JINI WA DARAJA LA SALENDA SEHEMU YA 5
SIMULIZI: JINI WA DARAJA LA SALENDA
MTUNZI: ALLY MBETU
SEHEMU YA TANO
Suzana alikwenda hadi mlango wa chumba cha wageni na kuingia ndani, Brighton mapigo ya moyo yalikuwa makubwa. Alijisogeza hadi kwenye kochi na kujilaza akiwa ameshikilia mkono mmoja kifuani kuizuia presha kutokana na vurugu itakayotokea chumbani. Siku zote Suzana alimhakikishia Brighton kuwa siku atakayomkuta na mwanamke ndiyo siku atakielewa kichaa chake. Akili nyingine ilimtuma awahi chumbani kabla Suzana hajafanya lolote. Alinyanyuka alipokuwa amejilaza na kwenda chumba cha wageni. Alipofika alifungua mlango na kuingia ndani, Suzana aliyekuwa akianua nguo yake ya ndani, alishtuka na kumuuliza: “Vipi mbona umeingia kama unafukuzwa?” “Aa..aa..,” alijibu kwa kubabaika huku akipepesa macho
chumbani kumtafuta Balkis. “Vipi mbona unatembeza macho chumba kizima kuna nini?” Suzana alimuuliza. “Walaa, niliweka CD yangu kwenye meza.” “Sasa ulivyokuja hivyo, umeniona mimi mwizi?” “Walaaa, nilikuwa najiuliza niliiweka huku au wapi?” “Brighton, umeanza lini kuweka vitu vyako humu chumbani?” “Suzana hii ni nyumba yangu, nina uhuru wa kuweka kitu popote.” “Mbona leo Brighton sikuelewi?” “Kivipi?” “Umekuwa mtu mwenye mawazo mengi pia mwenye hasira tofauti na siku zote.” “Nipo sawa.” Brighton bado hakuamini kama kweli chumbani hakuna mtu, wasiwasi wake huenda amekwenda choo cha wote kilichokuwa upande wa mwisho wa nyumba ile. Bila kuongeza neno alitoka na kwenda moja kwa moja msalani ili kumuwahi kama Balkis yuko huko asitoke. Alipofika msalani hakukuta kitu, alijikuta akibaki akilishangaa bafu huku akijiuliza Balkis amekwenda wapi, ikiwa hakuna mlango mwingine wa kutokea. Akiwa bado ameshangaa Suzana alisimama tena nyuma yake na kumuuliza: “Brighton upo sawa?” “Nipo sawa.” “Hapana, kuna kitu kinakusumbua hutaki kuniambia.” “Suzy, nipo sawa.” “Hapana Brighton una tatizo unanificha, mimi nani kwako?” “Mpenzi wangu.” “Nani wa kumueleza shida zako?” “Lakini Suzy mimi sina tatizo lolote,” Brighton aliendelea kujitetea japo maji yalikuwa shingoni. “Sikubali, kuna kitu unanificha, basi mimi nipo chumbani ukimaliza matatizo yako utanikuta.” Suzana alisema huku akielekea chumba cha kulala, baada ya kuondoka Brighton aliendelea kuelea kwenye bahari ya mawazo juu ya kitu kilichotokea muda mfupi pale alipomshuhudia Balkis akiingia chumba cha wageni na wakati huo Suzana alikuwa anaingia. Bila kupumzika, alikwenda moja kwa moja chumba cha wageni alichoingia Balkis. Lakini cha ajabu, Balkis hakuwepo chumbani wala msalani, alijiuliza atakuwa wapi? Alijikuta akirudi tena chumba cha wageni kupata uhakika kama kweli Balkis hayumo. Chumba cha wageni hakikuwa na vitu vingi vya kuweza mtu kujificha, kitanda na tivii ndogo. Alipofungua mlango na kuingia, alishtuka kidogo akimbie alipomkuta Balkis akiwa