KOFI LA KISOGO SEHEMU YA 8



“KOFI LA KISOGO”

Na:Arnold Machavo

Mbeya—Tanzania

Sehemu ipatayo ya 08
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
««Ilipokomea...
“Kwanini unanikimbia sasa?” Waridi alihoji baada ya kuambiwa ukweli.
“Hakuna kitu eti nimefikiria tuu nisogee pembeni,” Zena alimjibu huku akitabasamu. Tabasamu lenye ishara ya kuwa amani ipo kati yao hivyo dada mtu asihofu...

TEREMKA NAYO...»»
“Sawa hakuna tatizo nashukuru sana kwa msaada wako chei wangu.”
“Hahaha eti chei. Hicho kijina chenu na mama nilishakisahau usinikumbushe kabisa hata sikitaki,” Zena aliongea na kusababisha kicheko kwa wote wawili mara baada ya kukumbuka jinsi jina hilo la utani lilivyokuwa likitumika hususani kipindi walipokuwa wadogo.

Jioni Hussein aliporejea nyumbani alipokelewa na kitu cha kwanza kwake kilikuwa ni kumuona Hassan wake furaha yake kubwa. Walipotulia Waridi ndiye alikuwa wa kwanza kugusia juu ya kutaka kuondoka kwa Zena.
“Haa kwanini sasa? maan...” Hussein aliongea.
“Aah aah jamani kaumri kanasogea na yeye,” Waridi alimjibu kwa kumkatisha.

“Shida siyo hiyo. Nimepata nafasi adhimu aliyoniuliza nimuulizie kwa baadhi ya watu huko.”
“Nafasi ipi mume wangu?”
“Alisema anahitaji kazi ya kufanya usafi kwenye hospitali hata kwa miezi kadhaa tuu. Nilipowaulizia baadhi ya rafiki zangu waliopo pale wamenihakikishia kuwa nafasi ipo.”
“Eeh! nashukuru sana shemeji!.” Zena alishukuru mno baada ya kupata shavu.

“Kwahiyo mlifanya kimyakimya daah sawa.”
“Surprise hiyo kwenye maisha kawaida.”
“Ila nashangaa kwanini mdogo wangu anakwenda kutafuta kazi hiyo. Kufua mashuka ya wagonjwa na kudeki yake maeneo hapana sijapenda.”
“Ongea naye dada yako huyo, mimi aliniuliza nafasi, nikamtafutia na imepatikana. Kazi ni kwake,” Hussein aliongea maneno hayo na kuondoka kwani mjadala ulioonekana kufuata haukumuhusu hivyo hakuwa na haja ya kusikiliza.

Waliendelea kuzozana kwa muda ndugu wale wawili huku kila mmoja akiona mawazo ya kwake ndiyo bora kuliko ya mwenziye. Bahati nzuri na mbaya Zena alisisimamia msimamo wake kuwa lazima aende. Bora akafanye hata kama ni kwa muda mfupi lakini kuliko kutokufanya kabisa. Waridi alimuona kama anamdharilisha yeye au familia yao lakini hayakuwa maamuzi ya Zena kuikacha fursa hiyo. Zena kupangiwa juu ya hilo na ilihali anaishi nyumbani kwa Waridi. Pamoja na yote hakuna kilichoharibika kwani alimwambia kuwa endapo mambo yakienda kombo basi atarudi kupata uelekeo mpya lakini anataka kujaribu kwanza.

Baada ya siku kadhaa Hussein alimuunganisha kwa baadhi ya rafiki zake waliosoma nao miaka hiyo ambao walikuwa wafanyakazi wa pale hospitalini. Zena alipata shavu nono na hakuwa na budi kulipokea. Hakutaka kuondoka kwa haraka katika nyumba ile. Alitazamia kufanya kazi kwanza na baada ya kupata ahueni ndipo aweze kutimua vumbi. Kazi ilikuwa ya asubuhi na jioni hivyo wakati wa mchana alikuwa huru kufanya majukumu mengineyo. Hii ilimpatia ahueni kwani ndivyo alitarajia.

Waridi baada ya kuona kuwa Zena anaweza kuondoka siku si nyingi alipata wazo la kutafuta dada wa kazi kwa ajili ya kumsaidia shughuli kadhaa. Ingawa lengo kuu la kuwatafuta watu hawa huwa ni kusaidia kazi kazi za kupika, kufua na usafi lakini baadhi yao hujikuta wanaweza kusaidia mpaka kumpooza kichwa cha familia. Hatukatai wanaweza mno jukumu hilo lakini hawakujia wala kuitiwa kuja kufanya hilo.

