MCHUNGAJI MCHAWI. EPISODE:10
Story: MCHUNGAJI MCHAWI.
Mtunzi: Nellove
Episode: 10
Ilipoishia...
Mchungaji Joshua alibaki ndani na mtoto hata Hivyo hazikupita dakika nyingi sana sauti ilisikika
"Mamaaaaaa!!!" Kelele hizi zilisikika kisha sauti kali ya kukoroma ilianza kusikika kutoka sebuleni.
Mchungaji alishituka sana hivyo aliinuka haraka na kukimbia hadi sebuleni ili kujua ni kipi kimetokea.
Endelea...
Hatua chache zilizopigwa haraka haraka zilimfikisha sebuleni ambako alimkuta mkewe akiwa chini hajielewi. Moyo wake ulienda mbio japo hakutaka kabisa kuruhusu hofu kuingia ndani yake. Alisogea taratibu hadi mahali alipokuwepo mke wake,,, alichuchumaa na kumchunguza kidogo kwa kumgusa gusa maeneo ya shingoni na kifuani.
"Mmmh!!" Mchungaji aliguna na kumgusa tena maeneo hayo kisha alisimama,, mikono kaitupa kiunoni.
Uchunguzi wa haraka uliofanyika na mchungaji ulitoa jibu kuwa mke wake hakuwa anahema wala kupumua,, hii hali ilimpa wasiwasi sana. Mchungaji Joshua alipigwa na butwaa hata hivyo alikumbuka kuwa mkewe ana historia ya kusumbuliwa na tatizo la kifafa lakini sasa mazingira ya tukio hili lililomkuta mke wake leo hayakuwa mazingira ya kawaida,,, kusikika kwa sauti kali ya kelele pamoja na kukoroma ndani ya muda mfupi uliopita vilimchanganya Mchungaji!!
"Kimemkuta nini?"
Alitafakari cha kufanya ndipo wazo la kumuombea mke wake lilipokuja. Alianza kufanya maombi lakini hata kabla ya dakika tatu ilisikika sauti ya mtoto chumbani akilia sana. Hakutaka kujali sana,, aliendelea na maombi lakini kadri alivyoendelea ndivyo mtoto naye alivyoongeza kilio. Hakuwa na budi kuachilia zoezi la maombi na kwenda chumbani kumuangalia mtoto wake mdogo kabisa.
Mtoto alikuwa analia sana na hakutaka kutulia hata kidogo. Nguvu kubwa ilitumika kumbembeleza lakini wapi,,, pengine alihitaji maziwa lakini Mama yake alikuwa chini hajielewi,, maziwa yangetoka wapi?? mchungaji Joshua atafanya nini???
Aliendelea kumbembeleza mtoto wake hadi wakati alipotulia kidogo. Basi alimlaza kitandani na kurudi sebuleni ili kuendelea na maombi. Alifanya maombi kadri alivyoweza lakini hapakuwa na mabadiliko ama mafanikio yoyote. Mke wake hakuamka wala kutikisa kidole.
Hili jambo lilimshangaza kwani watu wengi kanisani huwaponya kwa kuwagusa na kutamka mara moja tu,, sasa iweje leo maombi makali na ya muda mrefu kwa mkewe yasifue dafu? Alishangaa mno.
Kule chumbani mtoto alianza kulia tena na pengine ni afadhali mara ya kwanza kuliko sasa kwani wakati huu alikuwa analia kwa nguvu sana utadhani kuna kitu kinamfinya ama kumtisha. Mchungaji aliamini ni njaa inamsumbua,, lakini sasa atanyonya wapi?? Pengine angekuwa mkubwa angemkorogea uji sasa ndio kwanza ana miezi mitatu,,, hakika huu ulikuwa mtihani mzito kwa mchungaji,,
ibaki kusimuliwa na Nellove,, omba yasikukute.
"Ee Mungu wangu,, unataka kunifundisha jambo gani Baba???" Alimhoji Mwenyezi akiamini kila jambo linalotokea lina kusudi fulani. Sasa je kusudi la jambo hili ni lipi???
Hakuacha kuomba kabisa lakini waweza sema labda Mungu wake alikuwa mbali ama amemgeuzia kisogo ndani ya siku hii kwani kadri muda ulivyosonga basi lile jambo liliendelea kuwa tatizo kubwa kuliko awali na mafanikio hayakuonekana.
Usiku mzima hakulala,, alishindia jukumu la maombi bila kusahau kumbembeleza mtoto aliyekuwa analia kila baada ya dakika chache sana.
Usiku ulikuwa mrefu sana lakini haikuwa sababu ya asubuhi kutokufika. Ilikuwa asubuhi ya siku nyingine,, siku ambayo iliendelea kulibeba tatizo lile lililomkumba ghafla mchungaji Joshua. Uchovu pamoja na kukauka kwa sauti vyote hivi vilitokea kwa mchungaji kutokana na kufanya maombi kwa muda mrefu. Vivyo hivyo upande wa mtoto sauti ilipotea kabisa kwani takribani masaa 6 amelia.