amejilaza kitandani akiwa amepitiwa na usingizi. Kwake aliona kama maruweruwe, alifikicha macho kutaka kupata uhakika wa kile alichokiona mbele yake. Akiwa bado kapigwa na butwaa, Balkis aligeuka na kufumbua macho, alipomuona Brighton aliachia tabasamu na kusema: “Mpenzi mbona umeingia bila hodi?” “Aah! Ulikuwepo?” “Kuwepo wapi?” “Chumbani.” “Chumba gani?” “Si humu ndani.” “Ndani wapi?” “Sijakuelewa, hebu nieleweshe vizuri, nilikuwa wapi kivipi?” “Muda mfupi ulikuwa wapi?” “Brighton, swali gani hilo? Nimekuaga nakuja chumbani na umekuja umenikuta, sasa unaniuliza swali gani hilo?” “Mbona nimekuja chumbani sikukukuta?” “Hukunikuta! Hapa unazungumza na nani?” “Suzana alikuja huku, kwa wasiwasi wa kukuona ilibidi nije ili isitokee vurugu lakini sikukuona.” “Sijui unamaanisha nini, hebu nenda kwa Suzana ukamuondoe wasiwasi, nimekueleza mapema acha kujitia jakamoyo.” “Umejuaje?” “Ukirudi nitakuambia, muwahi mchumba wako.” Brighton alitoka kwenda chumbani kwake na kumuacha Balkis akimsindikiza kwa macho. Ni kweli Suzana alimuona Balkis? Mbona hakuonekana mwanzo chumbani?Brighton alijitahidi kurudi katika hali yake ya kawaida kabla ya kuingia chumbani. Alipoingia alimkuta Suzana amekaa upenuni mwa kitanda akiwa ameshika tama. “Suzana mpenzi wangu vipi?” “Vipi nikuulize wewe?” “Mbona mimi nipo sawa, hebu twende tukaoge mpenzi wangu tuje tulale.” Alimshika mkono na kumnyanyua kisha waliongozana naye bafuni, baada ya kuoga walirudi kitandani. Kwa vile Suzana alikuwa na hamu na mpenzi wake, baada ya kuikosa huduma ya kitandani kwa muda mrefu. Brighton hakujiamini kwa asilimia miamoja kukifanya alichomuitia mpenzi wake. Lakini ilikuwa kama alivyoelezwa na Balkis kuwa dawa aliyompa inafanya kazi, Suzana aliweza kufurahia mapenzi kwa muda wote, Brighton alijikuta akijisahau kuwa Balkis naye anamhitaji, baada ya kumstarehesha mpenzi wake alipitiwa na usingizi mzito. Ulipofika usiku wa manane Brighton alishtuka usingizini na kujikuta akifanya mapenzi na Balkis tena chumbani kwake. Baada ya penzi tamu la Balkis ambao aliamini hakuwahi kupewa chini ya jua zaidi ya ndotoni. Alipepesa macho mule chumbani labda atamuona Suzana lakini hakumuona. Ili kupata uhakika Suzana yupo wapi alimuaga Balkis kwenda msalani, pamoja na kuwa na choo cha chumbani lakini alitoka kwenda cha watu wote. Ajabu Balkis hakumuuliza chochote, alitoka mpaka chumba cha wageni na kukikuta kitupu. Alikwenda hadi msalani pia hakumuona. Alijiuliza Suzana atakuwa wapi au ameondoka, lakini haikuwahi kutokea Suzana aondoke usiku tena bila kuaga. Alijikuta akijiuliza bila kupata majibu kuwa yupo ndotoni au kweli, alitoka hadi nje ya nyumba lakini hakukuwa na dalili zozote za kuwepo Suzana. Alimfuata mlinzi wa Kimasai na kumuuliza kama Suzana ametoka. “Rafiki shemeji yako ametoka?” “Sijaona yeye ikitoka, niliiona inaingia tu.” “Rafiki