumbukumbu zake zilimkumbusha kuwa jana yake alitoka nyumbani na kwenda ofisini na kisha alitoka. Breki yake ya kwanza ilikuwa ofisini kwa shoga yake Sharifa na kumuelezea yaliyomsibu baada ya kulala kwa mpenzi wake Brighton, lakini ajabu siku ya pili alijikuta kitandani kwake. Alikumbuka baada ya kumuelezea shoga yake alimpa ushauri kabla ya kufanya lolote aende kwa Brighton kupata ukweli kama ni ndoto au kweli. Suzana akiwa bado amekaa kitandani aliendelea kuvuta kumbukumbu ya mambo aliyoyafanya jana yake. Alikumbuka baada ya kushauriana na Sharifa aliaga kazini na kwenda moja kwa moja kwa mpenzi wake. Alipofika Brighton alionesha kubabaika hata majibu yake yalikuwa kama mtu aliyemfumaniwa. Baada ya hapo hakumbuki kilichoendelea mpaka alipoamka na kujikuta tena kitandani kwake. Tukio la kujikuta kwake tena wakati anaamini jana asubuhi alikwenda kwa Brighton lilizidi kumchanganya akili. Kabla hajafanya lolote simu yake iliita alipoangalia ilikuwa ya Sharifa, aliipokea na kuzungumza. “Haloo Sharifa.” “Eeh, Suzy vipi, ndiyo ukaondoka kimoja na simu ukazima. Lakini hiyo ni tabia gani ukiwa na tatizo tuko pamoja likikuishia ananisahau?” Sharifa alilalamika upande wa pili. “Najua utanilaumu bila kujua.” “Suzy hata kama ulichokifuata kimekwenda vizuri, kwa vile uliniacha na mimi na maswali ulitakiwa kunijulisha.” “Sharifa nashindwa sijui nikuambie nini?” “Uniambie nini Suzy? Kitendo cha kukosa uungwana kwa kweli siyo kizuri hasa tukiwa watu wa karibu.” “Kabla sijakuambia kitu naomba nikuulize swali?” “Uliza tu. ” “Ni kweli jana nilikuja ofisini kwako asubuhi?” “Mbona unaniuliza hivyo?” “Shoga yangu nina maana kubwa sana ya kukuliza hivyo naomba unijibu usinidanganye.” “Ni kweli ulikuja.” “Si nilikuja kukueleza maajabu yaliyonitokea nilipolala kwa mpenzi wangu na kujikuta kitandani kwangu?” “Ndiyo.” “Ni kweli asubuhi sikufanya kazi nilikuaga nakwenda kwa Brighton.” “Ndiyo.””Basi dada yangu yaliyonitokea juzi kuamkia jana ndiyo aliyonitokea jana kuamkia leo.” “Una maana gani kusema hivyo?” Suzana alimweleza yote aliyokutana nayo na siku ya pili alipoamka na kujikuta kitandani kwake. “Suzana usiwe unachanganya mambo, pengine ulipotoka hapa badala ya kwenda kwa Brighton ulikwenda kwako ukalala na kupitiwa na usingizi mzito?” “Sijafikia huko kiasi cha kupoteza kumbukumbuku hivyo, nilipotoka ofisini nilikwenda moja kwa moja kwa Brighton. Jamani hata kama nilirudi nyumbani asubuhi ile ndiyo nilale nishtuke asubuhi ya siku ya pili?” “Mmh! Suzana kuna tatizo.” “Yaani huwezi kuamini sasa ndiyo inajidhilisha kuwa kuna kitu kinanichezea akili.” “Kwani Brighton yeye anasemaje?” “Lazima na yeye atakuwa na tatizo, siku mbili hizi simwelewi kabisa, amekuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.” “Suzana umezidi ubishi kila kitu nilikueleza, lakini hutaki kuamini wacha yakukute.” Suzana yupo njia panda anataka kujua yaliyomzunguka ni kweli au ni ndoto.“Tuache masihara, hebu nipelekwe kwa huyo mtaalamu, kilea kidonda mwisho kukatwa mguu.” “Leo ndiyo unagundua, nilikueleza toka mwanzo kuwa majini wana hadaa inayokuchanganya na mwisho wa siku wanakuingiza sehemu mbaya.” “Sharifa huu si wakati wa kunilaumu, nahitaji msaada wako la sivyo nitachanganyikiwa.” “Kama upo tayari, twende pamoja Bagamoyo.” ”Lini?” “Leo hii.” “Saa ngapi?” “Safari yetu itakuwa saa tatu?” “Basi shoga tutakuwa wote hali inatisha.” Walikubaliana kwenda wote Bagamoyo, baada ya kukata simu Suzana alinyanyuka kitandani ili kujiandaa na safari ya Bagamoyo. Baada ya maandalizi waliingia kwenye gari kwenda nyumbani kwa Sharifa kumpitia kwenda kwa mganga Bagamoyo. Njiani alijitahidi kumpigia simu Brighton simu yake haikuwa hewani, aliachana naye na kuendelea na safari yake mpaka kwa Sharifa. Aliwakuta wameisha jiandaa wakimsubiri, walipomuona tu hawakutaka kupoteza muda. “Jamani tutatumia magari yote?” Suzana aliuliza. “Hakuna haja
