KOFI LA KISOGO SEHEMU YA 5
“KOFI LA KISOGO”
Na:Arnold Machavo
Mbeya—Tanzania
Sehemu ipatayo ya 05
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
««Ilipokomea...
Waridi aliishia kuangua kicheko kwani Hussein alikuwa mtu wa masihara wakati wote tofauti na muonekano wake. Hata Waridi hakudhania kama alikuwa mtu wa namna hiyo. Au labda ni kila mtu anapotaka kurusha nyavu zake lazima aonekane anajali au mleta faraja na furaha...
TEREMKA NAYO...»»
Siku hazigandi, na ni kwa namna hiyo pia mambo hupita, husalia ama kuja mapya. Vivyo hivyo kwa upande wa Hussein na Waridi urafiki wao ulizidi kustawi na kushamiri kila uchao. Kwa ambaye angelifanikiwa kuwatia machoni basi la hasha angelikataa kuwa walifahamiana kwa muda mfupi. Walikuwa ni marafiki wa miezi kadhaa tuu tena waliofahamiana kwa bahati sana.
Kwa wakati huo Waridi alikuwa ni mtu wa masuala ya urembo wa kike. Kwa siku sita za wiki kila ilipofika mchana alikuwa akielekea kwenye saluni kwa ajili ya kuweka nywele za wateja wake kiustadi.
Hakusalia hapo pekee, pia alibobea katika nyanja za kupamba wanaharusi endapo angekabidhiwa kazi hiyo. Alitamani hata siku moja akiweka mambo yake safi basi afungue saluni yake na kupitia umahiri wake avutie wateja wake sehemu hiyo. Tatizo lilikuwa ni chekeli kwani haikuwa kazi rahisi kama watu wafikiriavyo. Alipodai kuwa anafanya kazi ya kupika vyakula katika mgahawa mkubwa wa mama mdogo yake, alivutiwa mno na kazi hiyo.
Tangu wakiwa wadogo Waridi alipendelea mno kupika chakula hata cha watu wengi. Hiyo ilikuwa kama chachu ya kutamani kujua kupika zaidi tena na tena. Alikuwa amejiegesha pale wakati akiendelea kupambania kupata angalau hata senti kadhaa za kusogeza maisha. Kwa muda aliyofanikiwa kuwepo pale mgahawani alijidhihirisha kuwa ni kweli anajua kupika na kuandaa chakula ambacho kilikubalika na wateja wengi waliyofanikiwa kula. Kiufupi waswahili wangesema anao mkono mzuri wa kuandaa biriani.
Mama mdogo alimsihi asalie pale ili watengeneze kipato wakiwa pamoja lakini Waridi alivutiwa zaidi na mambo ya kucheza na nywele. Mama mdogo alikuwa ameshaona ni jinsi gani wateja wake wengi wanavyosifia mapishi hodari ya chakula wanachokipata. Alitambua ya kuwa endapo Waridi akitimuka pale basi wateja wataona tofauti pia alihofia kupoteza baadhi ya wateja hata kama wangepotea wachache, ilimuumiza mno.
Naam ni kama aliingia ndani ya ufahamu wetu tunaotumia chakula kwa akina mama ntilie, jinsi tunavyohitaji kuganda sehemu moja. Kawaida yetu tulio wengi tunachagua sehemu moja yenye mapishi adimu na bora kisha tunatulia hapo. Siku ukitutibua au mapishi yakabadilika na kupoteza mvuto basi tunahama jumla na kutafuta mahali pengine. Hilo ndilo lilimuwazisha mama mdogo yake Waridi.
Jinsi siku zinavyosogea Waridi alitamani afungue saluni atakayomiliki yeye mwenyewe. Alikuwa mpole kwani pesa ndilo lilikuwa tatizo kubwa lililomkabili kwa wakati ule. Lakini alijikuta anaangukia kwa mtu aliyemtia hamasa, ujasiri na nguvu ya kuthubutu kufanya. Hussein ndiye alifanya yote hayo. Ilimpa moyo kuwa anaweza endao akaweka nia. Kwanza Hussein alimshauri kuwa angeanza na saluni ndogo ili kukuza jina na ujuzi wake kisha aendelee taratibu kwani mazuri mengi hayahitaji haraka.
Wazo hilo ni kama lilimuingia kichwani na kumchangamsha juu ya kuamka mapema kuliko kuendelea kusubiria neema imfikie. Hakuwa na cha kupoteza zaidi ya kufanya hivyo pamoja na changamoto lukuki zilizomkumba. Mgahawani nako hakuacha, aliendelea kupambana ili kupata uzoefu pia. Fursa kama ikionekana ichukue usisubiri mpaka ionekane unayoihitaji, ikija uzeeni je. Waridi kwa wakati huo alijikuta ni kama alihitaji kuwa mpishi hodari na si mtu wa kucheza na nywele. Alikuwa akiwaza juu ya hilo basi anacheka peke yake kama mtu aliyerukwa na akili.
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Ndani ya miezi hiyo Hussein alikuwa na ukaribu mkubwa na Waridi kuliko alivyotarajia yeye mwenyewe. Ingawa alikuwa makini ili kuusoma mchezo katika kusudi la kutorudia kukanyaga kaa la moto kwa mara nyingine kama alivyofanya awali. Kufanya kosa siyo kosa bali kurudia kosa ndiyo kosa lenyewe sasa. Alikuwa mstaarabu ili kuchagua dhahabu katika mawe mengi yaliyotapakaa kila kona kwenye eneo linalomzunguka. Ingawa alisahau kuwa si kila king'aacho ni dhahabu, unaweza kuokota jiwe linalong'aa na ukadhani umepata dhahabu kumbe la.
Kazi yake ndiyo ilikuwa kipaumbele kwanza kwani kitu cha kwanza kutetea ni tumbo maana kukera kwake kila mmoja anatambua. Hiyo ilimfanya aweke juhudi na bidii katika kutafuta vyanzo vingine vya kukusanya chekeli. Licha ya kupata senti kadhaa kutoka kibaruani anakofanya kazi, lakini pia alijishughulisha na kilimo kwani amezaliwa kwenye maisha hayo. Kilimo alichofanya yeye ni kuweka watu wanaomfanyia kazi halafu yeye anafuatilia mwenendo mzima.
Hakuona tabu juu ya namna hiyo, pia alipunguza baadhi ya matumizi yasiyokuwa ya lazima. Tena kwa bahati nzuri au mbaya alikuwa akitumia bia mbili tatu kila akijihisi kuzikumbuka, alijikuta anapata senti nyingi kwa ajili ya starehe hiyo. Mara moja moja akipata wasaa wa kunywa alikuwa anaungana na baadhi ya wafanyakazi wenzake wanaopendelea kunywa. Ukiwasikiliza wanywaji huwa wanasema ni bora kunywa mkuwa wengi tena ndiyo utamu unaongezeka. Hiyo ndiyo sababu hawapendi kunywea majumbani kwao bali huambatana pamoja na kutafuta sehemu tulivu ambayo watakunywa huku wakiendelea na mazungumzo yao.
Siku ziliyoyoma hatimaye Hussein alijikagua na kutosheka katika upembuzi wake yakinifu juu ya kuiokota dhahabu aliyoiona yeye katikati ya mawe. Waliungana na Waridi kwa ajili ya kuiaminisha jamii kuwa inawezekana wakaungana. Hussein aliona kuwa ni mtu aliyebahatika kuupata ubavu wake wa kushoto kabla haujapikiwa supu na kunywewa na mtu mwingine. Alianza kufuata taratibu zote kabla ya kumuiba binti wa watu baada ya kuona amechoka kukaa kwao. Kumpumzisha kwa kumhamishia kwake ndiyo ilikuwa suluhisho pekee.
Zama zilizopita kidogo kipindi fulani hivi kulikuwa na kasumba iliyogandia ndani ya baadhi ya watu wa jamii kadhaa, kuwa ukitaka kumpata mwali fulani hata kama yeye hataki, dada wa watu ananyanyuliwa halafu asubuhi ndoa. Hussein hakuwepo huko wala alifuata kila walichoagiza ili kupata na baraka zao. Naam! baada ya muda mfupi tuu tayari alikuwa ameshajiopolea mwali tena aliyouhitaji. Alionekana kupania mno kuliko hata Waridi mwenyewe.
Hussein alihitaji kuingia ndoa ndoani ili akajionee yeye mwenyewe acha hii tunayosimuliwa huku mitaani halafu tukiingia tunatamani kutoka tena. Kwetu Mbeya ndiyo kuna mazoea sana ya kusema nimeopoa jiko la kupunguzia lile baridi kali hususani la asubuhi. Wanasahau kusema kuwa jiko hilo linaweza kukuunguza vibaya sana na ukabakia na majeraha yasiyopona. Ni vyema tufahamu pia kuwa jiko hilo linatoa baridi lakini pia linaunguza vibaya sana.
Hussein alikabidhiwa dhamana ya kumlea na kumtunza binti wa watu kwa gharama yoyote ile na kuhakikisha anasalia kama alivyotoka kwao. Lakini alipewa ruksa ya kuvuruga na kumpiga binti huyo atakavyo yeye sehemu moja pekee. Aliifahamu yeye mwenyewe, na alisisitizwa asiiache salama hata kidogo kwani angeweza kunyang'anywa mwali huyo kwa kutofanya hivyo. Hata yeye alijikuta anajiaandaa vilivyo kutekeleza matakwa wa wajumbe hao wa nyumba kumi sijui tisa.
Waridi ni ua linalopatikana kwenye bustani nyingi za maua tena limetunukiwa harufu yenye kunukia vyema. Kwa bahati nzuri harufu hiyo unaweza kuinusa vyema ukiwa umefumba macho yote mawili. Nawapongeza akina Waridi wote kwani wanalifahamu hilo. Hussein alijiandaa kufumba macho yake yote mawili ili aweze kuupata msisimko na harufu nzuri kutoka kwa Waridi wake aliyekuwa ameketi jirani yake kufurahia umoja ule..
Tukutane sehemu inayofuata...
ITAENDELEA......
BAKI HAPA HAPA KWENYE APP YETU, MUITE NA MWINGINE.
Maoni
Chapisha Maoni