lazima ulilala, mbona ndani hayupo?” “Sijasinzia rafiki, shemeji haijatoka imo ndani.” “Kweli?” “Kweli kabisa rafiki.” Brighton aliamini kabisa mlinzi alipitiwa usingizi wakati Suzana anatoka, akiwa bado anajiuliza ni kweli Suzana alikuja au ilikuwa ndoto. Lakini akili yake ilimweleza kuwa Suzana alikuja kweli wala haikuwa ndoto na kufanya naye mapenzi na kila mmoja alipitiwa na usingizi mzito. Lakini aliposhtuka na kujikuta akifanya mapenzi na Balkis tena penzi tamu adhimu, bado alikuwa njia panda kujiuliza kilichotokea ni nini yupo ndotoni au ni kweli. Kwa maelezo ya mlinzi kuwa kweli alimuona anaingia lakini hakumuona anatoka ilizidi kumchanganya. Hata kama kweli alitoka bado asingeondoka bila kuaga, na kitu kile hakikuwahi kutokea toka waanze uhusiano wao. Akiwa bado yupo njia panda kwa kile alichokuwa akikiwaza juu ya kuyeyuka kwa mpenzi wake . Sauti ya Balkis alimtoa kwenye dimbwi la mawazo. “Brighton huku ndiko msalani?” “Aa..aah... nilikuwa napunga upepo.” “Imeanza lini na leo iwe ya pili?” “Ni kawaida yangu wala si leo.” “Kweli?” “Kweli kabisa.” “Kwa hiyo nikuache uendelee kupunga upepo?” “Hapana, wacha turudi ndani.” Brighton alirudi ndani na Balkis, walipofika kitandani bado alikuwa na
mawazo, lakini hakutaka kuumia kichwa alimuuliza Balkis. “Eti Suzana wakati anaondoka ulimuona?” “Swali gani hilo Brighton?” “Ooh! Basi.” “Kwanini unaniuliza habari za mpenzi wako mimi zinanihusu mimi?” Balkis alimuuliza kwa sauti kali kidogo. “Hapana mpenzi, inawezekana ulikuwa ninaota.” “Kuota nini?” “Kuwa Suzana alikuja leo.” “Kama alikuja yupo wapi?” “Inawezekana nilikuwa naota.” “Kama ulikuwa unaota basi tulale,” Balkis alimkumbatia Brighton, hakuchelewa usingizi mzito ulimpitia. **** Suzana aliposhituka usingizini hakuamini macho yake alipojikuta yupo nyumbani kwake amelala kitandani. Alirudia kutazama tena ni kweli au alikuwa akiota, akili yake ilimjulisha kuwa jana alipigiwa simu na mpenzi wake Brighton kuwa amepata dawa ya matatizo ya nguvu za kiume na alipokwenda kweli alikuwa amepona. Alikumbuka Brighton alimpa penzi tamu na kujikuta wote wakipitiwa usingizi, lakini ilikuwa ajabu kuamka asubuhi na kujikuta amelala kitandani kwake. Alijiuliza simu aliyopigiwa alikuwa anaota au kweli, kila alipolazimisha labda ni ndoto akili ilikataa na kuamini kabisa alikwenda kwa Brighton. Alijiuliza labda baada ya kufanya mapenzi alirudishwa nyumbani, lakini kwa upande wake kitu kama kile hakikuwahi kutokea. Kingine kilichomshangaza hata kama alirudishwa akiwa amelala hakuwa na fahamu. Alikaa kitandani kwa muda na kukumbuka anatakiwa kujiandaa kwenda kazini. Aliamka na kwenda kujiandaa, alipofika kazini bado akili yake haikumpa alimtafuta Sharifa amueleze kilichomtokea. Suzana na Brighton kilichowatokea watakigundua? Wakikigundua watachukua hatua gani? Balkis atatimiza dhamira yake?