ya kutumia magari yote, moja tu linatosha” “Hakuna tatizo.” Walikubaliana kwenda kwenye usafiri mmoja walipanda kwenye gari la Sharifa na kuelekea Bagamoyo. Walitumia dakika arobaini na tano kufika Bagamoyo, walipofika waliuliza wenyeji sehemu aliyopo mganga Njiwa Manga. “Samahani kaka,” Sharifa alimuuliza kijana mmoja aliyepita karibu na mlango wa gari lake. “Bila samahani dada yangu,” kijana yule alijibu huku akisogea karibu. “Habari za saizi?” “Nzuri tu dada.” “Eti, Njiwa Manga anaishi wapi?” “Njiwa Manga! Yupi, yule mganga?” “Eeh, huyo huyo.” “Unaona hii barabara kubwa?” “Ndiyo.” “Ifuateni, acha barabara ndogo mbili zinazokatisha kulia, ya tatu ufuate nenda moja kwa moja mpaka mbele utaona kuna nyumba ina bendera nyekundu hapo hapo kwa mzee Njiwa Manga.” “Asante,” Sharifa alishukuru huku akimpa elfu mbili. “Nashukuru dada yangu.” Waliachana na yule kijana na kufuata maelekezo yake, walipofika barabara ya tatu inayoingia kulia waliifuata na kwenda mwendo kidogo mpaka kufika kwa mganga Njiwa Manga. Walipaki gari sehemu iliyo salama na kutelemka, ilikuwa sehemu yenye eneo kubwa lililokuwa na nyuma kubwa moja na pembeni kulikuwa na mabanda madogo. “Karibuni,” binti mmoja aliyekuwa amevalia gauni refu na kitambaa kichwani aliwakaribisha. “Asante,” waliitikia kwa pamoja. “Karibuni kwenye benchi hapo chini ya mti.” “Asante,” walikwenda wote kukaa chini ya mti kusubiri maelekezo. Ilipita zaidi ya saa nzima bila kupata maelezo yoyote zaidi ya kukaribishwa kana wageni wengine na kuonesha sehemu ya kukaa. “Samahani dada,” Sharifa alimwita yule msichana aliyewakaribisha na kuendelea kuwakaribisha wageni wengine kama watatu, mmoja alikuja na gari na wengine wawili walikuja kwa miguu kuonesha walikuja na usafiri wa daladala. “Bila samahani,” alisema huku akisogea kuwasikiliza. “Eti mganga tumemkuta?” “Yupo, kama asingekuwepo nisingewaacha mkae mpaka muda wote huu.” “Kwa hiyo tutaonana naye saa ngapi?” “Mmh! Sijajua ila si muda mrefu, leo hakuna wagonjwa wengi.” “Wengine wapo wapi?” “Wapo ndani, wakipungua nanyi mtaingia.” “Haya,” waliachana na yule msichana aliyerudi sehemu yake kusubiri wateja wengine. Baada ya nusu saa waliitwa ndani, wakati huo ilikuwa imefika saa tatu na nusu asubuhi. Waliongozana wote watatu mpaka kwenye sebule kubwa iliyokuwa imetandikwa zuria bila kiti. Baada ya kuketi msichana aliyewafuata aliingia chumbani na kuwaacha wasubiri. Ilipita kama robo saa tena waliitwa ndani, waliingia wote watatu. Chumbani kulikuwa na mzee wa makamo aliyeonekana kula chumvi nyingi kutokana na kuenea mvi sehemu kubwa ya nywele zake. Alionekana ni mtu wadini kutokana na mavazi yake ya kanzu iliyokuwa nyeupe sana na juu alivalia kilemba cheupe. Pembeni yake kulikuwa na msahafu. “Asalamu aleykum,” mama Sharifa alimsalimia mganga. “Waleyku msalamu, karibuni.” “Asante,” waliitikia kwa pamoja. “Shikamoo,” Sharifa na Suzana walimwamkia mganga. “Marahaba mabinti zangu, karibuni.” “Asante.” “Haya, mna shida gani?” “Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo alituelekezwa kuja kwako,” mama Sharifa alitoa maelezo mafupi. “Mmh, nimekupateni, nipe majina yao.” Nini kitaendelea, watapata msaada kwa mganga Njiwa Manga?
@@@@@@@@@@@@@@@
ILIPOISHIA: “Haya, mna shida gani?” “Kuna vitu vimewatokea mabinti zangu, mpaka sasa vinawachanganya, japo kuna sehemu tulikwenda na kuelezwa tatizo lao, mmoja hakuwepo na mwisho wa yote ilionesha tatizo lile kwa upande wake ni zito hivyo yule tuliyemwendea alituelekeza tuje kwako,” mama Sharifa alitoa maelezo mafupi. “Mmh, nimekupateni, nipe majina yao.” SASA ENDELEA... “Naitwa Sharifa.” “Jina la mama yako?” “Habiba.” “Mmh! Na wewe mama?” “Naitwa Suzana.” “Jina la mama?” “Monika.” “Vizuri.” Baada ya kuyaandika majina yale kwenye karatasi nyeupe kwa kutumia wino mwekundu, mganga alifungua kitabu kimoja na kutafuta sehemu ya kusoma,alipoipata aliisoma kimya kimya huku akiandika baadhi ya vitu alivyoviona kwenye kitabu kile katika karatasi kwa lugha ya kiarabu. Baada ya robo saa ya kutulia na kusoma huku akiandika, alikohoa kidogo na kusema: “Nimeona vizuri, nina imani yaliyosemwa na mganga aliyetangulia yapo vile vile.” “Haa! Ina maana kweli sina kizazi?” Sharifa alishtuka kusikia vile. “Ni kweli huna kizazi, kilichoelezwa na mganga wa awali hakuna kilichopungua kwako wala kuzidi. Ila kwa Suzana yeye yake yameongezeka.” “Eeh?” Suzana alishtuka. “”Ila msiwe na wasiwasi” “Ninaweza kupona?” Sharifa aliuliza. “Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.” “Na mimi matatizo yangu?” Suzana aliuliza. “Ni kweli kuna mambo yanaonesha hapa yamekuchanganya na kushindwa kuelewa ni kweli au ni ndoto?” “Ni kweli mzee wangu,” alijibu Suzana. “Kilichotokea kwako ni kweli wala siyo ndoto, ni kweli ulilala na mpenzi wako na asubuhi ulipoamka ulijikuta ukiwa kwako. Pia, jana ulipokwenda kuulizia yaliyokutokea juzi kama ni kweli, ulishangaa alfajiri ya leo kujikuta upo tena kwako kitu ambacho kimekuwa kikikuchanganya sana. “Ukweli ni huu, anayewasumbua ni jini la kike linaitwa Balkis, jini huyu yupo chini ya bahari akiwa mtoto wa kwanza wa mfalme wa majini yaliyoko huko. Baba yake anaitwa Barami Hudirud. Wakati alipotakiwa kuolewa alionekana hana kizazi hivyo alipewa kazi ya kuja dunia kutafuta vizazi vya wanawake mia moja kama dawa ya kumuwezesha kushika ujauzito. “Kazi ile aliianza muda mrefu kwa kuja kwa nadra duniani, sehemu yake kubwa ilikuwa Daraja la Salenda ambako aliwaingia wanawake na kwenda nao makwao, usiku alivichukua vizazi vyao na kurudi chini ya bahari. Kazi ilionekana ikienda taratibu mno, hivyo wazazi wake walimuomba aje rasmi duniani ili aweze kupeleka kwa urahisi vizazi vya wanawake wengi na kumfanya awahi kufunga ndoa. “Siku ambayo uliona sherehe ya ajabu ndiyo ilikuwa siku rasmi ya jini Balkis akiagwa kutoka chini ya bahari kuja duniani. “Katika watu mwenye bahati ya kuiona sherehe ile ni wewe na ndiye uliyemvutia jini huyo hadi akaamua kukufuatilia kila ulichokuwa ukikifanya, alipomuona mchumba wako alivutiwa naye, ili ajue siri yako alianzisha uhusiano na mchumba wako bila ya yeye kujua kwa kufanya naye mapenzi kwenye ndoto. “Alifanikiwa kuwapotezeni kwenye ukumbi wa starehe, shida yake kubwa ilikuwa kukuchukua na kwenda kukuficha chini ya