Hakuwa na wazo lingine zaidi ya lile la kwenda kukoroga uji kidogo ili ajaribu kumnywesha mtoto japo alijua fika hakuwa na umri unaoruhusu kuingiza chochote tofauti na maziwa ya Mama yake. Alikoroga haraka na kuanza kumpatia kidogo kidogo,,, mtoto alipata kumeza na alipotosheka basi ikawa ahueni kwani usingizi ulimbeba muda huohuo. Faraja ya kiasi fulani ilitambaa moyoni mwa mchungaji Joshua,,, alimlaza mtoto wake.
Baada ya hapo alirudi sebuleni na kuanza tena kazi ya maombi bila kukata tamaa ama kuwa na wazo lingine pengine hata la kumpeleka hospitalini. Hata hivyo inashangaza jinsi mchungaji Joshua alivyoamua kushughulika mwenyewe bila kumshirikisha mtu yeyote ama kumpeleka popote,, inashangaza.
Aliendelea na maombi ila hapakuwa na tofauti yoyote na awali,,, bado Mama David alikuwa chini hajiwezi ,,nao muda ulienda mbele hadi ilipofika majira ya saa 1 usiku. Majukumu yalikuwa mawili lakini utadhani ni milioni mbili na yalishamuelemea mchungaji. Jukumu la kumuombea mke wake na kumbembeleza mtoto.
Alikaa sebuleni akimbembeleza mtoto huku anamtazama mke wake aliyekuwa chini. Machozi yalimtoka akimsihi MUNGU wake kumpa msaada katika hili,, kama sio kumuamsha mke wake basi amtulize mtoto wake asilie lakini mafanikio hayakuwepo.
"Ulifanya njia mahali ambapo hapakuwa na njia,, watoto wako walipata kupita salama. Ee Baba yangu wa mbinguni naomba nioneshe njia na univushe salama" alitamka akiwa amechoka kimwili na kiroho,, nafsi ya kukata tamaa ilibisha hodi.
"Mwanangu nyamaza basi,, Mama yako ataamka" alisema hayo utadhani mtoto anaelewa.
Alisimama na kuanza kutembea tembea naye kwa dakika kadhaa hadi wakati alipositisha zoezi hili kutokana na tetemeko la ghafla lililounguruma kwa nguvu ya ajabu eneo lile,, nyumba ilitikisika. Hakukaa sawa taa zilizima nyumba nzima na giza kubwa lilitamalaki. Moyo wa mchungaji ulidunda kutokana na hayo yote na namna yalivyotokea. Hofu ilitanda zaidi muda aliposikia sauti kutoka chumbani kwake.
"Joshuaaa!!!" Sauti hii iliambatana na upepo uliokuwa unavuma kistaarabu. Mchungaji hakujua ni nani anamuita.
Alibaki ameduwaa kiasi cha kutoisikia hata sauti ya mtoto anayelia. Sekunde chache yule mtoto alinyamaza ghafla na kufanya ukimya uwe mkubwa mahali pale.
'Kudu!! kudu!! kudu!!!' moyo ulidunda.
Basi baada ya hayo yote muda mfupi sana baadaye ilisikika sauti ya mlango ukiashiria kuna mgongaji. Alishituka hata hivyo hakutaka kwenda moja kwa moja kwani hakujua ni nani anagonga,, alisikilizia kwa sekunde chache.
Mlango uligongwa tena.
Mchungaji Joshua aliamua kutoka ila alitoka akiwa na wasiwasi mkubwa,, mkononi mwake alimpakata mtoto wake vilevile.
Alipofungua mlango tu macho yake yalitua juu ya wazee watatu waliokuwa hapo nje wanamtazama.
"""""""""""""""""""""""""""""''''''''''''''''''''''''""""""""""""""""""""""""""'''""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""
| 🇹🇿JAMANI KUMBUKENI MCHUNGAJI
| JOSHUA ATAKUWA MCHAWI NA HILI
| LIMEDHIHIRISHWA KWENYE SEHEMU
| YA KWANZA KWA MAANA SIMULIZI HII
| IMETUMIA MUUNDO REJEA.
| YANI NIMEWAONESHA ALIVYOKUWA
| ANAFANYA MAMBO YAKE KICHAWI NA
| SASA NAWAPITISHA KATIKA MATUKIO
| YATAKAYOFANYA YEYE KUWA
| MCHAWI.
|
| REJEA SEHEMU YA KWANZA
'''''""""""""""""''""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""""''''""'''''''''"'''''''''''""""
ITAENDELEA.....
BAKI HAPA HAPA KWENYE APP YETU, MUITE NA MWENZAKO.
Maoni
Chapisha Maoni