@@@@@@@@@@@@@@@@@@@
Alipofika alimkuta ndiyo kwanza anafuta vumbi kwenye kompyuta yake, Sharifa alipomuona Suzana aligundua ana matatizo. “Karibu shoga.” “Asante,” alijibu huku akisogeza kiti na kuketi. “Mbona uko hivyo?” “Mmh! Kuna kitu kimenitokea jana sikielewi hata kidogo!” “Kitu gani hicho?” “Unakumbuka jana nilikupigia simu?” “Ndiyo.” “Nikakueleza kuwa nimeahirisha kwenda kwa mganga?” “Ndiyo.” “Basi, Brighton si aliniita na kunieleza kuwa amepata dawa ya tatizo lake na kukosa nguvu za kiume.” “Ehe?” “Baada ya kunieleza vile nikaona hakuna sababu yoyote ya kwenda kwa mganga kwa vile dawa imepatikana.” “Ehe!” “Basi jana saa moja usiku nikaenda kwa mpenzi wangu.” “Lete raha dada.” “Tumekutana kama kawaida, baada ya kuoga tulipanda kitandani, si unajua usongo niliokuwa nao.” “Najua sana.” “Basi shoga, kama alivyonieleza ndivyo ilivyokuwa, mtoto wa kike nikajilia raha nilizozipoteza muda mrefu.” “Alikuwa na nguvu kama kawaida?” “Tena ziliongezeka mara mbili.” “Mmh! Makubwa, kampata mganga gani huyo?” “Anasema alikwenda hospitali.” “Jamani ona sasa, kumbe tunakimbilia kwa waganga tiba ipo hospitali, nilikueleza toka awali waganga wengine wanatengeneza ugonjwa, ionekane kweli tuna matatizo makubwa ili tuwape fedha nyingi.” “Shoga bado nakuja sijafika kwenye pointi yangu.” “Ipi tena?” “Sababu iliyonifanya nisiingie ofisini kwangu na kuja moja kwa moja kwako.” “Una tatizo gani?” “Tulipomaliza kufurahishana na mpenzi wangu huku nikifurahia mafanikio makubwa baada ya kupona tatizo lake, tulipitiwa na usingizi mzito. Lakini kwa maajabu makubwa nimeamka asubuhi na kujikuta nipo kwangu!” “Kujikuta kwako kivipi?” “Kitandani kwangu nimelala!” “Sasa kipi cha ajabu?” “Ina maana hujanielewa?” “Nimekuelewa! Yaani jana baada ya kukutana na mpenzi wako asubuhi ulipoamka ulijikuta umelala, sasa kipi cha ajabu kama ulilala usiku na asubuhi ukajikuta kitandani?” “Hebu nielewe vizuri nisemayo, jana nilikwenda kwa Brighton kama ilivyo kawaida, ninapokwenda hulala huko huko, hata safari yangu ya kuja kazini huianzia kwake.” “Hilo nalijua, sasa hapo tatizo nini?” “Jamani huoni tatizo! Nilale kwa Brighton niamke kwenye kitanda nyumbani kwangu tena nikiwa peke yangu.” “Suzana! Unayosema ni kweli au ulikuwa unaota?” “Sharifa, yaani niote mchana na usiku? Sikukupigia simu?” “Ulinipigia?” “Saa ngapi?” “Mchana” “Sasa huko kuota gani?” “Mmh! Basi kama ni kweli usemayo kuna namna lazima tuliangalie kwa macho mawili.” “Yaani toka nimeamka sijielewi kabisa.” “Umempigia simu Brighton kumuuliza?” “Huwezi amini kila nikipiga simu yake inaonekana anazungumza.” “Basi kuna umuhimu wa wewe kwenda kwake ili ukapate ukweli, japo mimi bado naamini baada ya kunipigia simu inawezekana kabisa ulipitiwa na usingizi na kuota ulikuwa na Brighton na asubuhi ulipoamka ukajishangaa upo kitandani kwako. Lazima utaamini kabisa umetokewa na kitu kisicho cha kawaida.” “Sharifa hiki ninachokueleza ni kweli kabisa si cha kuota, haya ni maajabu.” “Au ndiyo Jini Balkis?” “Jini Balkis! Kama ni Balkis, Brighton asingeweza kufanya kazi.” “Nimekueleza yule jini ana mambo mengi ya kukuchanganya pale unapokaribia kuujua ukweli.” Suzana anaanza kuingia kwenye mtihani mzito wa Jini Balkis, nini hatima ya yote?