MSITU WA AJABU EPISODE:66
Story: MSITU WA AJABU
Episode:66
Mtunzi:Nellove
Ilipoishia...
Alipomaliza kufunga alikirudisha kwenye begi na kuchukua kingine maana walikuwa navyo vingi. Alirudia kauli yake.
"Kuna kitu kinachanganya nashindwa kuelewa"
"Ni kitu gani?" Aliuliza Joram lakini hata kabla ya kujibu Sylvestre alianguka chini huku damu zikimtoka puani na kwenye masikio. Wote walishituka na kumgeukia hata hivyo hazikupita dakika nyingi naye Daniel alianguka.
Songa nayo...
Butwaa iliwapiga wote kwa sababu ya hiki kilichotokea. Sylvestre pamoja na Daniel wote walikuwa chini na kadri sekunde zilivyosogea mbele hali zao zilionekana kutokuwa sawa kabisa. Wale wengine wakiongozwa na Mr Tommy walifanya haraka na kumsogelea mwenzao. Ambacho Kilifanyika hapo ni kuchukua baadhi ya vifaa vilivyokuwa ndani ya begi na kuanza kufanya mambo waliyoyajua wao wenyewe katika kuhakikisha mwenzao anakuwa sawa.
Wote walimsogelea Sylvestre wakati huo Daniel aliachwa peke yake bila msaada wowote. Hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi na hata upumuaji wake ulianza kuwa wa shida.
Dakika ziliendelea kwenda mbele. Hali ya Sylvestre iliendelea kuimarika na hata zile damu zilizokuwa zinatoka puani na kwenye masikio zilikata wakati huo sasa, hali ya Daniel haikuwa mbaya tu bali kuna mabadiliko yalitokea pia, damu zilianza kutoka puani na masikioni lakini hakuna hata mmoja aliyethubutu kumsogelea na kujaribu kumpa msaada.
"Nimekwisha mimi. Nakufa huku najiona" Daniel alijisemea katika fikra zake, alipotaka kutoa sauti aliishia kugugumia tu na kumumunya maneno. Kutamka maneno haikuwa rahisi. Alitapa tapa pale chini akionesha kutamani kitu asichokuwa na uwezo wa kukipata au kukifanya. Alitamani kuongea, alitamani kusimama, alitamani hata kunyanyua mkono ilishindikana.
"Jamani hamnioni?? Hamuoni ninavyoteseka?" Alijaribu kuongea kwa nguvu lakini sauti iliyotoka ilikuwa kama ya mtu mwenye ububu.
Hali ya Sylvestre ilipokuwa vizuri kabisa walijiweka sawa na kuanza kupiga hatua kuelekea mbele.
"Hapa sasa tutafanya kazi yetu kwa urahisi kabisa" alisema Mr Tommy. Waliondoka huku wakipuuzia zile kelele za Daniel aliyekuwa pale chini. Waliondoka.
Kazi ya kukamata mizuka iliendelea. Kama ilivyoelezwa hapo awali kuwa kulikuwa na vifaa mbalimbali vya kufanyia kazi yao hii ikiwemo nyenzo ya kunasa mizuka bila kusahau miwani. Miwani ile iliwasaidia kung'amua ni wapi mizuka hii ipo, wakishawaona basi huwanasa na ile nyenzo na wakishanaswa basi hubadilika umbo na kuwa kama cheche za moto. Umbo lao hili huwa rahisi kufungwa katika vile vimkebe. Sasa kutokana na uwepo wa miwani basi inakuwa si rahisi kuondoka bila kumaliza kunasa mizuka yote iliyopo ndani ya msitu huu.
Kazi iliendelea huku ikionekana kuwa rahisi zaidi ya mwanzo. Hakukuwa na changamoto yoyote ile na kwakuwa walikuwa na vikebe vya kutosha basi haikuwa shida kwao kuendelea kunasa mizuka ile ambayo ilikuwa mingi sana kwa idadi.
Huu upande wa pili bado mambo yalikuwa magumu tena mno kwani hadi sasa hata nguvu za mwili zilimwisha Daniel. Dakika ziliyoyoma akiwa katika hali ile ila muda fulani hivi ghafla ulitokea mwanga mbele yake.
Ule mwanga ulionekana kama kusogea eneo alilopo Daniel. Hofu ilizuka ndani yake lakini kwa kuwa hakuwa na chochote cha kufanya basi alitulia huku akiamini mambo ya msitu yameanza. Alijilaumu kwa kukubali kuja ndani ya msitu kwa mara nyingine, msitu uleule ambao ulimtesa pengine kuliko yeyote.
Mwanga ulisogea na kufika karibu zaidi kisha baada ya sekunde kadhaa ulijisogeza hadi usawa wa kifua cha Daniel na baada ya hapo ulitoweka. Kitendo hiki kiliufanya mwili wake kuwa mzito zaidi kiasi cha kushindwa hata kugeuza shingo. Achana na uzito huo, maumivu nayo yalianza kusambaa katika kila eneo la mwili wake hasa usoni. Kama angeweza kutoa machozi basi angetoa hata ndoo nzima, lakini angeyatoa wapi machozi?? nguvu ya kukamua machozi ilifutika.
Ni dakika tano tu tangu hali hii kutokea lakini aliona kama miaka mitano hivi ya mateso. Dakika tano zilipopita ule mwanga uliibuka tena usawa wa kifua na kuanza kurudi kule ulikotoka mara ya kwanza kisha ulipotea kabisa. Ajabu ni kwamba baada ya hili jambo Daniel alijihisi mwepesi mno na hata maumivu yaliyomtafuna nayo yalitoweka kabisa. Kwa namna hali ilivyokuwa alihisi labda anaweza hata kusimama au kufanya chochote kile kwa wakati huu.
Alipojaribu hakika iliwezekana. Alisimama na alipotaka kupiga hatua, alipiga tena si moja ni zaidi ya hapo. Hata alipogusa masikio na pua hakuhisi damu kutoka wala maumivu hayakuwepo. Lilikuwa jambo la kushangaza na hakujua imekuwaje. Sasa Ukweli kuhusu tukio hili ni kwamba ule mwanga uliposogea karibu na kifua chake uliingia mwilini na ndio maana mwili ulikuwa mzito ghafla. Ule mwanga ulifanya msaada kwa kupambana na hali ile iliyoingia ndani yake na baada ya kuweka mambo sawa ndipo ukatoka na kutoweka. Huu mwanga ni nini???Mwanga huu ni yule kiumbe wa nusu kuzimu.
Daniel alikuwa vizuri kabisa na sasa alianza kutafakari ni wapi pa kwenda, je arudi au awatafute aliokuja nao?
Alianza kupiga hatua huku akijitahidi kuushinda ule woga uliokuwa unazaliwa ndani yake. Kuwa ndani ya msitu wa OGOWE usiku, tena pekee bila mtu mwingine pembeni si jambo rahisi. Alijikaza kiume.
Ndani ya dakika 20 za kutembea bila kujua ni wapi atatokea, alifika mahali fulani ambapo alisikia kelele fulani za chini kudhihirisha kwamba palikuwa na watu. Hakuwa na shaka kwani aliamini watakuwa ni wenzake aliokuja nao.
Alijibana mahali kuchunguza vizuri ili kupata uhakika wa hiki alichokihisi. Mahali alipojibana palimpa wasaa wa kuona mwanga. Macho yake yalipoona zile taa zenye mwanga wa bluu alijua ni wale aliokuja nao hivyo alijitokeza pale. Hakika ulikuwa mshituko wa aina yake kwa hawa watu kwani hawakutegemea kama atapona. Mioyo iliwaenda mbio wakidhani ni kiumbe cha tofauti, Daniel aliwatuliza kwa kuwahakikishia kuwa ni yeye. Alisogea karibu na kwa msaada wa mwanga ule wa bluu alifanikiwa kumuona mmoja wa wale watu akiwa chini.
Alishuka chini kumuangalia vizuri, aligundua kuwa yule hakuwa hai.
"Mbona ameshafariki huyu" alitamka Daniel ila kabla halijatoka neno lolote ilisikika sauti kutoka juu
"Huuuuuuuuuuuuuuuuuuuuuu!!!!!!!"😯
Hii sauti iliwaogopesha wote, kila mmoja alinyanyua kichwa na kutazama juu. Hawakuona chochote kile sasa wakati wanaendelea kutazama huku na huku ile sauti ilisikika tena na kwa sasa ilisikika kwa chini na kwa karibu zaidi. Hazikupita hata dakika mbili kilizuka kishindo katikati yao na kila mmoja alianza kukimbia. Ilikuwa bahati tu walikimbilia upande mmoja.
Sasa mambo yalikuwa ni kukimbizana ndani ya msitu huo kila mmoja akijaribu kuokoa uhai wake. Kwa nyuma sauti ya muungurumo wenye kufanana na simba ilisikika. Milio iliendelea kuwa mingi kadri muda ulivyosonga na kadri walivyokimbia, na si sauti za muungurumo tu bali hadi sauti za wanawake waliosikika kama wanalia zilisikika zaidi.
"Huu msitu una balaa"
Waliendelea kukimbia lakini muda fulani baadae zile sauti zilianza kutoweka tena. Utowekaji wake ni wa maumivu yani kama wahusika wa hizo sauti walikuwa wakikutana na maumivu makali.
Basi baada ya hapo walipata nafasi ya kutulia huku kila mmoja akihema sana.
Baada ya kuhakikisha kwamba kila kitu kipo salama basi ilibidi wajipange upya kumaliza kazi yao. Wengine hawakuwa tayari lakini mkuu aliwataka wafanye kazi wamalize mapema. Hawakuwa na namna ilibidi wafanye kazi ile.
Kama ilivyo ada waliendelea kuelekezwa ni wapi pa kwenda. Walifanya kazi yao vizuri na kwa urahisi sana Pengine kuliko mara nyingine zozote. Kazi ilikuwa rahisi kwani ile mizuka haikuwa inaleta ukorofi kama ya awali.
"Tumebakiwa na kazi ndogo sana hapa"
Basi Katika kumalizia kazi yao, ilifika wakati mkuu wao alifanya kazi ya pekee kuunasa mzuka ambao kwa maelezo yake ni kwamba ulikuwa mkubwa na wenye nguvu kuliko mizuka yote msituni. Lakini licha ya hivyo lilikuwa jambo jepesi kumkamata kuliko alivyowaza.
Huu mzuka uliponaswa Daniel alishangaa kuhisi kama anamuona kiumbe wa nusu kuzimu akiongea huku anatoa machozi.
"Ahsante sana. Nashukuru sana kwa hili" Daniel aliogopa sana kuona hivi kwani hakujua maana yake ni ipi hasa. Alikuwa na uhakika kuwa huu mzuka uliokamatwa ndio yule kiumbe wa nusu kuzimu sasa Je kwanini anashukuru? Kwanini analia?? Daniel aliogopa kuonekana amesababisha matatizo kwa viumbe hivi ambavyo mara nyingi vimemsaidia.
ITAENDELEA.........
TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.
Maoni
Chapisha Maoni