VITA YA WACHAWI SEHEMU YA 7



VITA YA WACHAWI 07

MTUNZI ALLY MBETU

“Mchumba niliyetaka kumuoa kachukuliwa na mamba katika mazingira ya kutatanisha,” alimweleza mengine japo mwanzo hakumwambia.
“Mungu wangu pole sana,” Atuganile alijifanya kushtuka.
“Si bure lazima kuna mkono wa mtu.”
“Lakini mpenzi usisikitike sana mimi mpenzi wako wa damu si nipo?”
“Sawa, lakini huoni kama wanaweza kutufikiria vibaya labda tumepanga kumpoteza ili tuendelee kuwa pamoja. Japo tuko pamoja lazima kipindi hicho uhusiano wetu usiwe wa wazi sana kuonana kwetu iwe usiku tu.”
“Sawa, lakini sikubali utafutiwe mwanamke mwingine kama amepotea au amekufa nasubiri ndoa yangu.”
“Hakuna tatizo, kama hivyo sitakubali kuchaguliwa tena mwanamke,” Ambakisye alimuhakikishia mpenzi wake.
“Nimefurahi kusikia hivyo, basi naomba utumie hii dawa ili tujue tatizo nini.”
“Mmh! Sawa, lakini lazima nizungumze na baba ili nijue ataniambiaje.”
“Amba kwa nini usitumie tu ili tujue kitakuwa nini kuliko kuwapa presha wazazi wako?”
“Hapana lazima nimwambie baba kwa vile ni mtu wangu wa karibu ili nijue atanisaidia vipi kabla ya kutumia dawa.”
“Bibi Tumwambilile tatizo lako aliliona na kusema ukitumia dawa hii ndani ya siku tatu kila kitu kitaenda vizuri.”
“Sawa, lakini hili ni jambo zito kwa vile toka nizaliwe halijawahi kunitokea, jana nilijua ni uchovu wa safari lakini leo imenijulisha kuwa hili ni tatizo.”
“Kwa hiyo dawa hii niirudishe?”
“Hapana, niachie ila lazima nimwambie kwanza baba nisije sema hali imekuwa mbaya.”
“Mmh! Sawa.”
“Atu kuna kitu gani kati yetu?”
“Kipi?”
“Kwa nini matatizo yametutokea kwa siku moja, huoni hapo kuna mchezo fulani tuliochezewa?”
“Mmh! Kweli kabisa mpenzi wangu siku uliposhindwa kufanya kazi usiku wake ndipo niliharibu ujauzito wangu.”
“Unafikiri ni kwa amri ya Mungu?”
“Hapana lazima kuna mkono wa mtu.”

“Hujamuuliza bibi Tumwambilile tatizo lako linatokana na nini?”
“Aliniambia nikifukua sana uchafu nitakutana na uvundo na chanzo cha moto mkubwa ni cheche.”
“Alimaanisha nini?”
“Nilimuuliza, aliniambia kwa vile nimepona haina haja ya kuchimba sana.”
“Na mimi?”
“Kaniambia utumie dawa hii utapona kabisa.”
“Sasa fanya hivi nitakupitia kwenu ili twende tukamchimbe bibi Tumwambilile, nina senti kidogo najua atakubali kutueleza.”
“Sawa, basi mi nitakusubiri, muda mzuri jioni nitakuwa nimemaliza kazi.”

“Poa.”
Walikubalia amweleze baba yake ili wajue atamsaidia vipi pia ampitie jioni waende kwa bibi Tumwambilile wakajue matatizo yao yanatokana na nini. Kwa vile Atuganile hakutaka wazazi wa mpenzi wake wamuone alitokea dirishani na kwenda kumsubiri Ambakisye kwa mbele.
Baadaye Ambakisye alitoka na kumfuata njiani na kumsindikiza lakini mama ya Ambakisye aliwaona kwa mbali wakisindikizana na kumwambia mumewe.
“Baba Amba.”
“Unasemaje?”
“Umemuona mwanao kumbe alikuwa na mwanamke wake.”
“Kapitia wapi?”
“Hata najua.”
“Umewaona wapi?”
“Si walee,” alimuonesha Ambakisye aliyekuwa akimsindikiza mpenzi wake kwa mbali.
“Mmh! Kazi ipo ndiyo maana hakushtuka sana tulipompa taarifa ya kupotea kwa mpenzi wake.”
“Nina wasiwasi hata mwanetu anahusika na mpango huu, yaani hakutoa hata chozi ndiyo kwanza yupo na mpenzi wake.”
“Kule kuonesha ameumizwa na tukio lile na kufikia hatua ya kutaka kupambana, kumbe muongo mkubwa.”
“Kama ni hivyo basi vita yetu itakuwa ngumu.”
“Wee fuatilia kwa mtu wako ili tujue tatizo lipo wapi?”
“Lazima nifanye hivyo.”
“Kabla ya kulipua hakikisha Amba hahusiki tusijelia mikono kichwani.”
“Lazima nifanye hivyo.”
Wakati huo Ambakisye alikuwa akirudi kutoka kumsindikiza mpenzi wake. Alipofika karibu, wazazi wake walibadilisha mada ili asijue walikuwa wakizungumza nini.
“Baba,” Ambakisye alimwita baba yake.
“Unasemaje?”
“Samahani njoo chumbani kwangu mara moja.”
Baba yake bila kusema kitu alinyanyuka na kumfuata mwanaye chumbani, walipoingia Ambakisye alimueleza baba yake tatizo lililojitokea jana usiku na muda mfupi. Baba yake alishtuka kidogo na kumuuliza:
“Hali kama hii imewahi kutokea mara ngapi?”
“Ndiyo mara ya kwanza kibaya hata sehemu za siri zinasinyaa.”
“Eti?” baba yake alishtuka.
“Ndiyo baba hali hii imenitisha, kitu cha ajabu imejitokeza kwa wakati mmoja usiku wa jana ilianza kwangu kisha mwenzangu kutoka ujauzito kitu ambacho kinanitisha.”
“Inawezekana kabisa familia ya mpenzi wako inahusika.”
“Baba hebu kwanza angalia tatizo langu mbona mnapenda kuwashutumu kila kitu?” Ambakisye alisema kwa jazba kidogo.
“Hebu teremsha nguo zako nione.”
Ambakisye aliteremsha kaptura aliyokuwa amevaa na nguo ya ndani na kumuonesha baba yake ambaye alishtuka kuona mambo yapo vile.
“He! Hili ni tatizo.”
“Vaa twende mtoni.”

Ambakisye alivaa nguo zake na kwenda mtoni ambako watu walikuwa wakitumia kuoga. Kauli ya baba yake ilimfanya kujiuliza amegundua nini mpaka kumweleza waende mtoni, hakujua wanakwenda kufanya nini. Njiani mzee Amangise alichuma majani na kuendelea na safari yao.
Walipofika mtoni walitafuta sehemu iliyokuwa imejificha, baada ya kufika sehemu hiyo ambayo ilikuwa na miti mingi, alimwambia mwanaye atoe nguo zote kama anataka kuoga.
Ambakisye alifanya kama alivyoelezwa na baba yake, alitoa nguo zote na kusubiri kuona baba yake anataka kufanya nini.
Mzee Amangise alichukua majani mabichi aliyochuma njiani na kuyafikicha kisha aliyazungusha sehemu za siri za mwanaye na kumwambia aingie ndani ya maji.
Baada ya kuingia ndani ya maji, baba yake aliangalia sehemu za siri za mwanaye. Hali aliyoiona ilimshtua sana na kumuuliza mwanaye akiwa bado yumo ndani ya maji.
“Amba hali hii imekuanza lini?”
“Baba si nimekuambia jana usiku.”
“Hapana ugonjwa huu huwa wa kuzaliwa si wa kuugua ukubwani kama ungeugua ukubwani kwa dawa niliyokufunga ingeonesha ni tatizo la kutibika, lakini kwa hali hii inaonesha kabisa hata tufanye nini huwezi kupona.”
“Baba kwani naumwa ugonjwa gani?”Ambakisye alishtuka.
“Ugonjwa wa kukosa nguvu za kiume wa kuzaliwa.”
“Hapana baba, siwezi kuugua ugonjwa huo kwa vile ni jana usiku tu wala sina muda mrefu.”
“Hebu toka ndani ya maji.”
Ambakisye alitoka ndani ya maji na kuvaa nguo zake, alijikuta akikosa raha kwa maneno ya baba yake. Ilibidi apate ukweli wa tatizo lake kwa kumuuliza baba yake.
“Baba una maanisha ugonjwa huu hauponi?”
“Watu wanaokuwa hivyo huwa hawaponi, huu ni wa kuzaliwa nao kwako nashangaa kusema ni jana na kuwa katika hali hii. Mmh! Nimeishajua, naona sasa wananichezea baada ya kumchukua kichawi mchumba wako sasa wamekugeukia mwenyewe.”
“Kina nani?”
“Kwani waliondoka siku ya kikao wakisema tutawaona wao kina nani?”
“Una maanisha familia ya kina Atu?”
“Ndiyo, walisema watakukomoa naona wametimiza azma yao.”
“Huenda basi nao wamelipa kisasi cha Atuganile kutolewa ujauzito.”
“Wala hiyo siyo sababu hebu tupitie kwa Mwakasanga tukaangalie tatizo nini.”
Walikubaliana kupitia kwa Mwakasanga mtaalamu wa tiba za jadi, walipofika waliingia ndani ili wamweleze tatizo lao.
“Karibuni, naona leo baba na mwanaye mmenitembelea?”
“Ndiyo ndugu yangu.”
“Mbona nyuso zenu zinaonesha kuna tatizo?”“Ni kweli.”

Baada ya kusema vile Mwakasanga aliangalia juu akiwa ameshika mkono kidevuni kwa muda na kucheka kidogo kisha aliuliza:
"Mmh! Mlikuwa mnasemaje?"
"Nina imani umeona kila kitu."
"Ndiyo, mlikuwa mnatakaje?"
"Umsaidie mwanangu pia kumjua aliyefanya hivi."
"Waswahili wana usemi wao kuwa moto mkubwa ulianza cheche."
"Unamaanisha nini?"
"Unajua vizuri kwa hiyo vita mnayoitafuta haitakuwa na mshindi zaidi ya kubakisha magofu ya miji yenu."
"Vita na nani?"
"Mzee Amanyisye we' mtu mzima unajua ulichokifanya na ndicho ulichofanyiwa."
"Kwa maana hiyo wamelipa kisasi?"
"Walaa hawajalipa ila wanajipanga kulipa kisasi ila kilichotokea ulipiga wakapiga kila aliyepiga amefanikiwa kutimiza alichokikusudia bila waliotumwa kujua wanaharibu."
"Nimekuelewa, sasa utanisaidia vipi?"
"Wewe ndiye mwenye uwezo wa kumaliza tatizo kwa kwenda kwa mwenzio ili muombane samahani bila hivyo nakuapia hakuna mshindi. Mnaweza kuona mlifanya kidogo ndicho kilichompoteza mchumba wa mwanao. Kama nilivyokwisha kusema mwanzo wa moto mkubwa ni cheche na ninavyokwambia tayari moto umeishaanza kuchoma pori sijui nani atapona."
"Sasa utanisaidiaje?"
"Unatakiwa kwanza usafishwe kwa vile sasa hivi umechafuka kila nitakachokufanyia hakitakusaidia. Siku zote nguo nyeupe inataka mwili msafi."
"Mmh! Sawa, na huyu?"
"Nitakupa dawa atumie kwa siku tatu ikishindikana itabidi nimtibu kichawi."
"Sawa."
Walikubaliana kupanga siku ya mzee Amanyisye kupelekwa mzimuni kutubu aliyoyafanya ili aweze kupewa tiba. Ambakisye alipewa dawa ya unga ya kunywa na kuelezwa atumie kwa siku tatu kisha arudi. Alichukua dawa na kuondoka na baba yake aliyeamini amemjua mbaya wake hivyo ni kuingia vitani kuwasambaratisha.
Wakiwa njiani wanarudi nyumbani, Ambakisye alikuwa na mawazo mengi juu ya kauli za mganga zilizoonesha familia zote mbili zilipigana makombora, moja akiwa amelibeba yeye bila kujua ambalo liliwalipua wenyewe. Alipanga akitoka hapo akambane Atuganile amweleze alipewa nini na wazazi wake kumpelekea bila yeye kujua.
Pia hakutaka kukaa kimya alimgeukia baba yake na kumuuliza:
"Baba kumbe dawa uliyonipa ndiyo iliyotoa ujauzito wa mpenzi wangu?"
"Nani kakwambia?"
"Si Mwakasanga amesema."
"Ulimsikia amesema mimi nilikupa dawa ya kutoa ujauzito?" mzee Amanyisye alikuwa mkali kidogo.
"Hata ukisema kwa ukali baba mmenikosea, hivi nisipopona nitakufa mgumba wakati tayari nilikuwa na mtoto wangu?" Ambakisye alimuuliza baba yake kwa uchungu.
"Ambakisye aliyozungumza mganga ni mengine kabisa hayahusiani na matatizo yenu," baba yake alipinda ukweli.
"Sawa ukweli utajulikana tu muda si mrefu."
"Nimekukataza kujishughulisha na mambo ya waganga unaweza kuambiwa adui ni baba au mama yako ili tu kutugombanisha."
"Sawa baba nimekuelewa," Ambakisye alikubali shingo upande.
Walipofika nyumbani baba yake alimhimiza kunywa dawa aliyopewa na mganga na kumuomba tatizo lake liwe siri yao mpaka walimalize pia hata mpenzi wake asimweleze kinachoendelea upande wao. Ambakisye alimkubalia lakini kichwani alikuwa anawaza tofauti.
Baada ya kunywa dawa aliachana na baba yake na kujipumzisha kusubiri jioni atakapokwenda na mpenzi wake kwa bibi Tumwambilile. Alijilaza kitandani lakini mawazo yake yalikuwa mbali kuhusiana na tatizo lake pia kutoka ujauzito wa mpenzi wake.
Aliamini cheche za moto zilizoteketeza msitu zilizosemwa na mganga ni baba yake.
Lakini aliamini yote atayajua akienda kwa bibi Tumwambilile kwa kumbana na kumuahidi zawadi nzuri.
****

Jioni kama walivyokubaliana na mpenzi wake alimpitia kwao na kwenda kumsubiri kwa mbele. Kwa vile macho ya Atuganile muda wote yalikuwa barabarani alipomuona mpenzi wake akipita alimuacha apite kisha alimfuata kwa kumziba machoni kwa kutokea nyuma yake.
Ambakisye alimvutia kwa mbele ya kumkumbatia, kila mmoja alionesha furaha kwa mwenzake kutokana na kushibana mioyoni mwao.
"Za muda?" Atuganile alimuuliza mpenzi wake.
"Mmh! Kiasi namshukuru Mungu."
"Vipi, baba alisemaje?"
"Mmh! Alishtuka sana, alinipeleka mpaka mtoni kunipima kwani hakuamini kusikia tatizo langu lilianza jana usiku. Amesema tatizo lile ni la kuzaliwa nalo anashangaa mimi kulipata jana."
"Kwa hiyo amesema tatizo lako linapona?"
"Ndiyo nimeanza kutumia dawa leo."
"Mungu atakusaidia mpenzi wangu."
"Asante, Eti Atu, wazazi wako walikupa nini uniletee bila wewe kujua madhara yake?"
"Kitu gani?" Atuganile alishtushwa na swali la mpenzi wake.
"Sasa mimi nitajuaje ukiwa ulikibeba wewe."
"Mmh! Kwani ndiyo sababu ya tatizo lako?" Atuganile alishangaa swali la mpenzi wake ambalo lilimtisha na kuamini kama atajulikana yeye ndiye anayehusika hivyo lazima penzi lao lingevunjika.
"Ndiyo," alijibu kwa kutojiamini huku vidole vikiwa mdomoni.
"Basi ndiyo iliyonimaliza."

"Mungu wangu! Basi watakuwa wamenidanganya."
"Kina nani?"
"Wazazi wangu."
"Wamekudanganya kivipi?"
"Waliniambia ni dawa ya kufanya usiniache, kama ni kweli naomba usiniache mpenzi wangu."
Kauli ya Atuganile ilirudi katika agizo alilopewa Ambakisye na wazazi wake ambalo halikuwa tofauti. Kutumia uongo kama ule alimuua mwanaye bila kujua basi ndivyo ulivyoumizwa na yeye. Kwa hiyo hakuona sababu ya kulaumu kwa vile alifanya bila kufahamu.
"Atu, siwezi kukulaumu najua tatizo lipo wapi," Ambakisye alimtoa hofu mpenzi wake.
"Najuta mpenzi wangu kukubali kitu nisichokijua," Atuganile alisema huku akilia kilio cha majuto.
Ambakisye alimbembeleza mpenzi wake na kumuomba waendelee na safari yao ya kwenda kumuona bibi Tumwambilile.

ITAENDELEA........



TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU 🔞 SEHEMU YA 11

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5

CHOMBEZO: MASSAGE ROOM🔞 SEHEMU YA 21