WAKILI WA MOYO SEHEMU YA 16



WAKILI WA MOYO

SEHEMU: 16

MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’

ILIPOISHIA:
“Hakuna tatizo.”
Hans aligeuza gari na kuelekea Masaki, muda wote Mage alikuwa amejilaza kwenye siti baada ya kuilaza kwa nyuma. Hans alisimamisha gari kwenye maegesho ya Sea Cliff hoteli.
SASA ENDELEA...

“Bebi tumefika,” alimshtua Mage aliyekuwa amefumba macho.
“Kachukua chumba kabisa,” Mage alijibu bila kufumbua macho.
“Sawa.”
Hans aliteremka na kwenda kulipia chumba kisha alirudi kumweleza Mage.
“Tayari.”
Aliteremka na kufunga gari lao kisha waliongozana hadi ndani ya chumba walichokikodi. Mage alipofika alijilaza kitandani macho alitazama juu mikono alilalia kwa nyuma. Pembeni ya macho yake michirizi ya machozi iliendelea kuteremka na kulowesha shuka.
“Vipi bebi?” Hans alizidi alishtuka.
“Hans sijui nikueleze nini uelewe najua jamii itanitenga kwa ajili ya uamuzi wangu wa kuvunja uchumba, wapo watakao niona sina akili lakini anayejua mapenzi ataniunga mkono. Nimekubali kubeba lawama zote za wanadamu lakini niufurahishe moyo wako. Sijui nitakaporudi nyumbani mama atanipokeaje naweza kutengwa na familia kwa uamuzi wangu huu.”
“Kwani huyo jamaa umeisha mwambia ukweli?”
“Siku tatu zilizokuwa naye Bagamoyo nilizitenga mahususi kwa ajili ya kumweleza taratibu kuuvunja uchumba wetu rasmi. Ningeweza kumwambia tu, lakini naheshimu mapenzi yake kwangu.”
“Amepokeaje?”
“Ilikuwa kazi kwelikweli jamaa alichachamaa mpaka kutishia kutoa mtu roho, siyo siri alikuwa amekufa kaoza nina wasiwasi akawa mwendawazimu au kuchukua uamuzi wa kujinyonga.”
“Mi nafikiri mshale umerudi porini haujapotea, Mage nakuapia kwa Mungu kutoujutia uamuzi wako. Kama ulivyojitoa kwangu nami nitazishia mapenzi mara mia ya mwanzo. Nina amani ulikubali kuolewa kwa shinikizo, lakini moyo wako bado ulikuwa kwangu nami unaamini hivyo.
“Hii ni nafasi nyingine ya kuidhihilishia dunia kuwa mimi na wewe tulizaliwa ili tuwe mwili mmoja. Mage nashukuru kuuponya moyo wangu uliokuwa na maumivu ya muda mrefu kulishwa nisicho kitaka, lakini kwa sasa nakula ninachokitaka.”
“Hans naamini unanipenda zaidi ya kunipenda ndiyo sababu ya mimi kukubali kurudi kwako, wasiwasi wangu mkubwa ni familia yako. Hans nitakufa na mtu kila atakayetia mkono katika penzi letu sijali ni nani,” Mage alitoa mkwala mzito.
“Mage nitalipigania penzi letu nakuahidi hakuna atakayeingilia penzi letu, nakuahidi mapenzi ya peponi. Nitayafuta machozi yako kwa kitambaa cha upendo,” Hans alisema huku akimfuta machozi kwa kiganja cha mkono.
“Hans nimejilipua ukinitenda umenimaliza,” Mage alisema kwa sauti ya kilio huku akijitupia kifuani kwa Hans.
“Nakuhakikishi na harusi yetu haitachukua muda mrefu.”
“Kweli Hans?” alimuuliza huku akiyatoa macho yake yaliyojaa machozi kumtazama Hans.
“Toka uliponitamkia matumaini ya kurudi kwangu nilikwenda mbali zaidi ya maandalizi ya ndoa yetu. Nilikuwa nasubiri kauli yako ili nikueleze hili.”
“Wazazi wako je?”
“Niliwaeleza wakasema hawawezi kunichagulia tena.”
“Huoni kama ule wasiwasi wao juu ya kifo cha mkeo utazidi na mimi kuonekana ndiye muhusika?” Mage aliingiwa wasiwasi.
“Nilijua hilo litatokea lakini nimewaeleza mimi ndiye niliyekufuata japokuwa wewe haukuwa tayari kurudiana na mimi hasa baada ya kukutosa kukuoa pia familia yangu kukuingiza kwenye matatizo. Nashukuru walinielewa.”
“Mmh! Sawa, kwako umemaliza sijui kwangu mama atapokeaje.”
“Atakuelewa kwa vile anajua penzi letu lilivyokuwa naamini moyo wake utafurahi kumpata mkwe sahihi.”
“Mmh! Tutaona.”
Walikwenda kuoga kisha walipata vinywaji na kufurahisha nafsi zao walipanga kuondoka pale saa sita usiku.
****
Muda ulizidi kukatika bila Mage kuonekana kitu kilichozidi kumtia wasiwasi mama yake na kujiuliza atakuwa amepitia wapi. Mawazo yake yalimpeleka labda yupo kwa shoga yake Brenda. Lakini aliamini kama aliondoka nyumbani siku tatu zilizopita alitakiwa afike nyumbani kwanza ndipo aende kwa shoga yake.
Alipiga simu ya Mage haikuwa hewani kitu kilichofanya azidi kuingiwa wasiwasi, aliamua kumpigia simu Brenda. Simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa na kushindwa kuelewa kuna nini ikiwa simu ya Mage haipatikani na simu ya shoga yake haipokelewi.
Akiwa katika ya mawazo simu iliita aliichukua haraka na kupokea ilikuwa inatoka kwa Brenda.
“Haloo mama.”
“Brenda, kwema?’
“Kwema mama, samahani simu ilikuwa mbali kidogo nimekuta umepiga, unasemaje mama?”
“Mage amefika huko?”
“Sijamuona, kwani amerudi?”
“Nasikia amerudi toka saa kumi na moja lakini mpaka sasa sijamuona na simu yake haipatikani.”
“Umemuulizia shemeji Colin si ndiye aliyekuwa naye?”
“Mmh! Ipo kazi.”
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Basi ngoja nimpigie Colin alinieleze Mage kaenda wapi.”
“Itakuwa vizuri.”
Baada ya kukata simu, alimpigia Colin nayo haikuwa hewani kitu kilichozidi kumweka njia panda asijue nini kinaendelea aliamua kumpigia mama Colin simu iliyopokelewa.
“Haloo shoga kuna habari gani maana mimi mwenyewe moyo hauna raha, toka Colin kafika kajifungua ndani kuna habari gani huko?” mama Colin alipokea na kuanza kumwaga maneno.
“Dada mbona umezungumza mengi, huku mpaka muda huu Mage sijamuona wala simu yake haipatikani. Nimemuulizia kwa shoga yake hajafika, simu ya Colin haipatikani kuna nini katikati mbona sielewi, Colin yupo?”
“Ndiyo.”
“Naomba kuzungumza naye.”
“Sawa.”
Mama Colin alimpelekea simu Colin aliyekuwa amejilaza akitafakari kilichotokea. Mpaka muda ule alikuwa akiona kama ndoto yenye ukweli. Alijiuliza maandalizi yote na matangazo ya sherehe ya kukata na shoka atafanya nini atawaeleza nini jamaa zake aliojitolea kusimamia sherehe ya harusi yao kwa gharama zao.
Rafiki zake wa nje ya nchi aliosoma nao Ulaya nao alijiuliza atawaambia nini ikiwa tayari walikuwa wameshona suti kwa ajili ya sherehe ile na walikuwa tayari kuja nchini ikiwa pamoja na kukodi vyumba kwenye hoteli za nyota tano na malipo yalikuwa tayari.
Kila alivyofikiria alikosa jibu, alitamani hata kumshawishi Mage akubali amuoe hata kwa mkataba wa mwezi mmoja ili jamaa zake wakiondoka waachane lakini wakiwa wamedhudhulia sherehe yake iliyopangwa kutekekeza mamilioni ya fedha. Pamoja na kuujua msimamo wa Mage bado aliamini kupitia wazazi wao anaweza kukubaliana nao.
Lakini wazo la kuendelea kumbembeleza aliona kama kujidhalilisha, alikumbuka kitu. Alinyanyuka kitandani na kwenda kwenye kabati, kabla hajashika mlango uligongwa alipaza sauti ukuuliza.
“Nani?”
“Mimi,” ilikuwa sauti ya mama yake.
“Naam mama, unasemaje?”
”Hebu fungua mlango.”
Alirudi hadi mlangoni na kufungua mlango, alionekana amechoka sana kitu kilichozidi kumuumiza mama yake.
“Mama Mage anataka kuzungumza na wewe.”
“Kuhusu nini?”
“Inasemekana toka ulipoachana naye hajarudi nyumbani na simu yake haipatikani, Colin mwanangu usiwe umemuacha wewe mtoto wa watu akaenda kujinyonga?”
“Mama mimi na wewe tunataniana hasa katika jambo zito kama hili? Inaonekana tukiwa ndani ya uchumba Mage alikuwa na mpenzi wake. Ni wazi lilikuwa shinikizo toka kwa mama yake ili nimuoe lakini ukweli umejidhihili maji hayachanganyikani na mafuta.”
“Hebu kwanza zungumza na mama Mage.”
“Mama nitaongea naye nini?”
“Ulichonieleza.”
Colin alichukua simu ya mama yake ambayo ilikuwa wakati huo imekata na kupiga, baada ya muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo dada.”
“Hapana ni mimi Colin.”
“Ooh! Baba za siku mbili?”
“Nzuri, shikamoo.”
“Marahaba.”
“Naam mama.”
“Eti baba, mwenzio yupo wapi?”
“Sijui,” alijibu kwa mkato.
“Kwa nini unasema hujui wakati mlikuwa wote siku tatu.”
“Mama, nimeachana na Mage baada ya kunifukuza ndani ya gari lake kama mbwa.”
“Wee! Kwa sababu gani?” mama Mage alishtuka.
“Ana mtu ambaye ndiye aliyemuingiza dunia ya mapenzi na kwa kunitamkia kuwa amevunja uchumba wetu. Kumbembeleza kwangu kumekuwa kero kwake na kuamua kuniteremsha njiani kisha kunitupia mzigo wangu huku akinitolea maneno ya dharau kuwa yupo mwanaume wa ndoto yake.”
“Yupo wapi baba, yule mwanaume alimtenda.”
“Basi ameamua kurudi huko.”
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Si kwa mpenzi wake,”Colin alijibu kwa kifupi.
“Lakini baba linazungumzika, mimi ndiye mzazi wake.”
“Ni kweli wewe ndiye mzazi wake lakini moyo wa uamuzi ampende nani unabakia kwa Mage.”
“Basi baba, niachie kazi hiyo.”
“Wala usisumbuke mwachie uamuzi wake, mapenzi hayalazimishwi japo kaniweka katika wakati mgumu maishani mwangu.”
“Baba…baba..naomba usifike huko nimekueleza niachie mimi naomba kuzungumza na mama yako.”
Colin alimpa simu mama yake aliyekuwa amesimama pembeni yake akiwa amepigwa na bumbuwazi kutokana na kauli za mwanaye.
“Haloo dada.”
“Dada kwanza nisamehe sana kama kweli asemayo Colin ni kweli, yaani nilidhania utani kumbe kweli. Dada naomba uniachie suala hilo.”
“Sawa, nikutakie usiku mwema.”
***
Majira ya saa sita usiku Mage aliingia ndani ya sebule ya nyumbani kwao, alishangaa kumkuta mama yake yupo kwenye sofa akiwa amepitiwa usingizi. Alimsogelea na kumbusu shavuni kitu kilichomfanya mama yake ashtuke. Mbele yake alikuwa amesimama mwanaye Mage.
Kabla ya kusema lolote aliangalia saa kubwa ya ukutani iliyomuonesha ni saa saba kasoro usiku. Hakuiamini aliangalia ya mkononi iliyokuwa sawa na ya ukutani, alimwangalia mwanaye kuanzia juu mpaka chini kama ndiyo siku yake ya kwanza kumuona kitu kilichomshtua Mage.
“Vipi mama?”
“Unatoka wapi?” mama yake alimuuliza kwa sauti kali huku akinyanyuka kwenye kochi.
“Kwani vipi?” Mage alijifanya kushangaa.
“Nijibu unatoka wapi muda huu?”
“Niliporudi nilipita kwa shoga yangu.”
“Nani?’
“Debora, humjui.”
“Kufanya nini?”
“Mama mbona maswali mengi?”
“Kwa nini unanitia aibu, Colin umemfanya nini?”
“Kama alivyokuambia kwa vile alichokueleza niliisha kueleza muda mrefu si kigeni kwako.”
“Kwa hiyo umerudiana na Hans?”
“Ndiyo mama ndiye chaguo la moyo wangu.”
“Wewe si ulikuwa unasema humpendi tena na mapenzi yako yote kwa Colin?”
“Mama ningempenda Colin kama Hans asingekuwepo, kama matatizo yangemtokea nimo ndani ya ndoa nisingeweza kutoka. Lakini amerudi kabla ya ndoa sina budi kumpokea, mama Hans nampenda zaidi ya kupenda nipo tayari kunioa bila mahari.”
“Mage mwanangu nitaweka wapi sura yangu?”
“Ukiwaogopa walimwengu huwezi kufanya jambo la kimaendeleo, watasema mwanzo lakini watanyamaza na kusahau.”
“Mage mwanangu naomba ukalale ili kesho tuzungumze vizuri.”
“Sawa mama.”
Mage alikwenda kulala na kumuacha mama yake akiwa bado yupo sebuleni.
***
Mama Colin usiku ulikuwa mkubwa kwake kila alivyojitahidi kulala usingizi ulikataa, aliamini kabisa Mage hana tatizo bali mwanaye ndiye aliyevunja uchumba na kusingizia Mage ana mwanaume mwingine anayempenda. Akili yake ilimpeleka kwa Cecy tu msichana aliyemuona ndiye tatizo kwa vile tokea awali aliona dalili mbaya.
Alipanga kesho asubuhi kwenda kwa kina Mage ili aweze kuzungumza naye na akimwambia Colin ndiye aliyevunja uchumba basi bleki yake ya kwanza kwa Cecy na kukitia moto kibanda chao na kumfanyia kitu kibaya ambacho hata kisahau mpaka kufa kwake.
Asubuhi alikuwa wa kwanza kufika mbele ya nyumba ya kina Mage na kipiga honi mbele ya geti. Baada ya kufunguliwa geti aliliingiza gari ndani na kwenda kupaki kwenye maegesho. Aliteremka na kuelekea ndani ambako ilionesha bado wamelala baada ya kumkuta msichana wa kazi akifanya usafi, alipomuona alimkaribisha:
“Karibu mama.”
“Asante, mama yupo wapi?”
“Bado yupo chumbani kwake.”
“Kamwite.”
Msichana wa kazi alikwenda kumuamsha mama Mage, baada ya muda alitokea na kushtuka kumuona mzazi mwenzie asubuhi ile.
“Karibu dada.”
“Asante, mmeamkaje?”
“Mmh! Tunamshukuru Mungu.”
“Mage yupo?”
“Yupo chumbani kwake.”
“Ndiye kanileta asubuhi yote hii.”
“Ngoja nikamwamshe.”
“Sawa.”
Mama Mage alikwenda chumbani kwa mwanaye na kumuamsha.
“Vipi mama mbona asubuhi sana?”
“Mama Colin anataka kuzungumza na wewe.”
“Ha! Mbona asubuhi sana?” Mage alishtuka.
“Kwani uliyofanya madogo?”
“Mmh! Haya twende nikamuone.”
Walitoka pamoja hadi sebuleni alipokuwa amekaa mama Colin.
“Shikamoo mama,” Mage alimsalimia mama Colin.
“Marahaba mwanangu, samahani kwa kukurupusha asubuhi.”
“Bila samahani mama.”
“Naomba tuzungumze kidogo.”
“Hakuna tatizo.”
“Na mimi niwepo?” mama Mage aliuliza.
“Kwanza naomba tuzungumze wawili kisha tutazungumza wote.”
Mama Mage aliondoka na kuwaacha mtu na mkwewe, baada ya kubaki wawili mama Colin alimuuliza Mage.
“Mage mwanangu, kuna tatizo gani kati yako na mwenzako?”
“Hakuna tatizo lolote.”
“Mbona anasema kuwa eti wewe umevunja ndoa yenu, ni kweli?”
“Ni kweli.”
“Kama ni hivyo sasa mbona unasema hakuna tatizo?”
“Ndiyo mama hakuna tatizo, ila ni kweli alichokisema Colin.”
“Wewe na yeye nani kavunja uchumba wenu?”
“Mimi.”
“Kwa nini?”
“Mama kabla ya kuwa na Colin nilikuwa na mchumba wangu ambaye kipindi hicho akuwa ameoa. Lakini kabla ya ndoa, alipata matatizo ya kufiwa na mkewe na kurudi kwangu. Kwa vile ndiye aliyekuwa chaguo la moyo wangu aliporudi kuniomba niwe naye wala sikuhitaji ushauri nilimkubalia na ndiye nategemea ufunga naye ndoa na si Colin,” Mage alisema kwa kujiamini.
“Mage, hebu kuwa mkweli naomba usinifiche, Colin amekufanya nini kilichopelekea kuchukua uamuzi huo?”
“Kwa haki ya Mungu hajanifanya lolote baya.”
“Hujamfumania na mwanamke?”
“Walaa.”
“Kwa nini unavunja ndoa yako? Mage nakuahidi kukupa chochote ukitakacho ili tu ukubali kufunga ndoa na Colin.”
“Mama naomba kuwa mkweli wa moyo wangu, japokuwa bado mdogo mapenzi nayajua kwa vile yalinijeruhi. Ningeweza kuolewa na Colin jina lakini mapenzi yangu yangekuwa kwa Hans. Lakini siwezi kufanya kitu kama hicho sitaki kumtesa Colin bila sababu.”
“Hans ndiye nani?”
“Mwanaume wa ndoto yangu.”
“Mmh! Nimekuelewa, basi Mage naomba ubadili uamuzi ili uolewe na Colin.”
“Siwezi kuulazimisha moyo wangu, najua nawavunjia heshima, lakini nayaogopa maumivu ya moyo, niliumia sana wakati Hans ameoa. Kurudi kwake kwangu ni kutibu majeraha ya moyo wangu siwezi…siwezi kubadilika kwa vile nampenda sana Hans,” Mage alisema kwa sauti ya hisia kali.
“Mmh!” mama Colin alishusha pumzi ndefu na kusema:
“Nimekuelewa.”
“Una la ziada?” Mage alimuuliza.
“Mpaka hapo sina, nikuache upumzike.”

ITAENDELEA..........




TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU 🔞 SEHEMU YA 11

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5

CHOMBEZO: MASSAGE ROOM🔞 SEHEMU YA 21