“Kwa hiyo kuna umuhimu wa kwenda kwa mganga?” “Ikiwezekana, lakini kwanza nenda kwa mwenzako ili umuulize kama kweli jana mlilala pamoja.” “Mmh! Itabidi nifanye hivyo.” “Asubuhi hii?” “Sharifa siwezi kufanya kazi vizuri, akili yangu bado ipo njia panda ukweli wa kitu hiki nitaupata kwa Brighton.” “Kazi?” “Lazima niombe ruhusa, nimechanganyikiwa, sijui itakuwaje kama huyo jini atakuwa kanivaa na mimi?” “Kama kukuvaa kakuvaa muda mrefu, sasa inawezekana ndiyo anajionesha kwamba na wewe upo kwenye mtandao wake.” “Mungu wangu! Kama ni hivyo nitakuwa nimekwisha,” Suzana aliingiwa na hofu. “Suzana acha kujikatia tamaa, hebu tafuta ukweli ili tujue tufanye nini, ikiwezekana twende leo leo, nitaomba ruhusa nikusindikize.” “Basi wacha nikaombe ruhusa niende kwa Brighton nikapate ukweli, bila hivyo nitachanganyikiwa.” “Haya shoga utanijulisha,” Suzana aliagana na Sharifa na kwenda kuomba ruhusa kisha alielekea nyumbani kwa Brighton. *** Balkis akiwa amejilaza kitandani na Brighton, alimuona Suzana akielekea pale, kama kawaida yake alimueleza mpenzi wake: “Suzana anakuja.” “Umejuaje?” “Nijue vipi, la muhimu jiandae kumpokea mpenzi wako.” “Sasa nimpeleke chumba gani?” “Mlete humu humu.” “Wewe unatoka?” “Niende wapi?” “Si chumba wa wageni.” “Mi sitoki, Suzana anakuja kukuuliza kama jana alikuja kulala hapa.” “Umejuaje?” “Nisikilize kwanza ndipo uliniulize maswali.” “Mh!” “Naomba unisikilize, ukijichanganya shauri yako.” “Mbona unaniambia hivyo?” “Ndiyo maana nakueleza, nisikilize kwa makini.” “Sawa.” “Suzana anakuja kuulizia kama kweli jana alikuja hapa, mjibu kuwa hakuja. Tumeelewana?” “Lakini mbona mimi nafahamu jana alikuja?” “Kama alikuja mbona asubuhi hukumuona?” “Hata mimi nashangaa.” “Wewe na Suzana mliota ndoto ya aina moja kuwa jana mlikuwa pamoja lakini kila mmoja alipoamka hakumuona mwenzake.” “Balkis! Mbona unanitisha, wewe ni nani?” “Kwani wewe unanionaje?” “Nakuona mtu wa kawaida, lakini unayozungumza yananishangaza sana.” “Mbona ya kawaida, ni kipawa ambacho mwanadamu hupewa na Mungu kujua yajayo.” “Mmh! Nilikufikiria vibaya.” “Ulinifikiria vipi?” “Labda jini!” “Brighton tokea lini jini akazungumza na mwanadamu?” “Huwa nasikia majini huweza kujigeuza na kuwa wanadamu na kuishi nao.” “Kama ningekuwa jini ungefanyaje?” “Ningekufa kwa mshtuko.” Mara kilipita kimya cha ghafla, kitu kilichomshangaza Brighton. Haukupita muda mlango wa chumbani uligongwa. “Mkaribishe Suzana,” Balkis alimwambia Brighton aliyepatwa na mshtuko. “Wapi?” Ilikuwa ajabu Balkis alizungumza kwa sauti ya juu, lakini Brighton aliuliza kwa sauti ya kunong’ona. “Kuwa muelewa, nimekueleza mkaribishe humu ndani.” “Ili atufumanie?” “Ndiyo.” “Ili iweje?” “Utajua akiishaingia ndani.” Sauti ya kugonga mlango iliendelea nje huku ikionekana kabisa kitendo cha kuchelewa kufunguliwa mlango kilimuudhi sana Suzana. “Brighton kama hutaki nije kwako si uniambie kuliko kunifanyia visa?” “Mkaribishe,” Balkis alimueleza Brighton kwa kumkaripia. “Ingia,” alimkaribisha akiwa na wasiwasi
mkubwa. Suzana aliingia na kwenda kukaa kitandani, pembeni kabisa ya Balkis. Brighton alikuwa kama mtu aliyeshikwa na ganzi na kushindwa kuelewa kama mpenzi wake ameingia ndani. Suzana baada ya kuingia alimshangaa kwa mara nyingine. “Brighton upo sawa?” “Eeh.... aah.. Unasema?” Brighton alijikuta akibabaika kujibu. “Makubwa ina maana hujaniona naingia?” “Nimekuona.” “Hata kunikaribisha? Kweli mapenzi yamekwisha,” Suzana alizungumza kwa sauti ya kilio. “Suzana...,” Brighton alipotaka kusema alimtupia jicho Balkis aliyekuwa amejilaza pembeni ya Suzana huku akitabasamu. “Brighton, una nini mpenzi wangu?” “Si..si..sina,” majibu ya Brighton yalizidi kumshangaza Suzana. “Kuna nini humu ndani, mbona sikuelewi? Jana nilikuja ukawa katika hali hii hii na leo tena, kuna kitu gani mpenzi wangu! Kwa nini hutaki kuniambia?” “Brighton mkatalie kwamba jana hakuja hapa,” Balkis alimwambia kwa sauti aliyosikia Brighton peke yake. “Brighton mbona kama haupo na mimi! Una nini mpenzi wangu?” Suzana aliporomokwa na machozi na kumfuata Brighton alipokuwa amesimama kama kapigwa na shoti ya umeme. Alianza kumpapasa huku akiendelea kumuuliza jinsi alivyoonekana mtu aliyehama kimawazo. Je, nini kitaendelea? Brighton atamsikiliza nani kati ya Suzana na jini Balkis?
@@@@@@@@@@@@@
Brighton alikuwa kama yupo ndotoni akijiuliza yanayotokea mbele ya macho yake ni kweli au ni kiini macho. Chumbani kulikuwa na watu watatu, Balkis hakujificha zaidi ya kulala kitandani, tena peupe. Hata Suzana alipoingia, pamoja na kukaa pembeni yake hakuonesha kuona kitu cha tofauti mle ndani. Alizidi kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Balkis si kiumbe cha kawaida, hata sauti yake aliyompa maelezo bado ilionesha kuisikia peke yake. Kuhama kimawazo kulizidi kumnyima raha mpenzi wake ambaye naye alikuwa na yake yaliyotakiwa kupata majibu kutoka kwa Brighton. “Brighton jana nimekuja hapa na kulala na wewe, lakini ajabu nilipoamka asubuhi nimejikuta nipo kitandani kwangu. Ni kweli jana nilikuja au nilikuwa naota?” “Brighton, kataa! Sema hakuja?” Balkis alipaza sauti ya juu. Lakini Brighton alijikuta mdomo ukiwa mzito kumjibu mpenzi wake huku jasho la hofu likimtoka. “Brighton una nini mpenzi wangu, nijibu basi, si ni wewe ndiyo ulinipigia simu jana na kuniambia nije?” “Brighton kataaa,” Balkis alizidisha sauti iliyoumiza ngoma za sikio. “Brighton kuna nini hapo kitandani mbona unapaangalia sana, au kuna mwanamke?” “Ha..ha..kuna..ki..” “Brighton unafanya nini?” Balkis alipiga kelele iliyokuwa na mlio mkubwa kama radi iliyofanya ngoma za sikio za Brighton zisikie maumivu makali. “Brighton mpenzi wangu una nini au umeshavamiwa na jini Balkis?” “Nani?” Jina la Balkis lilimshtua. Kauli ile ilimuudhi jini Balkis, akapuliza upepo uliompata usoni Suzana ambaye aliishiwa nguvu na kupitiwa na usingizi mzito. Brighton alimuwahi kabla hajaanguka chini na kumlaza kitandani pembeni ya Balkis. “Suzana... Suzana,” alimwita kwa kumtikisa. Suzana hakujibu kitu, alionekana mwenye usingizi mzito. Brighton alimuona Balkis jinsi alivyompuliza hadi kupitiwa na usingizi mzito. “Balkis umemfanya nini Suzana?” “Acha upumbavu,” Balkis alimjibu kwa hasira. “Balkis mbona sikuelewi?” “Hunielewi kivipi?” “Itakuwaje umpulize mtu apoteze fahamu?” “Nilikwambia nini?” “Nilikwambia utoke, kwa nini hukutoka?” “Mimi ni nani yako?” “Kwa tabia yako ya miujiza siwezi kukuoa, unaonekana si mtu wa kawaida.” “Unasemaje?” Kauli ile ilimchefua Balkis. “Siwezi kukuoa.” “Kweli?” “Kweli,” Brighton alijibu kwa kujiamini. “Asante.” Baada ya kusema vile Brighton alishangaa kuona sura ya Balkis ikijikunja na kuwa kama mzee, uzuri wote ulipotea. Wasiwasi ilizidi kumjaa kwa kuamini huenda kweli Balkis si mwanadamu wa kawaida bali ni jini. Baada ya kugundua kuwa Balkis si kiumbe wa kawaida, aligeuka ili awahi kuchukua Biblia ili amkemee, hakupiga hata hatua moja, mkono wa Balkis alinyooka na kuwa mrefu, ukamrudisha alipokuwa, kisha alimshika sehemu za siri na kuzivuta kwa nguvu kama anatoa kitu. Brighton alihisi kama amepigwa shoti ya umeme sehemu za siri kisha alizisikia zikiwa za baridi kama zimetoka kwenye jokofu. Kwa sauti kali ya hasira Balkis alisema: “Hutasimamisha