PENZI LISILO NA MWISHO SEHEMU YA 2



Simulizi: PENZI LISILO NA MWISHO

Mtunzi: NYEMO CHILONGANI

SEHEMU YA 2

ILIPOISHIA

“Wakina nani?” ilisikika sauti ya msichana mmoja, ikamfanya Razak kuogopa, akageuka kule sauti ilipotoka, akanyoosha bunduki kuelekea kule.

“Unataka kuniua?” ilisikika sauti hiyo ikiuliza.

“Wewe ni nani?” aliuliza Razak huku kwa mbali akitetemeka.....

ENDELEA

alihisi kama alikutana na jini kutokana na muda na mahali penyewe.

“Naitwa Aisha...”

“Aisha wa wapi?”

“Wa hapahapa...”

“Unataka nini?”

“Kwani wewe unataka kuwaua wakina nani?”

“Wewe nani?”

“Kwani nimekwambia mimi nani?”

Muda wote Razak alikuwa akitetemeka, japokuwa alikuwa pembezoni mwa bahari hivyo na upepo mwingi kupuliza lakini kitu cha ajabu kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Alitetemeka, alihofia, moyo wake ulimwambia kwamba yule aliyesimama mbele yake hakuwa binadamu bali alikuwa jini ambalo kazi yake ilikuwa ni kukaa pembezoni mwa bahari kwa ajili ya kufanya mawindo yake.

Msichana yule alisimama sehemu iliyokuwa na giza, Razak hakuweza kumuona uso vizuri hivyo kubaki akiyafikicha macho yake ili aweze kumuona vizuri msichana huyo aliyekuwa amesimama sehemu isiyokuwa na mwanga wa kutosha.

“Nikusaidie nini?” aliuliza Razak, hata sauti yake, ilionyesha ni jinsi gani alikuwa na hofu.

“Nataka unisaidie hela ili kesho nikale...” ilisikika sauti ya msichana yule ikijibu.

Hapo ndipo Aisha alipoanza kupiga hatua kuelekea kule alipokuwa Razak ambaye alisimama na bastola yake.

Alipotokeza na kusimama sehemu yenye mwanga, Razak hakuamini yule mtu aliyekuwa akimwangalia. Alikuwa msichana mrembo mno, mzuri wa sura mwenye umbo matata ambalo lilimfanya kutulia na kumwangalia vizuri.

Kichwa chake kikaanza kumwambia kwamba msichana yule alikuwa jini kwani kulikuwa na majini mengi yaliyokuwa yakijitokeza nyakati za usiku tu, tena yalikuwa mazuri ambayo kazi zao kubwa zikiwa ni kuua na kunyonya damu.

Mkono wake ulishika bastola lakini hakuweza kufanya kitu chochote kile, mwili wake ulikuwa ukimsisimka, hofu ikamshika moyoni, akabaki akiwa amesimama tu akimwangalia msichana yule.

“Wewe ni nani?” aliuliza Razak, swali moja alilolirudia mara ya pili.

“Nilisema naitwa Aisha...”

“Mmmh!”

“Nini?”

“Nikusaidie nini?”

“Hela ya kula!”

“Kwani wewe ni ombaomba?”

“Hapana! Ni chokoraa tu, sina kitu, kila siku ninashinda mitaani na wenzangu...” alijibu Aisha.

“Na wale waliokimbia unawajua?”

“Ndiyo!”

“Ni wakina nani?”

“Ahmed na Mohammed, mapacha wanaoishi mitaani kama mimi,” alijibu msichana huyo kwa sauti ya upole.

“Una miaka mingapi?”

“Kumi na saba!”

“Kwa nini upo hapa?”

“Mbona maswali mengi na wewe kama polisi! Unanisaidia hunisaidii?”

Razak aliyatuliza macho yake kwa Aisha, kila alipokuwa akimwangalia, hakuamini kama angewahi kukutana na msichana aliyekuwa na sura nzuri kama aliyokuwa nayo Aisha aliyesimama mbele yake.

Akashindwa kuvumilia, kule aliposimama alijiona akiwa mbali hivyo kuanza kumsogelea. Moyo wake ulianza kwenda sehemu nyingine kabisa, kulikaribia dimbwi zito la mahaba.

Ni kweli alikuwa amekutana na wasichana wengi wazuri akiwemo Sabrina lakini yule aliyesimama mbele yake, alikuwa mzuri zaidi ya wote. Japokuwa alikuwa na mavazi machafu lakini hilo halikufanya kuuficha uzuri wake.

Alipokuwa akimsogelea, naye Aisha akaanza kurudi nyuma, alikuwa akitetemeka, hakuwa akijiamini hata kidogo, alimuogopa mwanaume huyo na ile bastola iliyokuwa mkononi mwake ikamuongezea hofu zaidi.

Aisha hakutaka kusimama, alihisi kwamba mara baada ya Razak kuwakosa vijana wale basi angeweza kumkamata yeye mwenyewe, alichokifanya ni kuanza kukimbia kuelekea Feri.

Alikuwa mzoefu wa njia, alijua wapi palikuwa salama wapi palikuwa hatari, alikimbia harakahaharaka huku nyuma Razak akipiga kelele kumuita lakini hakusimama, akatoweka machoni mwake.

“Aishaaaa...Aishaaa...” alibaki akiita, mbele yake hakukuwa na mtu, aliangalia huku na kule, alikuwa peke yake hali iliyomfanya kurudi lilipokuwa gari lake, akaingia ndani ya gari, mawazo yalimjaa juu ya msichana huyo aliyekutana naye usiku wa siku hiyo, hata safari ya kuelekea Kigamboni, haikuendelea, akageuza gari na kurudi nyumbani kwao, Osterbay huku kichwani akiwa na mawazo mengi juu ya Aisha.

*****

Asubuhi ilipofika, Razak akaamka, akayafikicha macho yake na kutoka kitandani. Akaanza kukumbuka kile kilichotokea usiku uliopita kama kilitokea kweli alikuwa alikuwa katika moja ya ndoto fulani.

Alitulia na kukumbuka vizuri, kichwa chake kikamwambia kwamba kile kilichotokea hakikuwa ndoto bali kilikuwa kitu halisi, ni kweli alikutana na msichana mrembo ambaye hakuwahi kumuona maisha yake yote.

Alijaribu kuivuta sura ya msichana yule kichwani mwake, urembo wake ukautetemesha moyo wake, hakuamini kama kweli ndani ya dunia hiihii kungekuwa na msichana mrembo kama alivyokuwa Aisha huku akiwa chokoraa.

Siku hiyo alitaka kumuona tena Aisha, alikuwa na uhitaji naye, ikiwezekana amwambie kwamba awe mpenzi wake na mwisho wa siku kumuoa.

Wakati akiyafikiria hayo, mara akasikia simu yake ikiwa imeingia ujumbe mfupi, kwa harakaharaka akaichukua simu ile na kuanza kuusoma ujumbe huo uliotoka kwa Sabrina.

“Nataka uniache na maisha yangu,” ulisema ujumbe huo kutoka kwa mpenzi wake, Sabrina.

“Poa, mimi mwenyewe ndiyo nilitaka kukwambia hivyohivyo” naye alijibu.

Muda huo haukuwa wa kumfikiria Sabrina, alimchoka msichana huyo kwa sababu katika kipindi cha karibuni katika uhusiano wao, haukuwa umetulia, kila siku ilikuwa ni kugombana tu.

Moyo wake ulikuwa kwa msichana mwingine kabisa, chokoraa ambaye alikutana naye usiku wa kuamkia siku hiyo, kwa jinsi alivyomjibu Sabrina ujumbe ule, hata yeye mwenyewe alijishangaa kwani alimpenda sana msichana huyo, cha ajabu, ujumbe ule aliujibu harakahara pasipo kujifikiria.

Alipomaliza kuoga, akatoka sebuleni, akakutana na wazazi wake, akazungumza nao kisha kuwaambia kwamba ana safari ya kueleka sehemu fulani ambapo kulikuwa na mtu muhimu alitaka kumuona.

“Nani?” aliuliza baba yake.

“Rafiki yangu! Nitarudi...” alijibu Razak.

“Usichelewe, kuna mengi nitataka kuzungumza nawe...”

“Hakuna tatizo.”

Razak akatoka nje, sehemu ya kupaki magari, kulikuwa na magari mengi ya kifahari, alibaki akiwa amesimama, macho yake yalikwenda kwenye moja baada ya jingine, alitaka kuchukua gari ambalo lingemfanya kuonekana wa kawaida huko atakapokwenda, mwisho wa siku akaishia katika Porte ya kijivu, akaifuata na kuingia, baada ya hapo, akaanza safari ya kuelekea Posta.

Siku hiyo hakutaka kufanya kitu chochote kile, alichokitaka ni kuonana na msichana Aisha tu. Alitokea kumpenda sana, alimhitaji kuliko msichana yeyote yule.

ITAENDELEA....



TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU 🔞 SEHEMU YA 11

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5

CHOMBEZO: MASSAGE ROOM🔞 SEHEMU YA 21