Waridi alizungumza na mama yake amfanyie mpango huo kirahisi. Kwa bahati nzuri kuna binti ndugu yao alikuwa amemaliza kidato cha nne na hakuwa na kitu anafanya huko hivyo alipendekezwa aje kusafisha macho mjini pamoja na kukaa kwa dada. Tabia yetu watu wa mikoani tunapenda mno kwenda mjini kupunga upepo mjini hasahasa daslam. Hatukatai ni wasumbufu lakini mbona huwa mnatuagiza tuje na mchele au maharage ya Mbeya, vungeni basi.

Kazi kwa upande wa Hussein ilikuwa sehemu salama kwani alikuwa ni mtu wa kujituma vilivyo. Vivyo hivyo kwa upande wa Waridi kazi ilikolea katika mapishi hotelini kule. Zena na yeye hali ilikuwa si haba alianza kufaidi mema ya nchi yetu. Familia ilikuwa ni ya kazi kazi. Siku na wiki zilikimbia huku Hassan akiendelea kuongezeka na kuwa mchangamfu zaidi. Wakati huo tayari yule dada wa kazi alikuwa ameshafika mjini. Leila ndiye alikabidhiwa kwa Waridi kwa ajili ya uangalizi wa mtoto pamoja na shughuli zingine ndogondogo kutokana na kubanwa na majukumu mengi.

Namna siku zilivyokuwa zikisogea ndivyo Hussein aliendelea kuimarika kiuchumi. Miradi kadhaa aliyokuwa anaiwekea mkazo ilizidi kumpatia matumaini ya kupata ahueni ya maisha. Hakuna mafanikio yanayopatikana kwa wakati mmoja pekee, lazima kuna kipindi cha kupitia magumu. Kuna wakati mtu anaweza kuahirisha kufanya jambo fulani kwa sababu ya kukata tamaa.

Yote juu ya yote haitakiwi kukata tamaa kwenye kutafuta, lakini pia inatakiwa kutambua kuwa kuna wakati inabidi kuruhusu jambo kuliweka kando au kuachana nalo ili kuacha kuendelea kung'ang'ania mateso yasiyokuwa na faida wala uelekeo wa hapo baadaye. Mfano kwenye ndoa mtu hawezi kuwa anapigwa na kutolewa ngeu kila siku halafu anajipatia matumaini kuwa anavumilia ndoa. La hasha huo ni utumwa ni bora kuachana na hiyo ndoano kuliko kuendelea kuteseka. Na endapo kuna uhaba wa pesa kuna matatizo mengineyo ndani ya familia ndipo mtu anaweza kujishikiza kwani ndiyo tafsiri sanifu katika uvumilivu ndani ya ndoa.

Ilikuwa ni siku tulivu yenye hali safi ya hewa siku ambayo mara baada ya Zena kuamka na kufika hospitali alifanya usafi na kumaliza zamu yake kisha hakutaka kusalia eneo lile tena. Alirejea moja kwa moja nyumbani kupumzika jambo ambalo ni nadra sana kwake. Umbali haukuwa mrefu sana kutoka hospitali mpaka nyumbani kwa Waridi. Aliamua kutembea siku hiyo kwa ajili ya kunyoosha miguu.

Wahenga walituhadaa kwa kusema “mtembea bure siyo sawa na mkaa bure” sijui huyo akaaye bure walimaanisha yupi. Kwani aliyepata lifti ya bure ya gari au bajaji huwa amekaa bure na ni bora zaidi kuliko anayetembea bure na kumulikwa na jua au kunyewa na mvua hizi za masika.

Njiani alikuwa katika mwendo wa taratibu mithili ya mtu mgeni anayekariri mitaa akiogopa kupotea njia. Baada ya mwendo wa takribani dakika thelathini na mbili alikuwa tayari ameshafika mtaani penyewe. Alipofika nje ya geti la nyumba ya Waridi alishangaa alichokuwa akikiona mbele yake. Alibaki amefumba mkono wa kulia kwenye mdomo wake asiamini aonacho. Tena alikuwa amesimama akishindwa aelekee mbele au arudi alikotoka...



ITAENDELEA.........


TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU 🔞 SEHEMU YA 11

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5

CHOMBEZO: MASSAGE ROOM🔞 SEHEMU YA 21