milele, na mkeo hatazaa milele.” Baada ya kusema vile aliingiza mkono sehemu za siri za Suzana ili amtoe kizazi, kabla hajamtoa Brighton alipiga kelele: “Hapana, Balkis usifanye hivyo.” “Lazima niwatie adabu, binadamu gani asiye na shukrani.” “Nisamehe Balkis nipo tayari kukuoa.” “Mpaka kwa shinikizo?” “Siyo hivyo, mambo yako yananichanganya nashindwa kukuelewa wewe ni mtu wa aina gani?” “Mimi ni jini?” “Eeh!” Brighton alishtuka. “Unashtuka nini, mimi ni jini la chini ya bahari.” “Mungu wangu nimekwisha miye.” ”Uishe kivipi, katika muda tuliokuwa wote uligundua tofauti gani kwangu?” “Sijagundua.” “Penzi langu na wanadamu wenzio lipi lilikuwa tamu?” “La kwako.” “Mimi na mchumba wako nani mzuri?” “Wewe.” “Nani aliyesema kwamba Suzana hafai kuolewa?” “Mimi.” “Nilijitoa kwako ili kurudisha furaha iliyopotea, pamoja na kukubali kunioa bado nilimheshimu mpenzi wako, kosa langu nini?” “Nisamehe.” “Nitakusamehe, lakini nakurudishia ugonjwa wako ambao hautapona milele.” “Nisamehe Balkis nilikuwa sijajua.” “Hujajua nini?” “Hata sijui nilimaanisha nini nimechanganyikiwa Balkis, nisamehe sana.” “Mimi nakusamehe, lakini nakuacha na matatizo yako na mpenzi wako.” “Hapana usinifanye hivyo.” “Kumbuka nilikuponya ili nipate raha zako na si kwa faida ya mtu mwingine, nikiondoka naondoka na raha zangu.” Balkis atamsamehe Brighton?
“Nimekubali kuendelea kuwa na wewe Balkis usinifanye hivyo,” Brighton alijitetea kwa kupiga magoti mbele ya Balkis. “Kwa nini hutaki kunisikiliza?” “Nilichanganyikiwa baada ya kukuona ndani, nilijua lazima Suzana atakuona.” “Nilikueleza mimi ni nani?” “Jini.” “Jini huonekana kwa kupenda, Suzana asingeniona hata mara moja.” “Ningejuaje bila kuniambia?” “Kweli kosa ni langu la kutokukueleza mapema, nitakurudishia nguvu zako na leo hii nitaondoka na wewe kwenda kwetu kuishi maisha mazuri.” “Wapi?” “Ujinini,” Balkis alizungumza kwa sauti ya upole huku akijirudisha katika hali yake ya uzuri wa shani. “Na Suzana?” “Mwache tu, sitamdhuru, nitamrudisha kwake akiamka atajikuta kitandani amelala.” Baada ya kusema vile alimkumbatia Brighton na wote walitoweka mle ndani na kutokea pembeni ya bahari maeneo ya Daraja la Salenda. “Unanipeleka wapi?” “Brighton mpenzi acha woga, tunakwenda kwetu chini ya bahari.” “Si nitakufa na maji?” “Huwezi, ni sehemu nzuri sana ukifika hutakumbuka kurudi duniani.” “Nitaishi vipi na majini na mimi ni mwanadamu?” “Kama nilivyokueleza majini tupo kama wanadamu wa kawaida na kufanya mambo kama ninyi.” “Mmh! Sawa.” Walitembea taratibu kuelekea ndani ya maji, Brighton alikuwa na wasiwasi wa kuzama, wasiwasi wake labda Balkis anataka kumzamisha na kumuua baada ya kuonesha kiburi. “Balkis usiniue,” alijitetea. Balkis badala ya kumjibu alicheka sana, jambo lililozidi kumtisha Brighton, hakusimama aliendelea kusogea mbele katikati ya bahari akiwa bado amemshika mkono. Maji yalimfika magotini, tumboni yakaanza kuelekea kifuani mwishowe yakavuka mabega. “Balkis naomba unisamehe usiniue kwenye maji.” “Brighton hakuna mtu anaweza kuitupa shuka yake wakati wa baridi.” “Una maana gani?” “Wewe ndiye shuka langu, siwezi kukupoteza, bora nipotee mimi.” Wakati huo maji yalikuwa yamewafika chini ya kidevu, Balkis alimshika Brighton kichwani na kumzamisha ndani ya maji kwa nguvu, alitaka kupiga mayowe lakini alikuwa amechelewa. Aliposhtuka alijikuta wametokea kwenye mji mzuri ajabu. “Brighton, karibu sana huu ni mji wetu, nawe utaishi kama mfalme, mimi ni mtoto wa Mfalme wa Majini. Baba yangu anaitwa Bashami Hudirud.” “Asante.” Walikuja vibaraka weusi kama wanadamu wa kawaida lakini miili yao ilikuwa na nguvu sana. Juu walikuwa vifua wazi na chini walikuwa wamejifunga shuka kama nepi wakiwa wameongozana na vijakazi waliojifunga shuka nyeupe na kuiacha migongo yao nje
wakiwa wamebeba maua na farasi weupe wawili waliokuwa wametandikwa matandiko ya dhahabu. Vibaraka wenye nguvu walimbeba Brighton na kumketisha juu ya farasi, baada ya kukaa walimbeba Balkis na kumketisha kwenye farasi mwingine aliyekuwa mzuri kuliko aliyembeba Brighton. Baada ya wote kukaa kwenye farasi, safari ilianza kuelekea kwenye jumba la kifahari. Brighton alipatwa na wasiwasi kukuta mji unaosemwa ni wa majini ni mzuri ajabu na viumbe wake ni watu wa kawaida kama wa duniani. Ila njia nzima hakuna gari wala chombo chochote kinachotumia moto. Alikaribishwa ndani huku akipigiwa muziki wa vyombo vitupu lakini ulikuwa mtamu masikioni. Kabla ya kuingia ndani lilitandikwa zulia jekundu ambalo hakuwahi kuwaza kulikanyaga katika maisha yake. Baada ya kuingia ndani alikaribishwa na wasichana wazuri waliovalia magauni meupe yaliyowapendeza, walimwaga maua ya kunukia. “Brighton karibu kwetu,” Balkis alimkaribisha Brighton kwenye sofa lililotengenezwa kwa manyoya ya kondoo. “Asante,” alijibu huku akikaa kwenye sofa lililomfanya ahisi usingizi. “Jisikie upo nyumbani.” “Asante, mbona ni tofauti na nilivyofikiria?” “Kuhusu nini?” “Nilijua ninyi ni viumbe wa ajabu wenye mikia na meno ya kutisha, mbona ni binadamu kama sisi, kwa nini mnaitwa majini?” “Majini ni viumbe wenye uwezo mkubwa wa kufanya jambo lolote tofauti na wanadamu. Lakini nasi tunamuabudu Mungu kama ninyi.” “Mbona mnaua watu?” “Unatushangaa kwani hakuna wanadamu wanaoua wenzao?” “Wapo.” “ Mbona mnatushangaa sisi?” “Lakini nasikia majini hutumika kuwaua watu?” “Bado hakuna kitu tofauti na wanadamu, kuna wanadamu wachawi mbona hao hamuwazungumzii.” “Lakini mbona nasikia kuna majini kazi yao ni kuua tu sijui Jini Makata.” “Brighton hakuna wanadamu wanaotumwa kuua, hakuna majambazi wanaoua na kuchukua mali zao? Duniani sasa hivi kuna vita, wanadamu wanauana mamia kwa mamia bila sababu, hapo napo kuna majini?” Swali lile lilimfanya Brighton akose jibu, Balkis aliendelea kuzungumza. Je, nini kitaendelea?.
ITAENDELEA........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni