BEYOND LOVE (ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA 1



SIMULIZI: BEYOND LOVE (ZAIDI YA MAPENZI)

SEHEMU YA 1

Tom aliheshimika na kutisha, hakuna mtu aliyechezea shughuli zake kutokana na uhusiano mzuri aliokuwa nao na viongozi Serikalini, akiwa mdhamini wa Chama Tawala. Hakuna mtu ambaye hakumfahamu, kila alipopita watu walionyeshana vidole, alikuwa na marafiki wengi kupita kiasi. Ilipotokea akaa peke yake kwenye baa au hotelini, ndani ya dakika mbili tayari alishazungukwa na watu, kila mtu akiagiza alichotaka kutumia, kwa Tom kulipa haikuwa tatizo, fedha alikuwa nayo. Tabia hii ilimfanya awe na wapambe wengi kila alikokwenda, akilindwa na watu ambao wala hakuwapa kazi hiyo.

Hayo ndiyo yaliwahi kuwa maisha ya Tom, lakini vitu vyote hivyo havikuwepo tena, vilikuwa vimeyeyuka na yeye kujikuta amelala kitandani kwa miaka mitano bila kuwa na fahamu, akiwa amepooza mwili wote isipokuwa kichwa tu! Marafiki wote aliokuwa nao walimkimbia, mwanzoni kila mtu alifikiri angekufa wiki ya kwanza lakini akaendelea kuwepo mpaka mwaka ukaisha, ukaja wa pili, hatimaye wa tatu akiwa hana fahamu. Fedha zote alizokuwa nazo zikiwa zimetumika kumtibu kwenye hospitali mbalimbali duniani bila mafanikio yoyote, hatimaye mke wake mrembo, Mayasa Kamani ambaye kwa hakika walitumbua maisha pamoja wakati wa raha, akaja kumbwaga kwenye Hospitali ya Muhimbili na yeye kuingia mitini akiwa ameuza kila kitu kilichokuwa kimebaki.

Mama yake Tom, mjane bibi Bhoke Wambura, ilibidi asafiri kutoka nyumbani kwao Tarime kuja kumuuguza mwanaye, naye hakudumu sana akawa amefariki kwa ugonjwa wa shinikizo la damu mwanaye akiwa hana fahamu na kuzikwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye makaburi ya Kinondoni kwani haikuwepo hata senti moja ya kutosha kusafirisha maiti kwenda Tarime, Tom akabaki kitandani peke yake, marafiki zake wala hawakuulizia aliendeleaje na wauguzi wala hawakujishughulisha naye sana wakijua alikuwa ni mtu aliyesubiri siku yake, kwa miaka miwili zaidi aliendelea kulala kitandani.

Ilikuwa ni asubuhi siku ya Jumapili, wodi ya Mwaisela ikiwa kimya kabisa, wagonjwa wakiwa wametulia vitandani mwao. Mwanamke mwembamba mrefu, afya yake ikiwa imedhoofika alikuwa akimgeuza Tom kitandani ili amwoshe sababu alikuwa amejisaidia kwenye mashuka, hakuwa muuguzi bali mtu aliyejitokeza kumtunza Tom baada ya kukosa ndugu hata mmoja. Ghafla alishangaa alipomwona Tom amefumbua macho, lilikuwa ni jambo geni kabisa ambalo halikutegemewa kutokea, akashtuka na kumuachia, Tom akazungusha macho yake huku na kule chumbani na baadaye kumkazia sana macho mwanamke huyo.

“Wee Malaya nani amekuambia uje nyumbani kwangu? Hivi wewe mwanamke husikii? Nilishakuambia sikupendi kwanini unanifuatilia? Ondoka hapa, Mayasa akikuta utasema nini? Unataka kunichonganisha na Mayasa wangu? Ondoka upesi vinginevyo nitakupiga!” Tom aliongea akijaribu kunyanyuka kitandani, akashindwa, hapo ndipo akagundua hakuwa na hisia hata kidogo kuanzia shingoni hadi miguuni, hakuelewa ni kitu gani kimetokea.

“Tom! Tulia kwanza, huelewi kilichotokea ndani ya miaka mitano iliyopita, niko hapa kitandani kwako kwa sababu nilichonacho moyoni juu yako ni zaidi ya neno nakupenda, zaidi ya mapenzi; This is Beyond Love!” Aliongea mwanamke huyo akibubujikwa na machozi.

Tom hakuwa na habari juu ya kilichotokea maishani mwake, hakuelewa alikuwa amelala kitandani bila fahamu kwa muda wa miaka mitano, fikra zake zilimtuma kuhisi alikuwa amelala kitandani nyumbani kwake mahali ambako alishampiga marufuku Mariam kufika. Alipozungusha macho yake huku na kule ndani ya chumba alicholala, aliwaona watu wengine wakiwa juu ya vitanda na harufu ilikuwa mbaya tofauti kabisa na nyumbani kwake, akaelewa alipokuwa amelala ni hospitali, mara moja akaanza kuzivuta kumbukumbu zake juu ya kilichotokea mpaka akajikuta yuko mahali pale.

Picha iliyokuwa kichwani mwake kwa haraka, aliyoikumbuka kama kitu kilichotokea mwisho ni yeye akiwa ndani ya gari lake aina ya Vogue, akiwa amefunga vioo vyote huku akipulizwa na kiyoyozi, muziki laini uitwao Hello wa mwanamuziki Lionel Richie ulikuwa ukipigwa taratibu kutoka kwenye spika ambazo hazikuonekana. Shingoni alikuwa amevaa mkufu uliotengenezwa kwa mchanganyiko wa dhahabu, rubi na Almasi ambao thamani yake ilikuwa milioni ishirini na tano.

Si hivyo tu, usoni kulikuwa na miwani ya jua kutoka Kampuni ya DG, thamani yake ikiwa ni milioni moja saa yake ilikuwa ni ya milioni tano, nywele zake zilikuwa zimetengenezwa na kuwekewa dawa iliyozifanya zimeremete na kuwa na mawimbi, alipojiangalia kwenye kioo kilichokuwa juu mbele yake kwenye gari, alitabasamu na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyomuumba akiwa kijana mwenye kuvutia, yeye mwenyewe aliamini hakuwepo mwanamke wa kupindisha kama angeamua kumtokea.

Akijiangalia kupitia kwenye kioo hicho, alifanikiwa kuona gari nyeusi aina ya Rav 4 ikija nyuma yake, hakutilia maanani sana akiamini mwenye gari alikuwa na safari zake na alipojaribu kuangalia vizuri, alimwona msichana mzuri akiwa amekaa nyuma ya usukani.

Tom alizidi kukanyanga mafuta gari hilo likimfuata kiasi cha mita kumi tu nyuma yake mpaka akafika kwenye lango la kuingilia kwenye jumba lake la kifahari eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, akakanyaga breki na kubonyeza kitufe fulani kando ya mlango ili lango kuu lifungunge aingize gari lake, ghafla bila kutegemea kabla hajakanyaga moto, lango likiwa wazi, alishangaa kuwaona watu wawili waliovaa kininja wakiwa wamesimama kila upande wa gari lake, mmoja akipigapiga dirishani na kumwomba afungue, mshtuko mkubwa ulimpata, akaanza kutetemeka akiwa hajui nini cha kufanya.

Akiwa katika hali hiyo akifahamu kabisa alikuwa ametekwa, mmoja wa watu hao waliotoka kwenye gari lililokuwa nyuma yake, alikipiga kioo cha dirisha kwa kitako cha bunduki, chote kikavunjika na Tom kuwekewa mdomo wa bunduki aina ya SMG shingoni.

“Ndugu yangu, naomba usiniue kama ni gari chukua, niachie roho yangu niko tayari kukuongezea na vito vyote vya thamani nilivyovaa na hata fedha ya mafuta kama utahitaji!”

“Sihitaji fedha yako, nimefuata roho yako!”

“Nani amekutuma?”

“Hilo sio swali!”

Kilichofuata baada ya hapo ni milio miwili ya risasi, moja ikazama kichwani kwa Tom na nyingine shingoni, akaanguka kwenye kiti huku akitokwa damu nyingi. Majambazi wakamchukua na kutupa nje ya gari, wote wawili wakaingia ndani na kuondoka na gari lake kwa kasi ya ajabu, Tom akiachwa amelala ardhini akivuja damu nyingi bila kuwa na fahamu, wakati hayo yakitokea ilikuwa ni saa tatu na nusu ya usiku kwani alikuwa akiwahi nyumbani kuangalia taarifa ya habari ya ITV, saa nne kamili.

Hiyo ndiyo ilikuwa kumbukumbu ya mwisho iliyomwijia kichwani mwake baada ya kujaribu kukumbuka ilikuwaje akawa hospitalini, kichwani mwake alifikiri tukio la kuvamiwa lilitokea jana yake kumbe alikuwa amelala kitandani kwa miaka mitano mfululizo bila kuwa na fahamu akiwa amezungushwa huku

ITAENDELEA...........



TUPATIE NYOTA 5 KWENYE APP YETU KULE PLAY STORE NA KU COMMENT ILI TUPATE SUPPORT YAKO.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

CHOMBEZO: BINAMU 🔞 SEHEMU YA 11

KIJIJINI KWA BIBI SEHEMU YA 1-5

CHOMBEZO: MASSAGE ROOM🔞 SEHEMU YA 21