bahari ili aweze kuishi na mchumba wako kwa sura yako. Lakini alipokupeleka alikataliwa na wazazi wake kwa vile sicho kitu alichotumwa. “Ile ndiyo iliyokusaidia kurudi duniani bila hivyo ungejulikana kuwa umekufa. “Baada ya kukurudisha aliingia nawe katika vita nyingine ya kuchangia mapenzi, baada ya kuona mapenzi ya mchumba wako yote yapo kwako. “Aliamua kumuondoa nguvu za kiume ili msiweze kufanya tendo lile na yeye alikuja usiku na kufanya naye huku akiwa amemrudishia nguvu zake kamili. “Lakini la kuja usiku ndotoni hakulipenda, alitaka aje kama mwanadamu wa kawaida na kufanya mapenzi ya kawaida ya kutambuana na siyo ya ndotoni. “Aliweza kujitokeza hospitali, mpenzi wako hakujua kama yule ni jini, alimuona kama mwanamke mzuri na kumpa tiba ya ajabu iliyomponya kwa kuzirudisha nguvu zake za kiume. “Bila kujijua mchumba wako akaingia kwenye mtego wa kukubali kuanzisha uhusiano naye, kwa makusudi alipotoka hospitali alikwenda kumsuburi njia aliyojua atapita. “Baada ya kutoka hospitali, alimtafuta bila kumuona na kujikuta akitamani kuonana na
mrembo yule tena. “Wakati anatoka hospitali alikupigia simu mkutane nyumbani ili kukuondoa majonzi yote kutokana na kushindwa kukufikisha katika tendo la ndoa. Hata alipokueleza hukuamini, lakini alikuhakikishia kitu kilichokufanya uahilishe safari ya kwenda kwa mganga kumuangalizia matatizo yake. “Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba wako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, naye kujifanya kana kwamba hana shida na mumeo. “Lakini alimuuliza maswali, kama mumeo angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida.” Mambo yanazidi kufunguka, endelea kujua wasifu wa jini Balkis, nini kitaendelea? Kuyajua yote tukutane baadae
LIPOISHIA: “Nina imani mmebahatika kumuona Balkis jinsi alivyo mwanamke mzuri sana, ambaye hakuna mwanaume atakayemtaka akamkataa. Mchumba’ako akaingia kichwa kichwa kumtaka kimapenzi, kana kwamba hana shida na mumeo, alipoonesha dalili za kumtaka alimuuliza maswali ya mitego, kama angekuwa na akili angetambua kuwa yule si mtu wa kawaida. SASA ENDELEA... Lakini kutokana na kuchanganyikiwa na mapenzi, hakupata muda wa kujiuliza, Balkis alimuuliza maswali kuhusiana na uhusiano wenu, hakushangaa mtu kuonana naye mara ya kwanza kumuulizia vitu ambavyo hata watu wenu wa karibu hawajui. Alipomuulizia kuhusu kumtaka yeye wakati wewe ni mchumba wake, mwenzio alikukana na kusema kuwa wewe ni mpenzi wake si mke wake. Alipoulizwa kama yupo tayari kuoa mwanamke mwingine na kuachana na wewe, kutokana na kiwewe cha mapenzi alikubali kuwa yupo tayari na kuusema udhaifu wako. “Alipoulizwa tena yupo tayari kumuoa yeye Balkis alikubali. Aliutumia udhaifu wa mchumba wako kujenga uhusiano wa haraka na kutaka kuwa naye siku ile, pia alikubali. Walikubaliana kwenda nyumbani kwa mchumba wako, ili kutowagonganisha, mchumba wako alitaka kukupigia simu ili usiende, lakini Balkis alimzuia asikupigie simu na kukueleza uende na ulipokwenda ulimuona jinsi alivyobabaika baada ya kuingia na kwenda moja kwa moja chumba cha wageni alichokuwa ameingia Balkis muda ule ule. Ulishtuka baada ya kumuona ameingia ghafla chumbani, ni kweli?” “Ni kweli,” Suzana alijibu kwa sauti ya chini huku akiwa anaona muujiza mkubwa kutokana na maneno ya mganga ambayo mwanzo aliyaona kama simulizi ya kusisimua isiyo na ukweli. Lakini swali lile lilikuwa kama kitu kilichomtoa kwenye bumbuwazi. “Basi kitendo cha kuingia na kwenda moja kwa moja kilimtia wasiwasi mkubwa mchumba wako kwa kujua lazima utamkuta Balkis na kumfumania. Hata lugha zenu ziligongana kitu kilichokushangaza. Kingine kilichokushangaza kilikuwa kwa mpenzi wako kuwa tofauti na siku zote kukujibu kwa ukali jambo la kawaida. Baada ya kumuona humuelewi, ulikwenda chumba cha kulala, yeye alirudi hadi chumba cha wageni na kushangaa kumkuta Balkis akiwa amejaa tele kitandani. Alipotaka kujua alikuwa wapi alimwambia akuwahi chumbani ili akurudishe kwenye hali ya kawaida. Baada ya kuingia chumbani, penzi alilokupa ndilo lilikuchanganya na kusahau yaliyotokea muda mfupi. Usiku jini Balkis alikuja kukuchukua ukiwa usingizini na kukurudisha kwako na yeye kulala na mchumba wako mpaka asubuhi. Wote mlipoamka mlishtuka lakini hakuna aliyejua ukweli wa tukio la usiku ni kama ndoto au kweli. Ulipokwenda kwake asubuhi ya jana kupata uhakika kwa kilichotokea, ndani walikuwa mchumba wako na Balkis, ndiye aliyemweleza ujio wako. Ulipofika alikuwa mule mule chumbani amelala kitandani. Wewe hukumwona ila mwenzako alimwona kama kawaida, kitu kile ndicho kilichompa kigugumizi. Hali ile ilikuchanganya na kumuona kama mtu mwenye matatizo, wakati huo Balkis alimwambia mchumba wako kwa sauti ya juu ya kumkemea kuwa akikuuliza useme hukuja jana ili ujue kilichotokea si kweli bali ni ndoto. Lakini kwa yeye kuwepo pembeni ya kitanda karibu na Balkis aliyekuwa amelala pembeni yako bila wewe kumuona, ilizidi kumchanganya. Mchumba wako alipatwa na kigugumizi kwa kujua utanamuona Balkis, kubabaika kwake kulikufanya umtilie wasiwasi na kumuuliza swali ambalo lilimchanganya pale ulipotaja jina la Balkis kama jini, jina ambalo lilikuwa la mpenzi wake, kumtaja kama jini ilimuudhi sana Balkis na kukupuliza upepo uliokufanya upoteze fahamu. Kitendo kile mchumba wako alikiona na kumpandishia na kutaka kujua amekufanyia nini, Kauli ile ilimfanya Balkis kukasirika na kuondoa nguvu za kiume za mchumba wako na kutaka nawe kukutoa kizazi.” “Mama yangu!” Suzana alishtuka na kushika mdomo kusikia vile. “Usiogope, hakukutoa kizazi baada ya mchumba wako kumuomba msamaha na kuwa tayari kumuoa baada ya kumkataa kutokana na vitendo vyake visivyo vya kawaida. Baada ya Balkis kumsamehe aliamua kuondoka naye kwenda kuishi chini ya bahari.” “Mamaaa!” Suzana alipiga mayowe ya mshtuko. “Mungu wangu unataka kutuambia Brighton yupo ujinini?” Mama Sharifa aliuliza. “Ndiyo, lakini kwa sasa yupo katika matatizo.” “Matatizo! Matatizo gani tena jamani?” Suzana aliuliza kwa huzuni. “Baada ya kufika katika mji wa majini, baba mzazi wa Balkis alishtuka kuona mwanaye amekwenda na mwanadamu akimsema ndiye mume wake badala kupeleka alichotumwa. Hapo palitokea kutoelewana kati ya Balkis na baba yake, baba akitaka mwanaye arudi duniani kuendelea kutafuta vizazi zaidi vya wanawake ili apate dawa ya kuweza kupata ujauzito ili aolewe na jini mwenzake. Lakini Balkis hakuwa tayari kuolewa na jini mwenzake baada ya kuonja penzi la mwanadamu. Yeye aliamini kuolewa na mwanadamu kusingekuwa na haja ya kuendelea kuwatoa uzazi wanawake. Kwani angekutana kimwili na mwanadamu angeweza kupata bila kutumia dawa hiyo. Hapo ndipo palipozuka mvutano wa mtoto na baba, Balkis aliamini kwa vile anapendwa sana na baba yake atakubaliwa, lakini baba yake hakuwa tayari kuchanganya damu ya jini na mwanadamu. Baada ya kuona mtoto wake amemkosea adabu, alimuamuru mkuu wa Watwana anaitwa Kulani, Jini mweusi lakini mwenye nguvu. Kumchukua Balkis na mchumba wako kuwapeleka katika chumba cha giza.” “Kwa hiyo ndiyo harudi tena?” Suzana aliuliza. “Anaweza kurudi lakini mpaka atoke sehemu aliyofungwa.” “Bila ya hivyo hawezi kutoka?” Sharifa aliuliza. “Inategemea na uamuzi wa mfalme wa bahari kumtoa.” Mambo yanazidi kuwa mazito. Je, Brighton atapona au atauawa katika mji wa majini? Mganga njiwa Manga atawasaidia?
@@@@@@@@@@@@@@@
“Hawezi kumuua?” Suzana aliuliza kwa sauti ya kukata tamaa. “Hawezi, nina imani atatoka tu, kinachotakiwa ni kuvuta subira.” “Mmh! Na mimi tatizo langu?” Sharifa aliuliza. “Wewe tatizo lako limepata bahati moja kubwa ambayo sawa na bahati ya mtende.” “Bahati gani?” Sharifa aliuliza huku akijiweka sawa. “Kitendo cha kufungiwa Balkis katika chumba cha giza, kimewawezesha kuja huku bila ya matatizo. “Una maana gani?” Sharifa aliuliza. “ Majini ni viumbe wasiokubali kuona wanavurugiwa mipango yao, Balkis kama angekuwa hajafungiwa lazima angeizuia safari yenu.” “Angeizuia kivipi?” “Mngekutana na vitu vya ajabu njiani hata kupinduka na gari lenu.” “Si tungekufa?” “Msingekufa, mngeumia tu ili msiweze kumfuatilia.” “Na bahati nyingine?” “Bahati nyingine wakati wa kufanya dawa ya kurudisha kizazi chako hakutakuwa na upinzani wowote. Wala kazi yako haitahitaji vitu vingi vya kufanya na itaanza leo saa sita za usiku baharini.” “Kama angekuwepo?” “Mmh! Pangechimbika, waganga wengi wamepoteza maisha kwa ajili ya kutaka kuvuruga mipango ya majini. Pia tungehitaji vitu vya gharama ili kumdhibiti hapo kazi ingetakiwa kufanyika saa nane za usiku baharini katika maji ya shingo.” “Mmh! Sasa akitoka si ataweza kutuua?” “Balkis ni jini lenye huruma sana, katika maisha yake hapendi kufanya vitu vibaya, hata kuolewa ilikuwa ni shinikizo la wazazi wake tu ambao walimlazimisha kutafuta vizazi vya wanawake ili aweze kupata tiba ya matatizo yake ya kushindwa kupata ujauzito. “Mwanzoni alikataa katakata lakini aliahidiwa kupewa zawadi kubwa kama atapata mtoto hasa wa kiume. Alikubali kuifanya kazi ile kwa shingo upande, lakini moyoni mwake hakupenda hata siku moja kutenda kitendo chochote kibaya kwa wanadamu, siku zote aliwaza kuishi duniani na kuolewa na binadamu. “Hata kazi ya kutoa vizazi ilimchukua muda mrefu sana, kitu kilichowafanya wazazi wake kumleta duniani moja kwa moja ili aweze kupata vizazi hivyo kwa muda mfupi, bila kujua Balkis hakupenda kuifanya kazi ile. “Siku Suzana alipoona sherehe ya ajabu juu ya bahari, hiyo ndiyo ilikuwa siku rasmi ya kuja duniani kwa Balkis kusaka vizazi vya wanawake na kuvipeleka baharini. Aliandaliwa jini mwingine ambaye kazi yake ilikuwa ni kuvipokea vizazi hivyo juu ya bahari katika eneo lile la Daraja la Salenda na kuvipeleka kwenye stoo chini ya bahari. “Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake, tangu Balkis alipofika rasmi duniani kwa kazi hiyo, kwa siku moja alipeleka vizazi vinne tu na chako kikiwa kimojawapo. Kazi aliyotumwa alisahau baada ya kuvutiwa na uzuri wa mchumba wa Suzana na kujikuta akianzisha uhusiano wa siri bila mwenzako kujua. “Katika harakati za kuhakikisha anamdhibiti mchumba wako, muda mwingi aliutumia kuhakikisha anamchukua jumla badala ya kuifanya kazi aliyotumwa. “Aliweza kuwagonganisha kwa kuziua nguvu za kiume za mchumba wako na usiku ulipoingia alizirudisha ili afaidi yeye. “Hali ile ndiyo iliyowasukuma kutafuta suruhu ya tatizo lenu, alipoona mmeanza kupata mwanga aliwachanganyeni kwa kuzirudisha kitu kilichokufanya uone kama hakuna tatizo.Balkis alipofanikiwa kumnasa mchumba wako kwenye mtego wake, hakupanga kuondoka naye mapema. “Mngeendelea kushea mapenzi bila wewe kujua mpaka angeshika ujauzito. “Kosa alilolifanya mchumba wako ni kwenda kinyume na yale aliyokuwa akielekezwa na Balkis. “Kubabaika kwake kulipelekea wewe kuingia wasiwasi na kutamka neno lililomchukiza Balkis na kukupulizia hewa iliyokupoteza fahamu. Hali ile ilimfanya Balkis aone mpango wake umeharibika mapema, ili asiweze kumpoteza mpenzi wako aliamua kuondoka naye kwenda chini ya bahari. “Kutokana na huruma yake aliamini kama ataolewa na binadamu atakuwa ameokoa tatizo la wanawake kutolewa vizazi. Lakini ilikuwa tofauti na walivyotegemea wazazi wake ambao wao walimtuma kuishi duniani ili kufanikisha kupatikana kwa vizazi vingi vya mwanamke vitakavyomuwezesha kupata dawa ya kushika ujauzito ili aolewe na jini mwenzake. “Walishangaa kumuona akiwa na mwanaume wa kibinadamu na kumtambulisha kwao kama ni mume wake. Kitendo kile kiliwaudhi sana, naye hakutaka kukubali.Baada ya mvutano Balkis na mchumba wako waliwekwa kwenye chumba cha giza.” “Sasa kama unasema wazazi wake hawakukubali wataweza kumtoa salama Brighton?” Suzana aliuliza. “Hapa inaonesha maisha yake yapo zaidi ya hapo, Kwa hiyo hawezi kuuawa.” “Kama umeona anaweza kuendelea kuishi, itakuwa wapi duniani au kuendelea kufungwa kwenye chumba cha kiza?” Suzana alikuwa na shauku kutaka kujua hatma ya mchumba wake. “Kwa kweli haioneshi ataishi wapi ila kuna maisha marefu ya mchumba wako.” “Vipi kuhusu kazi yangu ya kurudisha kizazi kuna vitu vinatakiwa kwenda kununua?” Sharifa aliuliza. “Anatakiwa njiwa mwekundu tu, kwenye mabanda yangu anapatikana.” “Na mimi kumpata mchumba wangu utanisaidiaje?”
ITAENDELEA..........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni