MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN SEHEMU YA 18
MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 018
Simulizi za series
Kusikia jina la Faki, tena katikati ya shughuli nzito kama ile, haikuwa habari nzuri kabisa. Vikongwe walitinduka akili. Walitazamana katika macho ya kujiuliza nini cha kufanya, na bahati mbaya zaidi muda haukuwepo upande wao.
Haraka mmoja aliunyanyua mwili wa Malkia na kukimbia nao chumbani. Kitabu na mkasi vilitupiwa kando, ila kwakuwa muda haukutosha kuondosha kila kitu kitakachozua maswali, basi yakaachwa mengineyo. Kikongwe mmoja akaufuata mlango na kuufungua. Macho yake yalikutana ana kwa ana na bwana Faki aliyekuwa anatabasamu, tabasamu la kinafki.
Mwanaume huyo alikuwa amevalia suti nyeusi za mtindo poa wa kale. Nywele zake zilikuwa zimelala kana kwamba zimemiminiwa mafuta malaini. Uso wake, ufananao na wa fisi kwa namna zote, ulikuwa umezingirwa na ndevu zilizotindwa vema. Macho yake madogo yenye kona nyembamba yalikuwa yamezingirwa na rangi nyeusi. Kwa kuhitimisha, chini aling’ara kwa viatu vyeusi viangavu.
“Unahitaji nini kwenye upande wetu?” Aliuliza kikongwe. Uso wake ulijawa na fura. Ndani ya macho yake ungeweza kuona moto wa jazba.
“Nadhani tungeanza na salamu kwanza,” akasema Faki akiendeleza upana wa tabasamu. Hakuonekana kujali, wala kuhofia, lakini pia hakuonekana mwenye hasira. Ila kwakuwa moyo wa mtu ni chaka, basi ni vema tukaishia hapo.
“Kwani umekuja kufuata salamu huku?” aliuliza kikongwe. “Hapana,” akajibu Faki. “Ila nijuavyo mimi huwa tunasalimia wageni na kisha tuwakaribisha ndani.”
“Basi ni huko si hapa,” Kikongwe akaweka kituo. Faki alitabasamu tena alafu akawatazama wanyama wake kana kwamba anawahesabu. Alipogeuka alishusha pumzi akipandisha mabega. “Sawa, basi tusipoteze muda sana, acha niende moja kwa moja kwenye lengo. Tumekuja kuchukua cha kwetu.”
“Cha kwenu?” Kikongwe aliangua cheko la lazima. “Mlikiweka lini?” aliuliza.
Hapo Faki akaifinyanga sura yake kwa kughafirika. Alimsogelea zaidi kikongwe akamchoma kwa ncha ya kidole.
“Skiza we ajuza, kitu chochote kinachogusa ardhi yangu, chochote kile! Hata awe inzi ama sisimizi, basi ni changu! Changu peke yangu! – naomba kilichomo changu humo ndani. Tena upesi!” Kikongwe alitabasamu, meno yake meusi kama makaa ya mawe yakasalimu.
Aliufungua mlango wazi, akimtazama Faki. “Nenda kachukue hicho cha kwako,” Kikongwe alisema. Faki alirudisha tabasamu, hakusema jambo, akachukua hatua kuzama ndani.
Kitendo cha kumalizia mguu wake wa pili, mara ghafla akaona jumba lote limekuwa giza. Hakikuonekana kitu chochote hata kwa kukodoa. Kufumba na kufumbua mara sakafu nayo ikaanza kutitia! Faki alielea akienenda kwenye shimo asilolijua komo lake. Alihofia! Alipiga kelele kali. Alizamisha mkono wake ndani ya mfuko kisha akautoa haraka na kupakaza kiganja chake usoni.
Mara akajiona yu sebuleni, salama salmini! Alikuwa yu chini ameketi kitako, na wale vikongwe wakiwa wamesimama hatua chache mbele yake. Kumbe ilikuwa kiini macho! Hakukuwa na kitu kama kile, bali tu ulozi ulioundwa na kufundwa na vikongwe.
Faki akapiga kelele kutoa ishara kwa fisi wake waliokuwa nje. Ilikuwa ni nduru kali. Haraka kama upepo, fisi wakaanza kushambulia kwa kuvamia nyumba ya vikongwe. Ilikuwa ni patashika! Katika namna ya ajabu, vikongwe waligawanyika na kuwa watu kumi na tatu kwa idadi. Watu hawa wote walikuwa wana taswira ya vikongwe, usijue nani ni nani. Ila walikuwa na nguvu mno.
Walipambana na fisi kwa kuwatawanya na mikono yao. Fisi nao walitumia kucha na meno yao kupambana. Fisi huyu akirushwa kando, ama kuvunjwa shingo, basi anakuja mwingine au wengine upesi! Vikongwe waliraruriwa na kung’atwa, ila, wasiwe nyuma, nao waliwapokonya uhai fisi kadha wa kadha. Vita haikuwa lelemama!
Sebule iliharibika ikawa nyang’anyang’a. Vioo vilivyokuwa vimewekwa kwenye kona vilivunjika. Meza zilivunjwa, vyugu vikatawanyika. Sebule ilikuwa kana kwamba imetupiwa guruneti.
Fisi walipambana kwenda chumbani kuutwaa mwili wa Malkia, lakini hawakuwafanikiwa abadani. Kila walipotaka kudaka korido, mikono ya vikongwe ilifunguka na kuwatwaa, iliwavunja na kuwatengua. Hata kama walipambana kwa kutumia kucha na meno yao, hawakufua dafu.
Mpaka lahitimu lisaa limoja, fisi wote walikuwa wameshalazwa chini, hawajiwezi. Walikuwa wanakoroma kwa kuchoka ama maumivu. Fisi pekee aliyekuwa amebakia akiwa amesimama kwa miguu yake, alikuwa ni Faki! Bado alikuwa kwenye mwili wa binadamu. Muda wote huo alikuwa anatazama pasipo kufanya jambo.
Vikongwe walirudi kwenye miili yao mitatu. Walikuwa wanavuja damu kwa majeraha, ila bado walionekana wenye nguvu za kupambana zaidi. Faki alifungua vifungo vya koti lake akiwatazama vikongwe hao.
“Nisingependa tufikie huku,” alisema. “Ila kwakuwa mnataka, basi haina tabu.”
“Lenye alfa lina omega, Faki. Hutotoka hai.”
Wakasema vikongwe. Isipite muda wakanena maneno yao yasiyoeleweka, mara hali ya hewa ikaanza kubadilika. Hewa nzito ya kijani ilijaza chumba. Hewa hiyo ilikuwa inazunguka kana kwamba kimbunga ikielekea juu.
Ilipopotea, vikongwe hawakuonekana wapi wameelekea. Alionekana mtu mmoja jabali asiyeeleweka jinsia.
Alikuwa amejaza mikono kama vinu. Nywele zake zilikuwa ndefu zilizokatikakatika. Uso wake ulikuwa umekunjamana usijue pua wala mdomo vipo wapi. Kitu pekee kilichokuwa kinaonekana kwa uzuri, ni jicho moja kubwa. Jicho hili lilikuwa limekaa kwenye paji la uso.
Jitu hili likapiga kelele kali, upepo mkubwa ukazuka. Faki alimtazama kwa namna ya maulizo. Alikuwa tayari ameshafungua viifungo vya koti na shati lake. Basi akaweka mikono yake chini. Na mara akaanza kukengeuka kuwa mnyama. Mnyama huyu alikuwa mpana. Alijawa misuli. Meno yake yalirefuka na kucha zikamtoka. Manyoya nayo yalifumuka yakafunika mwili mzima.
Alikuwa fisi kamili sasa! Alinguruma kana kwamba simba. Alianza kusonga kwenda kushoto na kulia akionyesha meno yake makubwa, makali. Kufumba na kufumbua, jitu lile kama jabali likamvamia mbwa huyo. Walitupiana chini wakagaragazana.
Jitu jabali lilimnyakua mbwa likamrushia ukutani, ukuta ukacharaza nyufa kede kwa kishindo kikubwa. Fisi alinyanyuka haraka sana kana kwamba hajaumia. Alirusha miguu yake kumfuata jitu jabali. Jitu likamkamata mnyama huyo, ila kabla halijamfanya kitu, liling’atwa kwanguvu shingoni. Likapiga kelele kali za maumivu!
Kwanguvu alimnyofoa fisi, akamrushia tena ukutani.
Shingoni alikuwa na jeraha kubwa linalovuja damu. Alifunika jeraha hilo na mkono wake wa kushoto. Ule ukuta aliorushiwa fisi kwa mara ya pili, ulidhoofika mno, ukashindwa kustahimili na mara ukadondoka kumfunika fisi, Faki.
Jitu jabali halikutaka kungoja.
Akiwa amefunika jeraha lake shingoni, alikimbia kuelekea alipo fisi. Alidaka mkia wake akamvuta kana kwamba paka! Alimzungusha kana kwamba panga la feni alafu akamrushia tena ukutani. Fisi alipiga kelele kali. Alibomoa ukuta na kujeruhi mkono wake wa kuume.
Jitu likapiga kelele kali kutangaza ushindi. Alikuwa sasa anaelekea kummaliza adui yake, ila kabla hajafika, fisi watatu wakamrukia mgongoni kumparua na kumng’ata. Jitu jabali likatumia mkono wake kuwafagia fisi hao. Liliwatupia chini kama mkulima amwagavyo jasho kwa kidole. Kisha likawasinya kuwavunjavunja!
Fisi wakawa chapati. Jitu jabali liliporusha macho yake kutazama kule alipommwagia Faki, halikumwona! Alikuwa amepotea. Lilipepesa macho yake huku na huko pasipo mafanikio. Lilipiga hatua likiangaza. Lilitumikisha masikio yake kuskiza, lakini bado hakupata kitu.
Lilisogelea eneo lenye kifusi ambapo ndipo Faki alitupiwa, akatazama hapo hatua za mnyama lipate kujua mwelekeo. Likiwa hapo, mara likasikia mngurumo nyuma yake. Liligeuza kichwa kutazama, uso kwa uso likakutana na fisi hewani akiwa ameachama mikono. Kabla jitu halijafanya kitu, likavamiwa na kuangushwa chini.
Fisi aliwahi kuung’ata mkono wa kuume wa jitu. Aliung’ang’ania mno akijaribu kuunyofoa. Jitu lilituma mkono wake wa kushoto kumtoa fisi, fisi akaukwepa mkono huo na kuuparua kwa kucha zake dhalimu. Jitu likapiga kelele. Ila halikukoma. Sasa lilituma mikono yake yote miwili inayochuruza damu, haraka, likamkamata fisi shingoni.
Lilimminya kwanguvu zake zote mpaka aliposikia fisi akilalamika, na hatimaye mlio – kakak! Fisi akawa ametulia tuli, ulimi nje. Jitu likamtupia fisi kando na kisha likanyanyuka.
Vita sasa ilikuwa imekoma, vikongwe wakiwa wamebakia kama washindi. Miili yao ilinyofoka toka kwenye mwili ule mkubwa wa jitu jabali. Walikuwa wana majeraha makubwa na tena wakiwa wamechoka mno. Walitazama mazingira yao wakalaani. Walielekea chumbani kuutazama mwili wa Malkia pamoja na mkufu.
Lahaula! Mwili haukuwepo wala mkufu. Walitazama huku na huko, hakukuwa na kitu! Walitoka ndani ya chumba, wakaenda huko nje kuangaza. Napo hawakuona lolote. Mwili ulikuwa umeondoka na mkufu wake!
“Hapana!” aliwika kikongwe. “Hapana! Hapana! Hapanaa!” alilia kwa uchungu. Alipiga kelele kali zilizoita Tanashe nzima.
Labda wangeweza kusahau kuhusu mkufu, ila majeraha yaliyokuwa yametapakaa kwenye miili yao yangewakumbusha, tena kwa maumivu makali! Maumivu pasipo mbivu.
.
.
.
.
.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
.
.
.
.
“Mheshimiwa, una mgeni,” ilikuwa sauti ya mlinzi ikimnong’oneza Phares aliyekuwa chumbani akiketi kwenye kiti kirefu. Phares akatikisa kichwa chake, mlinzi akaondoka.
Mkononi mwake, Phares, alikuwa amebebelea mkufu wa dhahabu wenye kidani kikubwa chenye muundo wa saa. Kidani hiki, ndani yake, kilikuwa kina mshale mmoja uliokuwa unazunguka, na macho ya Phares yalikuwa yanafuatisha mshale huo.
Akili yake haikuwepo pale. Kwa namna moja, mshale ule uliokuwa unazunguka ulikuwa unamfanya asahau ulimwengu wa karibu na kuuwaza ule wa mbali. Kama si mlinzi kuja kumshtua, basi angeendelea kukodolea kidani kile kilichomteka mawazo.
Alinyanyuka akatengenezea shati lake jeupe lenye urembourembo kolani. Alikuwa amependeza kwa suruali yake nyeusi na viatu vyake vya ngozi rangi ya kaki. Alienda sebuleni, na pengine pasipo kuwaza nani anayemuita. Huko akamkuta Rhoda, mwanamke aliyempokea kwa tabasamu karimu, pana. “Habari, Phares!” alisalimu Rhoda akisimama.
“Njema, karibu.”
“Nimeshakaribia. Haukuwa unautegemea ujio wangu.”
“Kabisa, sikudhani kama ningepata pata mgeni kama wewe muda huu.”
Walipeana mikono wakiisindikiza na tabasamu, kisha wakaketi.
“Nimeshangazwa sana na msiba huu,” alisema Rhoda.
“Kila mtu ameshangazwa,” akadakia Phares. “Ila tumeona ni muda wa kwenda mbele sasa.”
“Sawa, ila ndio kwa muda mfupi kiasi hiki?”
“Ndio. Msiba haukuwa na watu kabisa, si wa nje wala wa ndani. Yanini udumu kwa masiku?”
Hakukuwa na maneno, kukawa kimya kwa muda. Rhoda alikuwa anaigiza kana kwamba ameguswa.
“Rhoda,” Phares aliita. “Ni nini umekuja kunambia?” akauliza.
Rhoda akashusha pumzi ndefu na kutazama chini. Hii ndiyo ilikuwa nafasi adhimu aliyokuwa anaitaka. Akili yake ilianza kuwazua upesi namna gani awasilishe mawazo yake. Basi akajikuta anatabasamu kabla hajasema.
“Hamna kitu kikubwa saana nilichonacho Phares, ila tu jambo dogo ninalotaka kukusitizia na kukuomba vilevile.”
“Lipi hilo? – Ni kuhusu mkufu?”
Moyo wa Rhoda ukatatuka kwa hofu. Macho ya Phares yalikuwa yanamtazama kwa umakini, akajitahidi kubakiza utulivu wake. Ni jicho moja tu la kushoto ndilo lilipepesuka.
“Ndio, ni kuhusu mkufu.”
“Bila shaka umekuja kuniomba nikautafute.”
Rhoda akakaukiwa kauli. Ni kana kwamba Phares alikuwa anajua haja yake hivyo basi akawa anamsanifu.
“Ni kwanini unautaka sana huo mkufu, Rhoda?” “Phares, laiti ungalikuwa unajua uwezo na nguvu ya mkufu huo, usingalikuwa hapa. Ungelikuwa huko nyikani kuutafuta.”
“Rhoda, sina haja na madaraka.”
“Si tu madaraka, Phares. Mkufu ni zaidi ya hilo! Kwani nini haja ya moyo wako?” Phares alikuwa kimya kidogo kama mtu anayetafakari. Rhoda alimtazama kwa uchu wa kungojea jibu.
Phares aliangaza huku na huko, na mara macho yake yakawa mekundu. “Nina haja moja kubwa, Rhoda. Haja ambayo inanipa maswali kedekede na kunikosesha amani kabisa ...”
“Ipi hiyo?” Rhoda alishindwa kuvumilia.
“Haja ya kujua asili yangu,” Phares akajibu na kuongezea: “Haja ya kujua wapi nilipotokea, wapi nyumbani kwetu, wakina nani wazazi wangu, wakina nani ndugu zangu. Haja hii imekuwa ikinitesa kwa karne sasa.”
“Phares, imewezekanaje ukafikia umri huu usijue kwenu ni wapi? Ulishawahi kuwa mtumwa?”
“Sijui.”
“Hujui? Ulishawahi kupata tatizo lolote la kumbukumbu?”
“Sikumbuki.”
“Ulikutanaje na Vedas?”
“Rhoda, sifahamu. Hakuna jambo nafahamu, hakuna jambo nakumbuka. Kila ninapovuta kumbukumbu zangu, mtu wangu wa kwanza kumuona ni marehemu Vedas. Si kingine!”
Hapo Rhoda akapata mashaka. Akili yake iligoma kabisa kuzaa majibu. Ila waswahili husema kufa kufaana, Rhoda akaona kuna fursa ndani ya tatizo hilo.
“Phares, unahitaji kuutafuta mkufu. Utakusaidia.” Phares akatabasamu kiupande. Aliona sasa hamu ya Rhoda inamvusha mipaka.
Alisimama akatengenezea koti lake akisema:
“Nadhani tutaongea siku nyingine, Rhoda.”
Rhoda akasimama haraka. Alimshika mkono Phares akimtazama usoni.
“Phares, kama unataka kujua, tafuta mkufu! Muda si mrefu wazee hawa wa baraza watajiuliza kuhusu wewe. Watakuuliza umetokea wapi na familia yako ina hadhi gani. Wanaweza hata wakakufukuzia mbali. Utaenda wapi na huna familia? Upo tayari ukaanze moja na ulikaribia mia? … Fikiri!”
Phares hakujibu kitu, ila maneno hayo hayakutokea upande mwingine wa sikio. Aliukwapua mkono wake toka kwa Rhoda, akaenenda zake. “Nahitaji muda,” alisema pasipo kujigeuza.
“Ila kumbuka muda ni mnafki!” Rhoda akamsisitizia. .
.
.
.
.
.
.
.
ITAENDELEA........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni